Katibu Mkuu Sekta ya Ujenzi Balozi, Eng. Aisha Amour akisisitiza jambo alipofungua mkutano mkuu wa tano wa Mafundi Sanifu jijini Mwanza. |
Katibu Mkuu Sekta ya Ujenzi Balozi, Eng. Aisha Amour akiteta jambo na Msajili wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) Eng. Bernard Kavishe katika Mkutano mkuu wa tano wa Mafundi Sanifu jijini Mwanza. |
Msajili wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) Eng. Bernard Kavishe akizungumza katika Mkutano mkuu wa tano wa Mafundi Sanifu jijini Mwanza. |
Baadhi ya Mafundi sanifu wakifatilia hotuba ya Mgeni rasmi Balozi, Eng. Aisha Amour (hayupo pichani) katika Mkutano mkuu wa tano wa Mafundi Sanifu unaoendelea jijini Mwanza. |
KATIBU Mkuu Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi), Balozi Eng. Aisha Amour ameitaka Bodi ya Usajili wa Wahandisi nchini (ERB), kusajili mafundi sanifu wenye sifa stahiki na kuwaunganisha katika miradi mbalimbali ya kitaifa inayoendelea nchini.
Akizungumza wakati akifungua mkutano mkuu wa tano wa mafundi sanifu jijini Mwanza, Balozi Eng. Aisha amesema Serikali inafahamu kwamba idadi ya mafundi sanifu nchini ni ndogo hivyo itaendelea kuboresha vyuo vya ufundi vilivyopo na kuongeza vingine ili kulinda kada ya mafundi sanifu.
“Naielekeza ERB kuleta Serikalini mpango mkakati utakaotatua changamoto hii ili kuipatia ufumbuzi na hivyo kulinda kada ya mafundi sanifu “, amesema Balozi Eng. Aisha.
Aidha, ameiataka ERB iendelee kujenga uelewa wa mafundi sanifu makazini na vyuoni juu ya umuhimu wa kusajiliwa na kuwakumbusha waajiri kufuata sheria kwa kuajiri mafundi sanifu waliosajiliwa.
Zaidi ya mafundi sanifu 500 wamehudhuria mkutano huo wa mwaka uliongozwa na kaulimbiu isemayo mchango wa mafundi sanifu katika kutekeleza mpango wa tatu wa taifa wa maendeleo wa miaka mitano.
Kwa upande wake, Msajili wa Wahandisi Eng. Bernard Kavishe amesema ERB imejipanga kuhakikisha inaratibu shughuli zote za wabunifu hususan wanaotengeneza magari ya umeme hapa nchini na kuwataka wadau wote wenye bunifu mbalimbali kuwasiliana na ERB ili bunifu zao zitambuliwe na kujengewa uwezo.
“Tunawaomba wadau wote wenye bunifu mbalimbali kuwasilisha ERB ili kuwaunganisha na kuwajengea uwezo wa pamoja kufika malengo ya bunifu zao”, amesisitiza Eng. Kavishe.
Wabunifu wawili kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na KAPEE Motors wameonesha bunifu zao za magari ya kutumia umeme yasiyokuwa na kelele na yanayolinda na kuhifadhi mazingira.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-ERB
No comments:
Post a Comment