DC SINGIDA : WAFANYABIASHARA VIPODOZI SHIRIKIANENI NA SERIKALI KATIKA KUDHIBITHI VIPODOZI VYENYE SUMU - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Friday 28 July 2023

DC SINGIDA : WAFANYABIASHARA VIPODOZI SHIRIKIANENI NA SERIKALI KATIKA KUDHIBITHI VIPODOZI VYENYE SUMU

Mkuu wa Wilaya ya Singida, Mhandisi Paskas Muragili, akizungumza na Wafanyabiashara wa Vipodozi Mkoa wa Singida Julai 27, 2023, wakati akifungua kikao cha TBS na wafanyabiashara hao cha kutoa elimu juu ya uelewa kuhusu vipodozi vyenye viambata sumu.

Na Dotto Mwaibale, Singida

MKUU wa Wilaya ya Singida, Mhandisi Paskas Mragili amewataka wafanyabiashara wa vipodozi mkoani hapa kushirikiana na Serikali pamoja na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kudhibiti bidhaa zenye viambata vyenye sumu.

Mragili alitoa ombi hilo wakati akifungua kikao cha TBS na wafanyabiashara cha kutoa elimu juu ya uelewa kuhusu vipodozi vyenye viambata sumu Mkoa wa Singida.

Hatua ya TBS kutoe elimu hiyo ilifuatia maombi yaliyotolewa na wafanyabiashara hao kwa Mkuu wa Wilaya ya Singida Mwezi Mei, 2023 wakati maafisa wa TBS walipoanzisha operesheni ya kupita katika maduka ya vipodozi kwa lengo ya kuondoa bidhaa hizo katika soko ambazo zinaathari kwa binadamu.

“Mwezi Mei mliniletea malalamiko kuwa maafisa wa TBS wamefika kwenye maduka yenu na kuanza kuondoa vipodozi ambavyo havikubaliki kwa matumizi ya binadamu mkidai operesheni hiyo ilikuwa ikifanyika bila ya kupewa uelewa wa matumizi ya bidhaa hizo, niliona mlikuwa na hoja ya msingi licha ya TBS kutangaza jambo hilo tangu mapema ndipo nilichukua uamuzi wa kuwazuia maafisa hao ili mpate mafunzo hayo na twende pamoja,´alisema Mragili.

Alisema anawapongeza sana TBS kwani baada ya kuwazuia kutokana na uungwana wao licha ya kuwa walikuwa wakitekeleza wajibu wao kisheria Mwezi Juni 2023 walirudi tena Singida na kufanya kikao na wafanyabiashara hao na kuwapa elimu na sasa wamerudi tena kwa mara nyingine kwa lengo lilelile.

Alisema Shirika la Viwango Tanzania (TBS) ndio limepewa jukumu la kusimamia vipodozi hivyo kupitia Mabadiliko ya Sheria ya Fedha ya Mwaka 2019 ambapo limekuja na mkakati  wa kuelimisha wananchi juu aina ya vipodozi vyenye viambata sumu vilivyopigwa marufuku kwenye soko la Tanzania ikiwa ni pamoja na kuendesha ukaguzi wa kushtukiza kwenye soko kwa lengo la kuviondoa , kutoa elimu kwa umma na kuvisajili.

Mragili alisema kuendelea kuviuza na kuvitumia vipodozi hivyo ni hatari kwani wanaliangamiza taifa jambo ambalo ni hatari na halikubaliki na kwamba baada ya mafunzo hayo hategemei kuona bidhaa hizo zikiendelea kuwepo kwenye soko ambapo alitoa tahadhari kwa wafanyabiashara hao kuviondoa mara moja kabla havijakutwa na maafisa wa TBS na kuvikamata.

“ Baada ya mafunzo haya hatutakuwa na huruma na mfanyabiashara yeyote atakayekamatwa akiendelea kuwa na vipodozi hivyo kwenye soko na hasije akatuambia ni bahati mbaya ninyi mnamtandao mkubwa nendeni mkawaambie na wenzenu kwani wanaoathirika navyo si wale tu mnaowauzia bali na ndugu zenu pia,” alisema Mragili.

Aliwataka wafanyabiashara hao waache kuangalia upande mmoja tu wa kuwa watakosa fedha bali wawe na dhamira ya kulinda afya za watanzania.

Awali akitoa mafunzo hayo Meneja wa TBS Kanda ya Kati, Nickonia Mwabuka alisema matumizi ya vipodozi hivyo vyenye viambata vyenye sumu ni hatari kwa afya ya binadamu na vimekuwa vikiwaathiri watu wengi na kuliongezea taifa gharama kubwa ya kuwatibu waathirika na kupunguza nguvu kazi ya taifa.

Alivitaja vipodozi visivyo salama ni vile ambavyo vina kemikali zinazoweza kuudhuru mwili na kuusababishia matatizo, ambavyo havijasajiliwa na TBS, vipodozi vyenye viambata (kemikali) vya sumu na vilivyopigwa marufuku, ambavyo muda wake wa matumizi umeisha, vipodozi ambavyo havioneshi tarehe ya kuharibika  (Expire-date).

Vingine ni vile ambavyo maelezo yake hayajaandikwa kwa Kiswahili au Kiingereza ambavyo vinaweza vikawa ni mafuta, losheni, krimu, pafyumu, poda na kadhalika.

Mwabuka alitumia nafasi hiyo kuwataka wafanyabiashara wa vipodozi hivyo kupeleka taarifa za vipodozi wanavyouza ikiwa ni pamoja na kuvisajili kwa lengo la kuhakiki ubora na usalama wake., hatua itakayowasaidia kujua ni vipodozi vipi vimepigwa marufuku na vile vinavyoruhusiwa kwenye soko la Tanzania.

Mwenyekiti wa Umoja wa Wauzaji wa Vipodozi Mkoa wa Singida, Pili Hussein akizungumza kwa niaba ya wenzake aliomba Serikali kuwadhibiti wafanyabiashara wakubwa wa bidhaa hizo ambao wamekuwa wakiwauzia.

“Tunashindwa kuelewa kuna vyombo husika vya ukaguzi katika bandari, viwanja vya Ndege na mipakani ambako bidhaa hizi zinapitishwa na wafanyabiashara wakubwa na kusajiliwa ambao wanafahamika lakini wanaacha kuwadhibiti hadi zikifika kwetu ndio wanakuja kuzikamata jambo hili sio zuri kwani linaturudisha nyuma na kufilisi mitaji yetu,” alisema Hussein.

Meneja wa TBS Kanda ya Kati, Nickonia Mwabuka, akitoa mada kuhusu uelewa wa vipodozi na madhara yake kwa wafanyabiashara hao.
Katibu Tawala Wilaya ya Singida, Goodluck Mwangomango, akimkaribisha Mkuu wa Wilaya ya Singida, Mhandisi Paskas Mragili kufungua mafunzo hayo ya siku moja.
Wafanyabiashara wa vipodozi Mkoa wa Singida wakiwa kwenye mafunzo hayo
Washiriki wa mafunzo wakifuatilia mada iliyokuwa kuwa ikitolewa na Meneja wa TBS Kanda ya Kati, Nickonia Mwabuka.

Taswira ya mafunzo hayo.
 

No comments:

Post a Comment