Na Adeladius Makwega-MWANZA
JUNI 16, 2023 Mwanakwetu alipotembelea ukurasa wa mtandao wa kijamii wa mwanahabari Remigius Mmavele na akakutana maelezo haya,
“Mungu akupokee na kukujalia pumziko la milele huko ulipotangulia ADOLF MBINGA, tulikuwa pamoja nyakati zote za furaha na mahangaiko, nyakati ya ugonjwa, sote njia yetu ni moja umetangulia ndugu, rafiki yangu Adolf Mbinga, mtaalamu wa kucharaza Solo gitaa uliyepata ujuzi huo Chuo cha Ufundi Ndanda.”
Mwanakwetu baadaya ya kusoma ujumbe huu akamtafuta mwanahabari Mavele na kuzungumza naye,
“Adolf Mbinga namfahamu sana, mpaka wakati anaumwa mimi na wenzangu tulifika nyumbani kwake na kumpeleka Hospitali hadi tukaamua arudi nyumbani, tangu amekwenda huko haijafika hata majuma matatu amefariki. Awali nilimtafuta nikafanya nae vipindi vya redio viwili. Anazikwa Kwao Kijiji cha Mpute Juni 17, 2023 saa 4 ya asubuhi lakini mimi sintoshiriki kutokana na majukumu ya kazi.”
Mwanakwetu alimpa pole Remigius Mmavele kwa msiba wa rafiki yake, kaka yake na nduguye huyo akisema kwa hata kitendo cha kumchukue Adolf na kumpeleka Hospitali ni kitendo cha kiungwana sana huku Mwanakwetu alitamani kufahamu juu ya mambo aliyoongea naye mwanamuzi huyu akiwa hai ni yepi?
“Adolf Mbinga katika vipindi vyangu vya redio aliungama wazi kuwa alitoka Bendi ya Twanga Pepeta na kumfuta Waziri wa zamani mhe. Mudhihiri Mudhihiri na kumshawisha anunue vifaa vya bendi ya muziki, mhe huyu alifanya hivyo , baadaye Adolf Mbinga aligeuka nyuma na kurudi Twanga Pepeta na hilo likamtia hasara mhe. Mudhhiri. Adolf Aliporudi Twanga Pepeta ndipo akapachikwa jina la MTUHUMIWA na wenzake kwa utani. Hata mimi (Mavele) nilipompigia simu mhe Mudhhiri alikata kusikiliza habari za Adolf Mbinga kwani alisema alimtia hasara kubwa.”
Mwanakwetu katika suala la kutiana hasara anasema kuwa kila mmoja wetu anayo simulizi ya maisha yenye kupanda milima na mabonde, maana panda shuka panda shuka ndiyo maisha ya binadamu.Mwanakwetu alimuuza mwanahabari Mavele je alimuliza Adolf Mbinga je katika muziki aliwahi kutunga wimbo wowote na je wimbo upi ulikuwa wa kwanza?
“Alitunga nyimbo nyingi na wimbo wa kwanza ulikuwa ni Neema wa Daimond Sound -wana Kibinda Nkoi miaka 1996 na baadaye zikaja zile nyimbo zake za Twanga pepeta kama Kisa cha Mpemba, Bwana Kijiko na Tabu za Maisha.”
Mwanakwetu mara alipomaliza mazungumzo na mwanahabari Remigius Mmavele alimtafuta Mwanamuzi Mwinyijuma Muumini- Kocha wa Dunia, hayo yalikuwa majira ya saa 10.20 ya jioni ya Juni 16, 2023 mwanamuziki huyu alikuwa stendi ya Mabasi ya Mikoani ya Mbagala Zakhem akisubiri basi lililokuwa linatoka Dodoma kuelekea Nachingwea apande kuelekea Kijiji cha Mpute-Nachingwea kushiriki maziko ya Adolf Mbinga ya Juni 17, 2023, huku Kocha wa Dunia akisema haya,
“Nilimfahamu akiwa Daimond Sound tangu mwaka 1996 na walikuwa wakifika Kenya, Mwaka 2000 nilipotoka Nairobi nikamkuta Twanga Pepeta na yeye alikuwa kiongozi wa bendi hiyo na baadaye tukaenda Mchinga Sound pamoja. Akiwa Twanga altunga wimbo wa Kidomo domo ambao tulipokwenda Mchinga tukaurekodi, Twanga Pepeta nilikuwa naimba kopi tu.lakini Mchinga Sound niliimba nyimbo nyingi na yeye kupiga gitaa.”
Kocha wa Dunia akiwa anazungumza na Mwanakwetu kwa njia ya simu katika eneo lenye makelele sana alisema kuwa wakiwa Mchinga Sound.
“Katika nyimbo zote za Mchinga Sound magitaa ya solo na rhythm wakati wa kurekodi kazi hizo zilifanywa na Adolf Mmbinga peke yake studio, baada ya kurekodi katika maonesho ya wazi alimuachia Godi kupiga gitaa la rhythm .”
Mwanakwetu aliyakumbuka mno maneno hayo ya Mwinjuma Muumini, akisema kuwa Adolf Mbinga hakujitapa kwa kuifanya kazi hiyo peke yake wengine wakidhani kuwa Godi alishiriki kurekodi gitaa za nyimbo hizo na kupiga rhytihm.
Mwanakwetu kwa heshima ya mchango wa mwanamuziki Adolf Mbinga katika muziki wa dansi wa Tanzania kwa karibu miaka 30 ya kazi anatoa pole kwa wanamuziki wote wa muziki wa dansi Tanzania kwa kumpoteza wanamuziki mwenzao, Pole kwa familia ya Adolf Mbinga , Pole kwa Kocha Dunia–Mwijuma Muumini na Pole kwa mwanahabari Remigius Mmavele.
Buriani Mwanamuziki Adolf Mbinga.
0717649257
No comments:
Post a Comment