Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi akizungumza na Mkurugenzi Msaidizi Utafiti Idara ya Menejimenti ya Maafa Bw. Charles Msangi (kwanza kushoto) alipotembela banda la ofisi yake katika Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Sabasaba Julai 6, 2023 Jijini Dar es Salaam.
Na Mwandishi Wetu
OFISI ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu na Bunge kupitia Idara ya menejimenti ya
maaafa imesema itaendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya namna ya kujikinga na majanga
mbalimbali pindi yanapotokea ili kupunguza athari za majanga hayo.
Akizungumza hii leo Julai 6, 2023 wakati alipotembelea maonesho ya
kimataifa ya 47 ya biashara maarufu kama sabasaba Katibu Mkuu wa ofisi hiyo
Dkt. Jim Yonazi amesema kuwa Serikali inaendelea Kushirikiana na wadau ili
kuhakikisha kuwa uwezo wa nchi katika kukabiliana na majanga mbalimbali pindi
yanapotokea unaboreshwa.
Aliongezea kuwa, Serikali itaendelea kuratibu vyema masuala ya menejimenti
ya maafa kwa kuzingatia mifumo ya kitehama ili kuwafikia wananchi kwa wakati
kuendelea kuleta matokeo yanayokusudiwa.
“Serikali imewekeza katika mifumo mbalimbali ya kiteknolojia inayosaidia
kutoa Viashiria vya awali vya majanga na pia kusaidia katika utoaji wa taarifa
kwa haraka,”Alieleza Dkt. Yonazi.
Pia akieleza mikakati ya serikali kuratibu masuala ya maafa alisema
imejipanga kuufikia umma wa Watanzania kuanzai ngazi ya Kijiji, Kata, Wilaya ,
Mkoa hadi Taifa na kwa kuzijengea uwezo kamati za maafa kwa ngazi zote na kuwa
na jamii stahimilivu ya maafa nchini.
“Katika mwaka huu mpya wa fedha, tumejipanga kuendelea kujenga uwezo kwa wadau wetu ili kuhakikisha uwezo wetu wa kukabiliana na majanga aina mbalimbali unaboreshwa kwa kuzingatia athari zake kiuchumi, kijamii na nyingine nyingi,” Alisisitiza Dkt. Yonazi.
No comments:
Post a Comment