Na Eleuteri Mangi, WUSM, Cape Town Afrika Kusini
KATIBU Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Saidi Yakubu, Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana Utamaduni na Michezo Fatma Hamad Rajab pamoja na ujumbe wa Tanzania wamekutana na timu ya Afrika Kusini wamejadili juu ya namna bora ya kutunza Urithi wa Ukombozi wa Afrika Kusini yakiwemo makaburi yaliyopo Tanzania.
Makaburi hayo ya wapigania uhuru wa Afrika Kusini yapo katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Kongwa mkoani Dodoma, Mazimbu na Dakawa mkoani Morogoro pamoja na Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika kikao hicho Mei 26, 2023 Cape Town Afrika Kusini, Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Saidi Yakubu amesema Tanzania inaguswa kwa namna ya pekee na suala ya historia ya Afrika Kusini kwa kipindi chote tangu wakati wa harakati za ukombozi hadi sasa ndiyo maana Tanzania inaendelea kuyatunza makaburi ya wapigania uhuru hao.
Amepongeza Afrika Kusini kwa jinsi ambavyo wanatunza historia yao katika maeneo mbalimbali nchini humo ikiwemo makumbusho ya Uhuru Park ambapo majina ya wapigania uhuru yameandikwa kwa kumbukumbu za kizazi cha sasa na vizazi vijavyo.
Bw. Yakubu ameongeza katika ziara hiyo ya kikazi, Tanzania imekabidhi majina 93 ya Watanzania ambao walitoa mchango wao katika ukombozi wa Afrika Kusini na kufikisha jumla ya majina 95 yakijumuishwa na jina la Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere, Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambalo tayari lipo kwenye orodha ya nchi hiyo.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya South African Heritage Resource Agency Wakili Lungisa Malgas amesema taasisi hiyo inasimamia masuala ya urithi wa utamaduni yakiwemo makaburi ya wapigania uhuru wa nchi hiyo na wataendelea kushirikiana na Tanzania katika kuyahifadhi, kuyalinda na kuyatunza makaburi hayo ambayo yanahistoria muhimu kwa nchi zote mbili.
Akiwa jijini Pretoria Katibu Mkuu Bw. Saidi Yakubu na Ujumbe anaouongoza amekutana na kufanya kikao cha pamoja na baadhi ya watendaji wa Wizara ya Michezo. Sanaa na Utamaduni ya Afrika Kusini na kubadilishana uzoefu ili kuboresha sekta hizo na kuwaletea maendeleo wananchi wa pande zote mbili.
Kwa upande wa Afrika Kusini wamesema linapokuja suala la ushirikiano, Afrika Kusini ipo tayari kushirikiana na Tanzania kwa kuwa udugo baina ya nchi hizo mbili ni wa kihistoria ambao umeasisiwa na viongozi Mwal. Julius MNyerere wa Tanzania na Nelson Mandela wa Afrika Kusini.
Aidha, pande zote mbili zimekubaliana kuendelea kushirikiana katika sekta za Utamaduni, Sanaa na Michezo ambapo mwaka Novemba 17 hadi Desemba 04, 2022 nchi hizo zilifanya tamasha la Msimu wa Utamaduni wa Afrika Kusini na Tanzania katika mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma na Morogoro.
No comments:
Post a Comment