Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Nape Nnauye akizungumza wakati alipofanya ziara ya kukagua miundombinu katika Kituo cha Mkongo na hali ya huduma za Mawasiliano kupitia Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano katika Kituo cha Kutoa Huduma kwa Pamoja Mpakani (OSBP) cha Namanga kilichopo mkoani Arusha.Machi 5,2023.
Na Mwandishi Wetu, WHMTH, Arusha
WAZIRI wa Habari, Mawasiliano na
Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye amelielekeza Shirika la Mawasiliano
Tanzania (TTCL) kushirikiana na Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) kuharakisha
utengenezaji wa mfumo wa ufuatiliaji na usimamizi (Dashibodi) wa vituo vyote
vinavyotoa huduma za Mkongo nchini.
Maelekezo hayo ameyatoa katika mpaka
wa Namanga-Arusha Machi 5, 2023 alipozuru kukagua miundombinu katika kituo cha
Mkongo kilichopo katika mpaka huo na hali ya huduma za Mawasiliano kupitia
Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano katika Kituo cha Kutoa Huduma kwa Pamoja Mpakani
(OSBP) cha Namanga.
"Kumekuwa na malalamiko ya kukosekana kwa huduma za mkongo au kasi ndogo ya mtandao katika baadhi ya maeneo, hivyo kukamilika kwa dashibodi hiyo
kutawezesha TTCL kuona na kufatilia vituo vyote nchi nzima ", amesema
Waziri Nape.
Ameongeza kuwa, "Tunataka mifumo ya TEHAMA ilete matokeo
yaliyokusudiwa, uwepo wa dashibodi utasaidia kufatilia vituo vya Mkongo na
kufahamu wapi kuna shida na chanzo chake ni nini ili kushughulikia na kurudisha
huduma kwa wakati ".
Amesema kuwa lengo la Serikali ni kuongeza usimamizi ili kuondoa usumbufu
na malalamiko ya wateja wa huduma za Mkongo na kuongeza mapato kwa Serikali.
Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Mhandisi Peter Ulanga amesema Shirika la TTCL pamoja na kutoa
huduma za Mkongo pia linawashauri wateja wake hasa pale wanapopokea malalamiko
ya kasi ndogo ya mtandao ambapo mara nyingi inasababishwa na matumizi makubwa
kuliko kiwango cha huduma (capacity) ambayo taasisi inanunua kutoka TTCL.
Amefafanua zaidi kwa kuelezea tatizo la mfumo wa ndani wa taasisi husika
pamoja na sehemu wanayohifadhia taarifa
za mfumo (server) kuwa na uwezo mdogo
husababisha kasi ya mtandao kuwa ndogo hata kama huduma ya Mkongo inawafikia
vizuri.
Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano umeunganishwa kwenda nchi jirani ya Kenya kupitia mpaka wa Namanga, Horohoro na Holili.
No comments:
Post a Comment