Mbunge wa Singida Mjini, Musa Sima akiwahutubia Wananchi wa Kata ya Unyamikumbi iliyopo Manispaa ya Singida katika mkutano wa hadhara baada ya kutembelea na kukagua miradi ya maendeleo tisa iliyogharimu zaidi ya Sh.Bilioni 2 katika mkutano uliofanyika Julai 20, 2023.
Na Dotto Mwaibale, Singida
MBUNGE wa Singida Mjini Musa Sima amemshukuru Mheshimiwa Rais, Dk. Samia
Suluhu Hassan kwa kupeleka fedha nyingi za miradi ya maendeleo kila sekta
katika Kata ya Unyamikumbi ambapo zaidi ya Sh.Bilioni 2 zimetumika kutekeleza
miradi hiyo.
Sima ametoa shukrani hizo jana Julai 20,
2023 alipokuwa akielezea miradi
iliyotekelezwa katika kata hiyo wakati wa muendelezo wa ziara yake ya kutembelea na kukagua miradi
hiyo pamoja na kufanya mkutano wa hadhara na kusikiliza kero za wananchi ili
kuzitafutia ufumbuzi ambapo moja ya kero kubwa ni upungufu wa walimu,nyumba za
kuishi pamoja na madarasa katika shule zilizopo pembezoni mwa manispaa hiyo na kuombwa kuifanyia kazi changamoto hiyo.
Katika ziara hiyo Sima aliambatana na wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Wilaya
ya Singida ambapo alisema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt Samia
Suluhu imepeleka fedha nyingi katika kata hiyo kwa ajili ya miradi ya maendeleo
ikiwemo ujenzi wa vyoo kwenye baadhi ya shule, ujenzi wa madarasa, miradi ya
maji na ujenzi wa daraja lililopo Kijiji cha Utamaha na kuwa lengo la Serikali kupeleka
miradi hiyo ni kutoa huduma bora kwa wananchi.
Alisema katika utekelezaji wa miradi hiyo kupitia mfuko wa mbunge ametoa
zaidi ya Sh.Milioni 10 kwenye maeneo tofauti ndani ya kata hiyo ili kusaidia
ukamilishaji wa miradi hiyo.
Aidha, Sima ameipongeza na kuitaka timu nzima ya viongozi wa kata hiyo,
wataalam na wananchi walioshirikiana kwa namna moja hama nyingine kuanzia
mwanzo katika usimamizi wa miradi hiyo inayoendelea na kufikia hatua za mwisho
kukamilika kuendeleza ushirikiano huo.
Mbunge Sima akizungumzia kuhusu mkataba wa Bandari ya Dar es Salaam dhidi
ya Kampuni ya DP World ya Dubai alisema kuna mambo makubwa mawili Usalama na
Biashara na kuwa Tanzania imeingia mkataba na kampuni hiyo kwa ajili ya kufanya
biasharawa na si vinginevyo.
Aliwataka wananchi wa kata hiyo kuwapuuza wale wote wanaotaka kupotosha
ukweli wa mkataba huo wenye tija kwa nchi yetu kuwa eti Rais Samia Suluhu
Hassan ameiuza bandari hiyo.
Alisema wabunge wasingeweza kuridhia kufanyika kwa maridhiano ya mkataba
huo baina ya Tanzania na DP World iwapo kama kungekuwepo kwa viashiria vya kuuzwa
kwa bandari hiyo.
Alisema kupitia
uwekezaji huo Tanzania itakuwa ikipata Sh.Trilioni 26 kwa mwaka tofauti na sasa
ambapo tunapata Sh.Trilioni 7 tu kupitia bandari hiyo kwa mujibu wa taarifa
zilizopo.
Alisema mkataba huo kwa kuzingatia sheria ya uwekezaji ilipendekezwa kampuni hiyo isajiliwe Brela
hapa nchini na iitwe DP World Tanzania na
wao wataingia mkataba na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) jambo ambalo
litasaidia kusitisha mkataba huo kwa sheria za nchi yetu iwapo watashindwa
kutimiza masharti na kuwa utahusisha Bandari ya Dar es Salaam tu na si na
nyingine kama inavyopotoshwa.
Diwani wa Kata hiyo, Kipandwa Ipini alisema miradi
iliyotembelewa na kukaguliwa na mbunge huyo jumla yake ni tisa na kuitaja pamoja
na thamani yake kuwa ni ujenzi wa vyoo Shule ya Msingi Sundu ambavyo
vimegharimu Sh.Milioni 18 ukiwepo na mchango wa wananchi.
Alitaja vyoo vingine kuwa ni vya Shule ya Msingi Ughaugha
A vyenye matundu 12 ambavyo vimetumia Sh.Milioni 15 pamoja na michango ya wananchi
huku Serikali ikitoa Sh.Milioni 11, madarasa ya Shule ya Msingi Unyamikumbi ambayo
yametumia Sh.Milioni 19 ikiwa na michango ya wananchi ambapo Serikali
ilichangia Sh.Milioni 15.
Alitaja mradi mwingine kuwa ni ujenzi wa madarasa manne
yenye thamani ya Sh.Milioni 80, barabara ya Ughaugha na barabara ya Kihade
jumla zimetumia Sh.Milioni 12 na kuwa ni barabara mpya ambazo zimefunguliwa kwa
ajili ya kuharakisha maendeleo ya wananchi, ujenzi wa daraja la Kijiji cha
Utamaha ambalo ujenzi wake umegharimu Sh.Milioni 98.4 na ujenzi wa madarasa
mawili Shule ya Msingi Sundu yaliyogharimu Sh. Milioni 25 na madarasa mawili ya
UVIKO 19 yenye thamani ya Sh.Milioni 40.
Alitaja kazi nyingine ni ujenzi wa maabara katika sShule
ya Sekondari ya Unyamikumbi ambao ujenzi wake umegharimu Sh.Milioni 30 na kuwa
jumla ya miradi iliyotekelezwa ina thamani ya Sh.Milioni 498,174,626.
Alisema miradi mingine ni ile ambayo bado inaendelea
kutekelezwa kama ujenzi wa jengo la mama na mtoto unaojengwa katika Zahanati ya
kata hiyo ambao mpaka sasa umetumia Sh.Milioni 5.8 ambapo hadi kukamilika kwake
zitahitajika Sh.Milioni 148.5 na kutaja mradi mwingine ni ule wa kuboresha maji
katika kata hiyo kutoka chanzo cha maji cha IRAO ambao utagharimu Sh. Bilioni 1.3 na kuwa
tayari umekwisha fanyiwa upembuzi yakinifu na kuwa fedha hizo zitafika wakati
wowote kuanzia sasa.
Diwani wa kata hiyo hakumung’unya maneno wala kusita na kurudi nyuma ambapo naye alitumia nafasi hiyo kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuiona kata hiyo kwa jicho la huruma na kutoa kiasi hicho kkikubwa cha fedha kwa ajili ya kukamilisha miradi hiyo ambapo alimshuru pia Mbunge wa Singida Musa Sima, wataalam, viongozi mbalimbali na yeye mwenyewe kwa usimamizi mzuri uliotukuka wakati wa utekelezaji wa miradi hiyo.
No comments:
Post a Comment