TANZANIA kupitia Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Dkt. Ladislaus Chang’a, amechaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi, “Intergovernmental Panel on Climate Change (IPCC)”, katika Mkutano wa 59 wa IPCC (IPCC-59) unaoendelea katika Ofisi za Umoja wa Mataifa Jijini Nairobi, Kenya kuanzia tarehe 25 hadi 28 Julai, 2023.
Dkt. Chang’a amechaguliwa katika nafasi hiyo katika uchaguzi wa viongozi wa IPCC (IPCC Bureau) uliofanyika tarehe 26 Julai, 2023. Wagombea katika nafasi ya Makamu wa Mwenyekiti wa IPCC walikuwa jumla nane, kutoka Tanzania, Australia, Cuba, Eswatini, Germany, Hungary, Urusi na Afrika Kusini. Katika kinyang’anyiro hicho zilihitajika nafasi tatu na waliochaguliwa ni Tanzania, Cuba na Hungary.
Aidha, Dk. Chang’a kwa kushirikiana na Maafisa wengine wa ngazi ya juu wa IPCC waliochaguliwa katika Mkutano huo wataiongoza IPCC katika mzunguko wake wa saba wa tathmini ya sayansi ya mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi ambao utadumu kwa takribabi miaka mitano hadi saba kuanzia mwaka huu 2023.
Dkt. Chang’a ni Mtaalamu mbobezi wa taaluma ya hali ya hewa kwa takribani miaka 30. Kwa zaidi ya miaka kumi (10), Dkt. Chang’a ametoa mchango mkubwa katika kutetea maslahi ya Tanzania, Afrika na Nchi zinazoendelea katika tafiti na tathmini za sayansi ya mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi na athari zake, pamoja na kuhakikisha kuwa Afrika na nchi zinazoendelea zinapewa kipaumbele katika juhudi na hatua zinazopaswa kuchukuliwa na jumuiya ya kimataifa katika kukabiliana na athari hizo kupitia majadiliano ya IPCC na Mkataba wa Mfumo wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (United Nations Framework Convention on Climate Change-UNFCCC).
No comments:
Post a Comment