Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa-TAMISEMI (ELIMU) Dk. Charles Msonde (katikati), akizungumza na Wanafunzi wa Sekondari ya Mwanzi iliyopo Manyoni mkoani hapa wakati wa siku ya kwanza ya ziara yake ya kikazi ya kutembelea na kukagua ujenzi wa shule kupitia mradi wa BOOST aliyoianza jana Julai 9, 2023.
Na Dotto Mwaibale, Singida
NAIBU Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa-TAMISEMI
(ELIMU) Dk. Charles Msonde amezihimiza Halmashauri za Wilaya kote nchini
kukamilisha miradi ya ujenzi wa shule zinazojengwa kwa fedha za BOOST ili
Tanzania iwe nchi ya mfano kwa mataifa mengine kuja kujifunza mafanikio ya
sekta ya elimu kutokana na kukamilika kwa miradi hiyo kwa kiwango cha juu.
Dk. Msonde ameyasema hayo leo Julai 9, 2023
wakati alipotembelea miradi ya ujenzi wa shule za msingi na sekondari za
Halmashauri za wilaya za Manyoni, Itigi, Ikungi na Singida.
Msonde alisema Halmashauri zihakikishe
zinakamilisha miradi ya BOOST ifikapo Julai 30, 2023 ili wanafunzi wajiunge
katika shule na kuanza kutumia majengo hayo.
'Tanzania itakuwa nchi ya mfano katika uboreshaji
wa miundombinu ya shule na nina amini kwa nchi nyingine za Afrika na mataifa
mengine yatakuja kujifunza kuona jinsi tulivyofanikiwa kutokana na kazi kubwa
na nzuri aliyoifanya Rais wetu Dk.Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi
kwenye sekta ya elimu," alisema Dk.Msonde.
Alisema fedha zilizopokelewa kwa awamu ya
kwanza ambazo zimetolewa kama mkopo na
Benki ya Dunia (WB) kwa ajili ya kutekeleza mradi huo wa BOOST kwa miaka mitano ni Sh. Trilioni 1.15 na umelenga kuimarisha
ujifunzaji katika elimu ya awali na msingi.
Dk.Msonde alisema kumekuwa na ongezeko kubwa la
wanafunzi wanao maliza kidato cha nne kwenda cha tano na sita hivyo kwa kuwa
Serikali ni sikivu ikaona ni vema kujenga shule hizo kwa ajili ya wanafunzi
hao.
Katika ziara hiyo Dk.Msonde alizipongeza
halmashauri za Manyoni, Ikungi na Singida kwa kuzisimamia vizuri fedha hizo na
kutekeleza miradi hiyo kwa viwango na kwa wakati na akahimiza kuongeza kasi
zaidi iliikamilike ndani ya muda uliopangwa.
"Nawaombeni ongezeni kasi ya kukamilisha
mradi huu kwa kuweka mafundi wengi ambao watakuwa wakishambulia kila kona
badala ya kusubiri mafundi waliopo kufanya kazi hiyo peke yao huku kasi yao
ikiwa ndogo," aliongeza Msonde.
Baadhi ya shule alizotembelea na kukagua ujenzi
huo ni Shule ya Sekondari ya Mwanzi iliyopo Manyoni, Shule mpya ya Msingi ya
Igonoa iliyopo Itigi, Shule ya Sekondari ya Mwanamwema Shein ambayo ipo Kata ya
Mgori Wilaya ya Singida na Shule ya Msingi Minyaa iliyopo Kata ya Kinyeto
Wilaya ya Singida.
Kesho Dk.Msonde atamalizia ziara yake mkoani hapa
kwa kukagua ujenzi wa shule hizo katika Wilaya ya Mkalama na Iramba na
kuzungumza na watumishi wa sekta ya elimu na kufanya majumuhisho ya ziara hiyo.
No comments:
Post a Comment