Mkuu wa Wilaya ya Singida, Mhandisi Paskas Muragili akihutubia wakati akifungua mafunzo ya usambazaji na matumizi ya matokeo ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 kwa viongozi hao yaliyofanyika Shule ya Sekondari ya Mwenge iliyopo Manispaa ya Singida Julai 8, 2023 kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba.
Na Dotto Mwaibale, Singida
VIONGOZI na watendaji wa ngazi mbalimbali za utawala
katika Wilaya ya Singida na Halmashauri ya Manispaa ya Singida mkoani hapa wametakiwa kutumia matokeo ya Sensa ya
watu na makazi ya mwaka 2022 katika kufanya maamuzi na kutathmini utekelezaji
wa mipango mbalimbali ya maendeleo.
Ombi hilo limetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Singida,
Mhandisi Paskas Muragili wakati akifungua mafunzo ya
usambazaji na matumizi ya matokeo ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 kwa
viongozi hao yaliyofanyika Shule ya Sekondari ya Mwenge iliyopo Manispaa ya
Singida leo Julai 8, 2023 kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter
Serukamba.
"Mafunzo haya
yanatekelezwa kwa mujibu wa Mpango kazi wa Usambazaji na Mafunzo ya Matumizi ya
Matokeo ya Sensa unaotokana na maono ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais
Dkt. Samia Suluhu Hassan ni dhahiri kuwa si kila mdau tukiwemo miongoni mwetu
tunafahamu vyema kutumia matokeo ya Sensa katika kufanya maamuzi na kutathmini
utekelezaji wa mipango mbalimbali ya maendeleo ambapo Serikali iliona ni vyema
kutoa mafunzo haya kwa wadau mbalimbali katika ngazi mbalimbali za kiutawala
kuhusu namna ya kutumia matokeo ya Sensa," alisema Mragili.
Alisema mafunzo hayo kwa namna moja au nyingine
yatawapa uwezo wa kushiriki katika kufanya maamuzi yanayohusu sera na mipango
ya maendeleo ya wananchi kwa kuwa wapo karibu nao, hivyo kutumia matokeo ya
Sensa watatekeleza majukumu yao vizuri ya kuwawakilisha wananchi.
Mragili alitumia nafasi hiyo
kutoa shukrani zake za dhati kwa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya wa Singida kwa
ushirikiano na Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Singida na Ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa kuratibu vyema
maandalizi ya mafunzo hayo.
Meneja wa Takwimu Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Mkoa wa Singida, Naing'oya Kipuyo
akizungumza kwa niaba ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Dk.Albina Chuwa alisema
mafunzo hayo ni mfufulizo wa mafunzo ya matumizi ya matokeo ya Sensa kwa
makundi mbalimbali katika jamii
yanayoendeshwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa
Serikali Zanzibar na kuwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mpangokazi wa Usambazaji
na Mafunzo ya Matumizi ya Matokeo ya Sensa ya Mwaka 2022
"Hadi sasa, mafunzo kama haya yamefanyika kwa
makundi mbalimbali yakiwemo viongozi wa ngazi za chini katika mikoa ya Dar es
salaam, Dodoma, Kigoma na Morogoro pamoja na mikoa mitano ya Zanzibar,"
alisema Kipuyo.
Kipuyo aliyata makundi mengine yaliyopata mafunzo hayo
kuwa ni Wakurugenzi wa Sera na Mipango wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, viongozi wa mikoa, Kamati za
Sensa za Mikoa na wajumbe wa Sekretarieti ya Mikoa ya Lindi, Mtwara,Pwani,Singida
na Wilaya ya Iramba.
Alisema mafunzo mengine yamefanyika katika ngazi ya
mkoa katika mikoa ya Mbeya na Ruvuma. Hivi sasa tunaendelea na mafunzo ya aina
hii katika ngazi ya Halmashauri na majiji katika mikoa ya Dar es salaam na
Dodoma.
Alitaja kundi jingine lililofaidika na mafunzo hayo
kuwa ni vyombo vya habari ambapo
wahariri wa habari wa redio zaidi ya 120 nchini pamoja na wanachama 25 wa Chama
cha Waandishi wa Habari Mkoa Singida na kuwa yataendelea kufanyika kwa ngazi
zote za utawala na kuhusisha makundi kama vile viongozi wa siasa, dini, mila na
destruri, Asasi za Kiraia, sekta binafsi, taasisi za elimu ya juu na za
kitafiti, Watu Wenye Ulemavu,vyombo vya habari na wananchi wa kawaida.
Kipuyo alisema
madhumuni ya mafunzo hayo ni kusambaza matokeo
ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 na kuwajengea uwezo wadau wote wa
namna ya kutumia matokeo hayo katika kutekeleza majukumu yao ya uongozi na
utendaji katika Serikali Kuu na Mamlaka za Serikali za Mitaa, Sekta Binafsi
ikiwemo biashara na uwekezaji, tafiti, utoaji huduma mbalimbali zikiwemo za
kijamii na uchumi.
Alisema kufanya hivyo
kutasaidia kuongeza uwazi na
kupanua wigo wa matumizi ya Matokeo ya Sensa kwa Serikali,
Sekta Binafasi na wananchi kwa ujumla ili kupanga mipango jumuishi kwa maendeleo endelevu.
Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa
Singida, Dk. Fatuma Mganga alisema kuhusu maelekezo ya Serikali juu ya matumizi ya matokeo ya
Sensa, mkoa huo umejipanga kuhakikisha mipango yao na programu zao zote za maendeleo zinapangwa
kwa kuzingatia matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi, Sensa ya Majengo na Sensa ya
Anwani za Makazi ya Mwaka 2022.
"Nieleze
kuwa katika mipango na programu zetu za mwaka wa fedha 2023/24 zimezingatia
matokeo ya Sensa na Takwimu nyingine zinazozalishwa na Ofisi ya Taifa ya
Takwimu," alisema Dk.Mganga.
Alisema
mbali ya kutekeleza maelekezo ya Serikali, mkoa umeweka msisitizo wa matumizi
ya matokeo ya Sensa kwa lengo la kuhakikisha kuwa mipango na programu hizo
zinajibu changamoto mbalimbali ambazo wananchi wanapambana nazo katika maisha
yao ya kila siku.
Aidha,
Dk. Mganga alisema matumizi ya matokeo hayo ya sensa ni kuhakikisha wananchi
wanapata huduma stahiki kwa wakati na zenye ubora unaozingatia mahitaji halisi
kulingana na idadi yao, jinsi yao, kuzingatia mahitaji maalum ya makundi
mbalimbali katika jamii na hali ya mazingira wanamoishi.
Alisema mafunzo hayo ni muhimu sana kwa sababu yanawajengea uwezo wa kuyatafsiri na kuyatumia matokeo ya Sensa ipasavyo na hatimae kukuza uchumi wa mkoa, kuongeza na kuimarisha upatikanaji wa huduma za jamii kwa wananchi na kuchagiza harakati ya kupambana na maadui watatu ambao ni ujinga, maradhi na umasikini.
Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Dk. Fatuma Mganga, akizungumza kwenye mafunzo hayo.
No comments:
Post a Comment