Mkandarasi wa ujenzi wa Shule Shikizi ya Msingi ya Ponde iliyopo Kijiji cha Ponde Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, Japhet Mikakalo (kulia), akiwaongoza viongozi wengine kukagua ujenzi wa shule hiyo jana jijini Dar es Salaam. Kutoka kushoto ni Ramadhan Abdu fundi Mjenzi wa shule hiyo, Mtunza stoo wa vifaa vya ujenzi wa shule hiyo, Mwalimu Allan Shemboza na Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Ponde, Omari Mbitemomo.
Na Dotto Mwaibale, Temeke
SHILINGI Milioni 800 zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya kujenga Shule
Shikizi ya Msingi ya Ponde iliyopo Kijiji cha Ponde Halmashauri ya Manispaa ya Temeke
jijini Dar es Salaam zinakwenda kuwakomboa wanafunzi wa kijiji hicho ambao
walikuwa wakitembea umbali mrefu kwenda maeneo mengine kusoma.
Wanafunzi hao walikuwa wakitembea zaidi ya kilometa tatu kila siku kwenda Kijiji
cha Mikwambe na Mkokozi jambo ambalo lilikuwa likiwapa adha kubwa ya kutembea
umbali huo kwa kwenda na kurudi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana
akiwa na viongozi wa kijiji hicho
na mkandarasi anayejenga shule hiyo wakati wa ukaguzi wa ujenzi wa shule hiyo,
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi ya Toangoma, Wande Mkonyi alianza kwa kutoa
shukurani nyingi kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha hizo kwa
ajili ya kutekeleza mradi huo mkubwa wa ujenzi wa shule hiyo ya Ponde.
Alisema shule hiyo ya Ponde itakuwa shule kubwa yenye madarasa 22 kati ya hayo mawili yatakuwa kwa
ajili ya elimu ya shule ya Chekechea ambayo itakuwa na bembea na vifaa vya
michezo, kutakuwa na jengo la utawala, kichomea taka, maktaba, nyumba ya walimu
ambayowataishi walimu wawili ‘Two in One’ na vyoo.
Alisema ujenzi wa shule hiyo unatokana na wingi wa wanafunzi katika shule
tatu ikiwemo Shule Mama ya Toangoma ambayo inawanafunzi 3761, Shule ya Msingi
Mikwambe ambayo ina watoto 3200 na Shule ya Msingi Mkokozi yenye wanafunzi
zaidi ya 2900 hali ambayo inaonesha jinsi watoto walivyokuwa wakisoma katika
mazingira magumu ya mrundikano hivyo kukamilika ujenzi wa shule hiyo itakuwa
mkombozi mkubwa sana kwao.
Mkonyi alitumia nafasi hiyo kuwashukuru Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya
ya Temeke, Mkuu wa Wilaya Mbunge, Diwani
na viongozi wote wa Kijiji cha Ponde akiwepo Mkandarasi anayejenga shule hiyo
Japhet Mikakalo, Mwenyekiti wa Bodi ya Shule hiyo na kamati ya ujenzi kwa ushirikiano mkubwa ambao umeufanya ujenzi
wa shule hiyo kuwa wa kasi na viwango vya hali ya juu.
Mkandarasi wa mradi huo Japhet Mikakalo alisema licha ya kuwepo kwa
changamoto za hapa na pale lakini kutokana na ushirikiano mkubwa uliopo kwa
viongozi wote waliotajwa hapo juu pamoja na wananchi umefanikisha hatua hiyo ya
kazi yenye ufanisi wa hali ya juu.
'' Binafsi nimshukuru sana Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Temeke na
Afisa Elimu Msingi kwa kutupa ushirikiano katika utekelezaji wa mradi huu ambao
unakwenda kuwakomboa watoto wetu kwani miradi ya namna hii kwa kuaminiwa na
Serikali nimekuwa nikiitekeleza kwa viwango kulingana na thamani halisi ya
fedha zilizotolewa,'' alisema Mikakalo.
Mikakalo alisema mwaka wa fedha2022/ 2023 ulipokuwa umeisha kulikuwa na
changamoto ya mfumo wa kifedha na kusababisha shughuli nyingi kukwama kwa
kusubiri malipo lakini wao waliendelea kufanya kazi kutokana vyanzo vingine ili kwenda na kasi ya
kukamilisha mradi huo kwa wakati kwa ajili kuwasaidia wanafunzi hao kuondokana
na adha ya kutembea umbali mrefu kwenda shuleni.
Mwenyekiti wa Bodi ya Shule ya Msingi Toangoma, David Kulinga ambaye pia ni
Mwenyekiti wa kamati ya ujenzi wa shule hiyo ya Ponde alisema ujenzi wa shule
hiyo ulianza Juni 27, 2023 na unatarajia kukamilika mwezi ujao na kuwa
unakwenda vizuri na wana amini utakuwa tayari ndani ya wakati kutokana na kuwa
katika hatua nzuri ya upauaji .
'' Matumaini ya kukamilisha kazi hii kwa muda uliopangwa yanatokana na kazi kubwa
anayoifanya mkandarasi wetu Mikakalo ambaye wakati wote yupo eneo la ujenzi
kuhakikisha kazi zinafanyika jambo ambalo linatutia moyo sana,'' alisema
Kulinga.
Kulinga naye alitumia nafasi hiyo kumshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan
kwa kazi kubwa anayoifanya si kwa Kata ya Toangoma bali kwa nchi nzima ya
kujenga miundombinu ya shule.
Alisema wakiwa kama watendaji waliopo chini wana kila sababu ya kuunga
mkono jitihada hizo za Serikali kwa kusimamia utekelezaji wa miradi hiyo ambayo
ni mkombozi katika kupata elimu watoto na inakamilika kwa thamani ya fedha
iliyokusudiwa na si vinginevyo.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Ponde, Omari Mbitemomo alisema mtaa huo ni kati ya mitaa 14 ambayo inaunda Kata ya Toangoma hivyo kupatikana kwa shule hiyo kuna kwenda kuwakomboa watoto wa eneo hilo ambapo alitumia nafasi hiyo kuwaomba wananchi kutunza miundombinu ya shule hiyo ikiwa ni moja ya njia ya kumheshimisha Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ambaye ametoa fedha za ujenzi wa shule hiyo.
Alisema watoto wa eneo hilo walikuwa na changamoto kubwa ya kwenda kusoma mitaa ya Mwampembe eneo la Kizuda na Mikwambe ambapo walikuwa wakitembea umbali wa kilometa zaidi ya tatu na wengine walikuwa wakienda Shule ya Msingi, Mkokozi ambapo walikuwa wakitembea umbali wa zaidi ya kilometa zaidi ya mbili na nusu.
No comments:
Post a Comment