SERIKALI itaendelea kuuwezesha Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kujenga nyumba za kisasa kwa ajili ya watumishi wa Umma na za kibishara ili kukabiliana na ongezeko la mahitaji ya nyumba yanayoongezeka siku kwa siku nchini.
Akifungua Majengo kwa ajili ya makazi kwa watumishi wa Umma katika eneo la Magomeni Kota na Canadian Village Msasani Peninsula Masaki jijini Dar es Salaam Waziri wa Ujenzi na Uchkuzi Profesa Makame Mbarawa amesema nia ya Serikali ni kuhakikisha watumishi wake wanaishi katika makazi yaliyo bora na hivyo kuleta tija na ufanisi katika kazi za Umma.
“Lengo kuu la Serikali ni kuhakikisha watumishi wanapata makazi salama na ya kisasa yanayoendana na sayansi na teknolojia., hivyo TBA hakikisheni wapangaji wote watakaopata nafasi ya kuishi kwenye nyumba hizi wanalipa kodi kwa wakati’ amesema Waziri Prof. Mbarawa.
Prof. Mbarawa amesema Serikali inatambua umuhimu wa makazi bora kwa wananchi wake ambapo mahitaji ya nyumba bora yanakadiriwa kuwa zaidi ya nyumba milioni tatu kwa nchi nzima hivyo Serikali itaendeelea kujenga nyumba za ghorofa zitakazoweza kuhudumia watumishi wengi katika eneo dogo.
Waziri Prof Mbarawa amewtaka TBA kuhakikisha watakaopanga kwenye nyumba hizo wanazitunza kwa kuzingatia kanuni za usafi na matumizi bora ya nyumba ili zidumu kwa muda mrefu.
“Watakaoshindwa kulipa kodi kwa wakati watoeni muweke wengine tunataka nyumba hizi ziweze kukusanya fedha na fedha hizo hizo zitumike kujenga nyumba nyingine nyingi zaidi’ amesisitiza Waziri Prof. Mbarawa.
Naibu Katibu Mkuu wa Ujenzi, Bw. Ludovick Nduhiye amesema Wizara itaiwezsha TBA kwa kuipa fedha ili kutimiza malengo ya Serikali .
Kwa upande Wake Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miudombinu, Mhe Selemani Kakoso ameipongeza Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kwa namna inavyofanya kazi kwa ubora na ubunifu na kuitaka Wizara kuiwezesha TBA kukusanya madeni wanayodai watumishi mbalimbali ili kujiimarisha kiuchumi na kujenga miradi mingine.
“Mfumo mpya mliuoanzisha sasa wa kukusanya kodi ambao utamuwezesha mwenye nyumba kulipa kodi kwa wakati utasaidia kupata makusanyo kwa wakati na hivyo kutimiza malengo hivyo uendelezeni’ amesisitiza Mhe. Kakoso.
Mtendaji Mkuu wa TBA, Arch. Daud Kondoro amesema ujenzi wa nyumba za kisasa katika maeneo ya Magomeni kota na Canadian village jijijini Dar es Salaam ni mwendelezo wa Wakala huo kujenga nyumba za watumishi katika maeneo mbalimbali nchini ambapo miradi kama hiyo inaendelea katika eneo la Nzuguni-Dodoma, Mtwara, Shinyanga, Kilimanjaro na Kagera lengo likiwa kukabiliana na upungufu wa nyumba bora kwa watumishi wa umma.
Zaidi ya Shilingi bilioni kumi zimetumika katika ujenzi wa miradi miwili ya Magomeni Kota na Canadian Village na nyumba hizo zina uwezo wa kuhudumia familia 28 kwa wakati mmoja.
(Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi)
No comments:
Post a Comment