Na Joachim Mushi, Dar
MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema mvua za Juu ya Wastani hadi Wastani zinatarajiwa katika maeneo mengi ya mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, kusini mwa mkoa wa Simiyu, kaskazini mwa mkoa wa Kigoma, Dar es Salaam, Tanga, Pwani (ikiwemo visiwa vya Mafia), kaskazini mwa mkoa wa Morogoro na pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba katika msimu wa mvua za Vuli, 2023.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC), Dkt. Ladislaus Chang’a, wakati akizungumza na vyombo vya habari kuhusiana na mwelekeo wa msimu wa mvua za Vuli zinazotaraji kuanza Oktoba hadi Disemba 2023.
Akifafanua zaidi, Dkt. Chang’a alisema maeneo ya mikoa ya Mara, kaskazini mwa Mkoa wa Simiyu, Arusha, Manyara na Kilimanjaro yanatarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani na uwepo wa El-Niño. Alifafanua kuwa kutokana na uwepo wa El-Nino vipindi vifupi vya mvua vinatarajiwa kujitokeza pia kwa mwezi Septemba, 2023 katika baadhi ya maeneo nchini.
Aliongeza kuwa mvua za Vuli, 2023 zinatarajiwa kuanza rasmi wiki ya nne ya mwenzi Septemba hadi wiki ya kwanza ya mwezi Oktoba, 2023 katika mkoa wa Kagera na kutawanyika katika maeneo mengine katika wiki ya pili ya mwezi Oktoba, 2023. Mvua za Vuli 2023 kwa maeneo hayo zinatarajiwa kuendelea hadi mwezi Januari, 2024.
“Mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya nne ya mwezi Septemba, 2023 katika maeneo ya magharibi mwa Ziwa Victoria na kusambaa katika maeneo mengine mwezi Oktoba, 2023. Kwa kawaida mvua za Vuli huisha mwezi Disemba, hata hivyo msimu huu mvua za nje ya msimu zinatarajiwa kuendelea mwezi Januari, 2024. Ongezeko la mvua linatarajiwa mwezi Disemba, 2023”. Alisema Dkt. Chang’a.
Dkt. Chang’a alitoa wito kwa wananchi kufuatilia taarifa za utabiri wa saa 24, siku 10, mwezi natahadhari zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania ikizingatiwa kuwa mwelekeo wa mvua uliotolewa ni kipindi cha msimu wa miezi mitatu, hivyo viashairia vinavyochangia mwenendo wa mifumo ya mvua na mabadaliko ya muda mfupi utazingatiwa katika uchambuzi wa utabiri wa muda wa kati na mfupi.
Pamoja na hayo, Dkt. Chang’a ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC) alisisitiza kuwa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania itaendelea kufuatilia mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na kutoa mirejesho ya mwelekeo wa mvua nchini kadri inavyohitajika. Aidha, wadau wanashauriwa kuwasiliana na Mamlaka ili kupata taarifa mahsusi za utabiri wa msimu ili kukidhi mahitaji maalum katika sekta zao.
Msimu wa Mvua za Vuli ni mahususi kwa maeneo ya nyanda za juu kaskazini mashariki (Mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro), pwani ya kaskazini (kaskazini mwa mkoa wa Morogoro, mikoa ya Pwani (ikijumuisha visiwa vya Mafia), Dar es Salaam, Tanga pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba), ukanda wa Ziwa Victoria (Mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Mara) pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma.
Wadau wa sekta mbalimbali za kiuchumi na kijamii zikiwemo Kilimo, mifugo, uvuvi, Usafiri na Usafirishaji, Utalii na Wanyamapori, Nishati, Maji na pamoja na Madini wanashauriwa kupanga na kutekeleza shughuli zao kwa kuzingatia taarifa mahususi za hali ya hewa zinazotolewa na TMA.
No comments:
Post a Comment