WAKUU WA TAASISI ZA SERIKALI WAHIMIZWA KUTENGA BAJETI YA MICHEZO - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Tuesday, 15 August 2023

WAKUU WA TAASISI ZA SERIKALI WAHIMIZWA KUTENGA BAJETI YA MICHEZO

Katibu Mkuu Ikulu Bw. Mululi Majula Mahendeka akiongea na watumishi wanamichezo wakati wa uzinduzi wa bonanza la Michezo ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) kwa niaba ya Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Dkt. Moses Kusiluka Agosti 12, 2023 jijini Dodoma.

Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Saidi Yakubu akiongea na watumishi wanamichezo wakati wa uzinduzi wa bonanza la Michezo ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) Agosti 12, 2023 jijini Dodoma.

Na Eleuteri Mangi, WUSM, Dodoma

WAKUU wa taasisi za Serikali nchini wamehimizwa kutenga bajeti kwa ajili ya michezo katika maeneo yao ya kazi na kuwapa watumishi ruhusa kushiriki michezo na mashindano mbalimbali nchini.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu Ikulu Bw. Mululi Majula Mahendeka wakati wa uzinduzi wa bonanza la Michezo ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) kwa niaba ya Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Dkt. Moses Kusiluka Agosti 12, 2023 jijini Dodoma.

“Michezo ni sehemu ya kazi, hivyo basi naelekeza wakuu wa taasisi wote watenge bajeti kwa ajili ya michezo ikiwa ni pamoja na kuwapa watumishi ruhusa kuhudhuria michezo na mashindano mbalimbali kama ilivyobainishwa kwenye kanuni za utumishi wa umma” amesema Bw. Mahendeka.

Ameongeza kuwa malengo ya serikali kuanzisha michezo ni kuboresha utendaji kazi unaojali matokeo na watumishi wa umma kuongeza bidii katika kutekeleza shughuli za umma ili kufikia malengo ambayo nchi imejiwekea.

Bw. Mahendeka amesema kuwa Serikali ilianzisha taasisi ya SHIMIWI kusimamia michezo katika Wizara na Idara za Serikali ambayo imekuwa chachu ya kujenga ari na mtindo bora wa maisha miongoni mwa watumishi ili kutoa huduma bora kwa wananchi na kujenga ushirikiano na umoja miongoni mwao.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Saidi Yakubu amesema kuwa dhima ya Wizara hiyo ni kujenga taifa lenye ushindani kwenye sekta za Utamaduni, Sanaa na Michezo na hiyo ni wizara ya kuwaondolea watu msongo wa mawazo “stress” kwa kuwaletea Watanzania furaha.

Katika kuendeleza michezo nchini, Bw. Yakubu amesema wizara hiyo inasimamia ujenzi wa kituo cha mazoezi na eneo la kupumzikia wananchi katika eneo la Nanenane jijini Dodoma kinachoatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 18 na ujenzi huo utagharimu takriban bilioni 22 na kutakuwa na viwanja vyote vya michezo ikiwemo mpira wa wavu, mpira wa kikapu, mpira wa netiboli na viwili vya mpira wa miguu.

“Hilo ni eneo lenu wote, SHIMIWI, watumishi wa umma, wakazi wa mkoa wa Dodoma, hili ni eneo ambalo wananchi wote wanakwenda kupumzika na kufanya mazoezi” amesema Bw. Yakubu.

Akiwakaribisha watumishi mkoani humo, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule amesema viongozi wa kitaifa akiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan wanasisitiza watanzania kufanya mazoezi na kushiriki michezo katika maeneo yao ili kupunguza magonjwa yasiyoambukiza.

Aidha, Senyamule amesema mkoa huo unasisitiza michezo kupitia makundi mbalimbali wakiwemo watumishi wa umma, wanawake, wafanyabiashara na wakati mwingine wabunge wakiwa kwenye vikao vya Bunge ili kutekeleza maelekezo ya Serikali na kujenga afya za watanzania.

Naye Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora Bw. Juma Mkomi amesema kuwa waajiri katika Wizara na taasisi mbalimbali wanapaswa kusisitiza watumishi kufanya mazoezi katika maeneo yao ya kazi angalau mara moja kwa wiki ili kujenga miili sawa na kuwa na umoja katika kazi na kujenga afya zao.

Akimkaribisha Mgeni Rasmi katika ufunguzi huo, Makamu Mwenyekiti wa SHIMIWI Taifa Bw. Michael Masubo ameishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kuweka mkazo katika michezo ikiongozwa na mwanamichezo namba moja Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikikisha michezo mahali pa kazi inafanyika ipasavyo.

Michezo ya SHIMIWI mwaka huu inatarajiwa kufanyika mkoani Iringa kuanzia Septemba 27 hadi Oktoba 14, 2023 ambapo watumishi watashindana katika michezo ya mpira wa miguu, netiboli, kuvuta kamba, riadha, mbio za baiskeli, karata, draft, vishale na bao.

No comments:

Post a Comment