RC SINGIDA ARIDHISHWA NA UTEKELEZWAJI WA MIRADI WILAYA YA IKUNGI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Wednesday, 7 June 2023

RC SINGIDA ARIDHISHWA NA UTEKELEZWAJI WA MIRADI WILAYA YA IKUNGI

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba (katikati), akizungumza wakati alipokuwa akiukagua mradi wa maji katika Kijiji cha Matare uliotekelezwa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Ikungi wakati wa ziara yake aliyoifanya Juni 6, 2023.

Na Dotto Mwaibale, Ikungi

MKUU wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba  amefurahishwa na kuridhishwa na usimamizi mzuri na ukamilishaji wa miradi ya maendeleo katika Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi na kuwapongeza viongozi wote kwa utekelezaji wa miradi hiyo kwa thamani halisi ya fedha zilizotolewa na Serikali.

Serukamba  ametoa pongezi hizo wakati wa ziara yake wilayani humo aliyoifanya leo Juni 6, 2023 ambapo alipata fursa ya kutembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo na kuhimiza ikamilike kabla ya Julai 1, 2023.

Aidha, Serukamba amewapongeza wataalam na wananchi kwa kuunga mkono juhudi za serikali kwa kuchangia utalaam na nguvu kazi katika kutekeleza miradi hiyo ambayo imegharimu fedha nyingi.

"Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imefanya kazi kubwa kwa kutoa fedha nyingi kwa ajili ya kutekeleza miradi hii naomba tumuheshimishe Rais wetu kwa kuikamilisha haraka kabla ya Julai 1, 2023 ili ianze kutumika," alisema Serukamba.

Alisema Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi imekuwa ikimpa raha kutokana na kufanya vizuri katika kutekeleza miradi ya maendeleo na kuwa imekuwa ikipata mafanikio hayo kutokana na ushirikiano uliopo baina ya viongozi, wataalam na wananchi.

Miradi aliyoitembelea na kuikagua ni mradi wa maji katika Kijiji cha Matare uliopo Kata ya Unyahati uliogharimu Sh. Milioni 386.8 ambao utawahudumia wananchi 5036, ujenzi wa madarasa katika Shule ya Msingi Matare na ujenzi wa mabweni mawili na bwalo katika Shule ya Msingi  Ikungi.

Miradi mingine aliyoitembelea na kuikagua ni ujenzi wa madarasa katika Shule ya Msingi ya Ikungi B, ujenzi wa madarasa katika Shule ya Sekondari ya Ikungi ambayo sasa imekuwa na kidato cha tano na sita, ukaguzi wa mradi wa Kikundi cha vijana kijulikanacho kama Ikungi Chapakazi ambao unajishughulisha na ufyatuaji wa matofali ambapo aliwataka wana kikundi hicho kurejesha mkopo waliokopeshwa na Halmashauri ya Ikungi ili waweze kukopeshwa vijana wengine.

Aidha, miradi mingine iliyokaguliwa na kuhimiza ikamilike haraka ni ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Ikungi, ukaguzi wa ujenzi wa madarasa katika Shule ya Msingi ya Dung'unyi na ujenzi wa barabara ya Ikungi- Matongo yenye urefu wa kilometa moja.

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, akipokea taarifa ya ujenzi wa madarasa katika Shule ya Msingi Matare.

Muonekano wa madarasa yanayo jengwa Shule ya Msingi Matare.

Muonekano wa kazi nzuri ya utunzaji wa mazingira katika Shule ya Msingi  Matare inayofanywa na walimu wa shule hiyo kwa kuwashirikisha wanafunzi.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba (katikati) akiwa na viongozi wengine wakati wa ukaguzi wa ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Ikungi.

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba (mbele) akiongoza msafara wa viongozi mbalimbali na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama wa wilaya hiyo kuelekea kutembelea jengo la Ustawi wa Jamii linalo ratibu na kusimamia shughuli za upingaji wa vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa watoto wa kike na kiume na wanawake katika Wilaya ya Ikungi.

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba (mbele) akiongoza msafara wa viongozi mbalimbali na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama wa wilaya hiyo kuelekea kutembelea jengo hilo.
Muonekano wa jengo hilo.

Muonekano wa mabweni mawili yalio jengwa Shule ya Msingi, Ikungi.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, akikata utepe kuashiria uzinduzi wa mabweni mawili na Bwalo katika Shule ya Msingi Ikungi. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Thomas Apson.

Muonekano wa ujenzi wa madarasa katika Shule ya Msingi Ikungi B.

Taswira ya ujenzi wa madarasa katika Shule ya Sekondari ya Ikungi.
Mhandisi wa Wilaya ya Ikungi, Edward Millinga (katikati), akitoa maelezo ya ujenzi wa madarasa katika Shule ya Sekondari ya Ikungi. Wa kwanza kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Justice Kijazi na wa pili ni Mkuu wa Shule hiyo, Madamu Neema Stephano.

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba (katikati) akiongoza msafara wa viongozi mbalimbali na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama wa wilaya hiyo wakati wa ukaguzi wa ujenzi wa Barabara ya Ikungi-Matongo.

Taswira ya mradi wa vijana Chapa kazi Ikungi, unaojishughulisha na ufyatuaji wa matofali.

Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Wilaya ya Ikungi, Zilfat Muja (katikati) akitoa maelezo kwa Mkuu wa Mkoa wa Singida (wa wanne kutoka kushoto) kuhusu mradi huo. Kutoka kushoto ni Afisa Maendeleo wa Wilaya ya Ikungi, Haika Masawe, Mwenyekiti wa kikundi hicho, Mwanahamisi Omari, Mkuu wa wilaya hiyo, Thomas Apson na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Ally Mwanga.

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba akitoka kukagua ujenzi wa madarasa katika Shule ya Msingi Dung'unyi wakati wa ziara hiyo. Katikati ni Diwani wa Kata hiyo, na kushoto kwa diwani ni Afisa Mtendaji wa kata hiyo, Yahaya Njiku.
 

No comments:

Post a Comment