Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongella, ndani ya Tawi la Benki ya NMB Kwa Mrombo jijini Arusha. |
BENKI Kuu ya Tanzania (BoT), imeipongeza Benki ya NMB kwa kuwa kinara miongoni mwa mabenki 44 nchini kwa ubunifu wa kuchangia ukuaji wa sekta ya fedha kwa kutanua mtandao wa matawi, hivyo kuongeza idadi ya watanzania wanaotumia huduma za kibenki, na hivyo kukuza kiwango cha amana za wateja.
Pongezi hizo zimetolewa na Mkurugenzi wa BoT Kanda ya
Arusha, Ibrahim Malogoi, mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongella, wakati
wa uzinduzi wa Tawi la Benki ya NMB Kwa Mrombo jijini Arusha, ambalo linakuwa
tawi la 229 kwa Benki hiyo nchini, hafla iliyohudhuriwa na Afisa Mkuu wa Wateja
Binafsi na Biashara wa NMB, Filbert Mponzi.
Uzinduzi wa Tawi la Kwa Mrombo linalokuwa la sita la
Benki ya NMB jijini Arusha, huku likiwa ni la 12 kwa mkoa huo na la 43 Kanda ya
Kaskazini, umefanyika leo, sambamba na makabidhiano ya msaada wa madawati 100
kupitia Programu ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR), kwa ajili ya Shule ya Msingi
Msasani iliyopo jirani na tawi hilo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Malogoi alisema sekta ya
fedha inakua kwa kasi kubwa nchini na kwamba wao kama ndio wasimamizi wakuu wa
sekta hiyo Tanzania, wanafarijika kwa ongezeko la matawi ya benki nchini, huku
akipongeza uamuzi wa NMB kufungua tawi Kwa Mrombo, eneo ambalo linakua kwa
haraka na kuongezeka kwa uhitaji wa huduma za kibenki.
Kwa upande wake, RC Mongella alisema anaamini kuwa NMB Tawi
la Kwa Mrombo ni kichocheo cha ukuaji kiuchumi kwa wafanyabiashara,
wajasiriamali na wananchi wa Arusha, na kuwa uwingi wa matawi mkoani mwake,
pamoja na uwekezaji mkubwa kidijitali uliofanywa na NMB, utaondoa foleni
matawini zinazokwaza ustawi kiuchumi, hivyo kurahisisha mzunguko wa utafutaji
na kuchochea fursa za maendeleo na kutoa wito kwa wana Arusha kutumia vema
fursa za kustawi kiuchumi zinazoletwa na NMB.
Awali, Mponzi alimshukuru RC Mongella kwa kutenga muda wa
kushiriki uzinduzi wa tawi hilo ambalo linaenda kuwa chachu ya maendeleo na
mkombozi wa wateja wao, wakiwemo mawakala wa NMB waliotapakaa katika mji wa
Arusha na mikoa mikoa jirani ya Kanda ya Kaskazini.
"Tunajivunia kukua kwa mtandao wetu wa matawi, sambamba
na uwekezaji mkubwa kidijitali, ambao unampa fursa mteja kufungua akaunti kwa
simu na hata kupata huduma, zikiwemo za Mikopo midogo isiyo na dhamana ya
Mshiko Fasta," alibainisha Mponzi mbele ya Mkuu wa Idara ya Mtandao wa
Matawi ya NMB, Donatus Richard na Meneja wa NMB Kanda ya Kaskazini, Dismas
Prosper.
No comments:
Post a Comment