SERIKALI YAAGIZA KUMALIZIKA KWA MZANI WA RUBANA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Sunday, 26 March 2023

SERIKALI YAAGIZA KUMALIZIKA KWA MZANI WA RUBANA

Meneja wa Wakala ya Barabara (TANROADS) mkoa wa Mara, Eng. Vedastus Maribe akitoa maelezo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Eng. Godfrey Kasekenya, kuhusu maendeleo ya ujenzi wa mzani wa kisasa wa Rubana utakaopima magari yakiwa kwenye mwendo (weigh in motion), uliopo Wilayani Bunda, mkoani Mara.

Naibu Waziri wa Ujenzi, Eng. Godfrey Kasekenya, akitoa maelekezo kwa Meneja wa Wakala ya Barabara (TANROADS) mkoa wa Mara, Eng. Vedastus Maribe, wakati akikagua ujenzi wa mzani wa kisasa utakaopima magari yakiwa katika mwendo (weigh in motion), wilayani Bunda, mkoani Mara.

Muonekano wa sehemu ya mradi wa ujenzi wa mzani wa kisasa wa Rubana uliopo katika barabara kuu ya Mpakani mwa Simiyu/Mara hadi Sirari utakaokuwa unapima magari yakiwa katika mwendo (weigh in motion), mkoani Mara. Ujenzi wa mzani huo wa kisasa unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Mei 2023.

SERIKALI imemuagiza mkandarasi wa kampuni ya CHICO anayejenga mzani wa Rubana utakaokuwa unapima magari yakiwa kwenye mwendo (weigh in motion), uliopo katika barabara kuu ya Mpakani mwa Simiyu/Mara hadi Sirari kuongeza kasi ya ujenzi wake ambao unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Mei 2023.

Agizo hilo limetolewa Wilayani Bunda na Naibu Waziri wa Ujenzi Eng. Godfrey Kasekenya, mara baada ya kukagua ujenzi wa mzani huo unaogharimu kiasi cha  Bilioni 22.2 na kusisitiza kuwa hakuna changamoto yoyote ya malipo kwa mkandarasi na mhandisi mshauri ya kusababisha ucheleweshwaji wa mradi huo.


"Niwahakikishie kuwa Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan imeamua kujenga na kusimamia uboreshaji wa miundombinu hapa nchini kwa jicho la pekee na ndio maana fedha zinapelekwa kila kona ya nchi na miradi inaendelea", amefafanua Eng. Kasekenya.


Kasekenya ametaja umuhimu wa ujenzi wa mizani hapa nchini ikiwemo kuilinda miundombinu ya barabara na madaraja ambayo inajengwa kwa fedha nyingi.


Ameeleza pia uwepo wa mizani inaondoa usumbufu kwa watumiaji wa barabara  kwani wasafirishaji watapimwa huku wakiwa kwenye mwendo na watasimama endapo watakuwa wamezidisha uzito kwa ajili ya kupima zaidi.


Vilevile uwepo wa mizani za kisasa nchini utaepusha kupitisha magendo kwa njia ya barabara hasa ukizingatia barabara hii ni kuu inaunganisha nchi na nchi.


Kasekenya amefafanua kuwa mizani hiyo pindi itakapokamilika ndiyo itakuwa kubwa, bora na ya kisasa katika Ukanda wa Ziwa maana itafungwa scanner yenye kuonesha kila kitu kilichobebwa ndani ya malori na vyombo vingine vya moto.


"Mizani hizi ni kwa ajili ya kusaidia barabara zetu zidumu zaidi hii ndio kitu ambacho kinafanya wasafirishaji wasizidishe mizigo na kuipunguzia Serikali gharama kubwa za ukarabati wa barabara" amesema Naibu Waziri huyo.


Akitoa taarifa ya mradi Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Eng. Vedastus Maribe, ameeleza kuwa maendeleo ya ujenzi wa mzani huo umefikia asilimia 50.6 na wanaendelea kuusimamia mradi ukamilike kwa muda uliopangwa.


Eng. Maribe ameongeza kuwa tayari kiasi cha Milioni 430 zimetumika kulipa wananchi kwa ajili ya fidia na eneo lipo wazi kwa ajili ya ukamilishaji wa mzani huo.


Naibu Waziri Kasekenya yupo mkoani Mara katika ziara ya ukaguzi wa miradi inayoendelea kutekelezwa na Sekta ya Ujenzi.

No comments:

Post a Comment