TMDA KANDA YA KATI YATOA ELIMU YA MATUMIZI SAHIHI YA DAWA MKOANI SINGIDA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Thursday, 4 May 2023

TMDA KANDA YA KATI YATOA ELIMU YA MATUMIZI SAHIHI YA DAWA MKOANI SINGIDA

Afisa Mwandamizi Elimu kwa Umma wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), Kanda ya Kati James Ndege, akizungumza na Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Dk. Salmin iliyopo Manispaa ya Singida wakati akitoa elimu ya namna bora ya matumizi ya dawa, vifaa tiba na vitendanishi yaliyofanyika leo Mei 4, 2023. 

Na Dotto Mwaibale, Singida

MAMLAKA ya Dawa na Vifaa tiba (TMDA) Kanda ya Kati imetoa elimu ya matumizi sahihi ya dawa, vifaa tiba pamoja na vitendanishi  kwa makundi mbalimbali ya kijamii na wanafunzi Mkoa wa Singida ili kuzuia madhara yanayoweza kutokea kutokana na utumiaji wa dawa hizo kiholela.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa utoaji wa mafunzo hayo Afisa Mwandamizi Elimu kwa Umma wa TMDA Kanda ya Kati, James Ndege alisema mafunzo hayo yamelenga kutoa elimu hiyo pamoja na kujifunza kutoa taarifa ya madhara yanayotokana na matumizi ya bidhaa hizo.

Alisema matumizi yasiyo sahihi ya dawa na vifaa tiba na vitendanishi yanasababisha athari kubwa kwa watumiaji, watu kupoteza maisha,kupata ulemavu na viungo mbalimbali kuathirika kama ini na , figo.

Ndege alisema elimu hiyo ni muendelezo ili wananchi waweze kujua namna bora ya matumizi ya dawa na ndio maana wameanzisha klabu katika shule mbalimbali ili elimu hiyo inayotolewa na TMDA iweze kusambaa kila maeneo na kuifanya jamii kuelewa athari za matumizi ya dawa hizo.

Aidha Ndege alitoa wito  kwa wananchi kuzingatia matumizi sahihi ya dawa ikiwemo kuepuka matumizi holela ya dawa kwa kutumia dozi kikamilifu sambamba na kupata vipimo na ushauri wa wataalam wa Afya kabla ya kutumia dawa hizo.

Alisema kuna changamoto kubwa kwenye jamii ya watanzania kwani baadhi yao wamekuwa wakitumia  dawa wanapojisikia kuumwa bila kupima wala kupata ushauri wa daktari na kwamba wengi wao zimewapelekea kupata madhara kiafya.

"Kuna changamoto kubwa katika jamii kwa watu kutumia dawa kiholela na sisi TMDA tunaendelea kuwaelimisha kuwa utumiaji wa dawa kiholela unaweza kusababisha usugu wa bakteria na kufanya dawa hizo kushindwa kufanyakazi kama inavyotakiwa" alisema Ndege.

Pia Ndege aliwataka wananchi kuzingatia muda wa kutumia dawa hizo kama walivyoelekezwa na madaktari kwani kutumia dawa hizo kwa muda ambao hawajaelezwa zinaweza kuwaletea changamoto za kiafya.

Aidha alitoa angalizo kwa wanafunzi wasichana kuacha ama kutojiingiza katika matumizi ya dawa za dharura za kuzuia mimba hasa katika wakati huu ambao wapo shuleni na umri mdogo na kuwa matumizi ya dawa hizo zinaweza kuwa na athari kubwa kwao za mfumo wa uzazi pindi wakiwa watu wazima na umri unaoruhusiwa kufunga ndoa au kupata watoto.

Ndege pia alitoa angalizo hilo kwa wanafunzi wavulana nao kuacha kutumia dawa za kuongeza nguvu za kiume ambapo nao wanaweza kupata athari zilezile ambazo zinaweza kuwapata wasichana na badala yake aliwataka kusoma kwa bidii na kufanya mazoezi hali itakayowasaidia kutowaza kufanya ngono.

Katika mafunzo hayo waliweza kuzindua klabu zilizoanzishwa na TMDA katika shule mbali kwa ajili ya kutoa elimu kuhusu matumizi yasiyo sahihi ya dawa, vifaa tiba na vitendanishi na masuala yote yasiyo salama ya matumizi ya dawa hizo.

Shule ambazo zimepatiwa mafunzo hayo hadi leo May 4, 2023 ni shule sita za sekondari za Kindai, Dk. Salmin, Ipembe, Senge Singida, Utemini na wananchi wa Kata za Mitunduruni, Majengo na Mungumaji zote za Manispaa ya Singida..

Mkaguzi wa Dawa Kanda ya Kati, Saraphina  Cleophace akizungumza na wanafunzi hao wakati akijibu maswali mbalimbali.

Mkuu wa Shule ya Sekondari  Dk.Salmin, Juma Thomas akielekeza jambo wakati wa mafunzo hayo.

Mkaguzi wa Dawa Kanda ya Kati, Saraphina  Cleophace, akimkabidhi vipeperushi Mkuu wa shule hiyo, Juma Thomas vitakavyotumika kuwafundishia wanafunzi.

Picha ya pamoja na wanachama wa Klabu ya TMDA Shule ya Sekondari ya Kindai.

Mlezi wa Klabu ya TMDA Mwalimu Alimas Jumanne Alimas wa Shule ya Sekondari ya Kindai akipokea vipeperushi vya kujifunzia kutoka kwa Mkaguzi wa Dawa Kanda ya Kati, Saraphina  Cleophace,

Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Dk.Salmin, Mwalimu Juma Thomas akizungumza na wanafunzi.

Wanafunzi wakipata mafunzo hayo.

Mafunzo yakiendelea.

Afisa Mtendaji wa Kata Mughanga, akizungumza na wananchi wa Kata hiyo (hawapo pichani) kabla ya kupata elimu hiyo.

Wananchi wa Kata ya Mughanga wakiwa kwenye mafunzo hayo.

Mafunzo yakiendelea.

No comments:

Post a Comment