WAWAKILISHI kutoka Mashirika mbalimbali yasiyo kuwa ya Kiserikali hapa nchini (NGO’s) yanayotekeleza miradi ya afya wamesema Elimu ya Afya kwa Umma, Idara ya Kinga, Wizara ya Afya ni Mama na Baba katika kufanikisha utekelezaji wa Miradi yao hapa nchini.
Wakizungumza katika kikao kazi cha pamoja kati ya Wadau wa Maendeleo na Serikali kuhusu kuainisha vipaumbele na mikakati ya utekelezaji (Health Promotion priority interventional activities) kwa mwaka 2023/2024 kinacholenga kuwa na Mpango wa Utekelezaji wa Afua za Elimu ya Afya kwa Umma (Health Promotion Annual Work Plan) na kuainisha vyanzo vya fedha za utekelezaji wa afua za kipaumbele baadhi ya Wadau hao akiwemo mwakilishi Shirika la Afya Duniani (WHO) Jeryy Mlembwa wamesema kuwa Wizara ya Afya kupitia Elimu ya Afya kwa Umma ni muhimu kuweka nguvu ya pamoja katika ushirikiano.
“Wizara ya Afya kupitia Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma mmepewa Majukumu kama walezi wetu katika utekelezaji wa miradi yetu ya Afua za Afya hivyo niwaombe na wadau wenzangu kuanzia leo tutambue tunapokwenda kutekeza miradi ya Elimu ya Afua za Afya tusiende moja kwa moja huko bila kuwashirikisha Elimu ya Afya kwa Umma hasa Masuala ya Uelimishaji, sisi kama WHO mojawapo ya kanuni tunazosisitiza wadau ni kuwa na mfumo unaotuunganisha pamoja katika utekelzaji wa afua za afya,” amesema Mlembwa Mwakilishi WHO.
"Elimu ya Afya kwa Umma ni kama Moyo wa Wizara ya Afya, sisi sote kama wadau tunapotekeleza masuala mbalimbali ya Afya ni muhimu kuwashirikisha na tukifanya bila uwashirikisha ni sawa na bure," amesema Dkt. May Bukuku mwakilishi kutoka UNICEF.
"Tunapotekeleza miradi ya afua za Afya huko kijijini hasa afya ngazi ya jamii lazima Wizara ya Afya kupitia Elimu ya Afya kwa Umma ijue na inapojua yenyewe inakuwa na mchango mkubwa katika masuala ya Uelimishaji hivyo ni Muhimu kuhishirikisha Elimu ya Afya kwa Umma" amesema Mussa Lunnyonga Mwakilishi AMERICARES.
Beatrice Mkani kutoka SIKIKA amesema Wizara ya Afya ni mlezi Mkuu katika utekelezaji wa Majukumu yao.
"Elimu ya Afya kwa Umma, Wizara ya Afya ndio Mlezi mkubwa anayetekeleza masuala ya Promotion kwa afua za Afya hivyo tunapokwenda kutekeleza tusiwaache nyuma tupite kwanza kwao kwa ushauri na ushirikiano kwa hakika tunaweza kuifikia jamii katika mwelekeo wenye Mpangilio zaidi," amesema Beatrice.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kikao hicho ambaye ni mwakilishi kutoka Elimu ya Afya kwa Umma, Idara ya Kinga, Wizara ya Afya, John Yuda amesema wao kama Serikali wanatambua mchango Mkubwa unaotolewa na Mashirika yasiyokuwa ya Kiserikali hivyo jitihada za pamoja zinahitajika hasa katika suala la uelimishaji.
“Tunatambua mchango Mkubwa unaotolewa na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kinachohitajika tu ni wote tushirikiane hasa katika afua hii ya Elimu ya Afya,” amesema Yuda.
Naye Msimamizi wa Ubunifu na Maudhui, Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma, Wizara ya Afya James Mhilu amesema mitandao ya kijamii katika ulimwengu wa sasa ina nguvu na kasi kubwa ndio maana Elimu ya Afya kwa Umma imewekeza zaidi huko na kuwaondoa hofu wadau kuwa wanapowekeza huko ujumbe unafika kwa jamii kwa wakati na haraka zaidi.
“Katika Ulimwengu wa sasa Mitandao ya Kijamii ina nguvu sana, na unaweza kujiuliza kitu kimesambaa mtandaoni lakini unashangaa habari ya kitu hicho imefikaje kijijini sehemu ambako hakuna Internet? kuna mbinu mbalimbali zinazotumika mfano mtu mwenye simu yenye uwezo wa Mtandao (Internet) anaichukua kisha anasambaza kwa ujumbe wa kawaida,” amesema James.
Hivyo, kutokana na mitandao ya kijamii kuwa nguvu zaidi, hivi karibuni jijini Dodoma Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teklonojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye alizindua Taasisi ya Waandishi wa Habari wa Mtandaoni (TOMA] yenye Makao Makuu yake jijini Arusha.
Mratibu wa Elimu na Mabadiliko ya Tabia Elimu ya Afya kwa Umma, Idara ya Kinga, Wizara ya Afya Peter Mabwe amesema kikao hicho kitaleta mabadiliko makubwa katika utekelezaji wa majukumu hasa katika afua za Afya.
Ikumbukwe kuwa kikao kazi cha pamoja kati ya Wadau wa Maendeleo na Serikali kuhusu kuainisha vipaumbele na mikakati ya utekelezaji (Health Promotion priority interventional activities) kwa mwaka 2023/2024 kilianza tarehe 13, Februari,2023 na kitaendelea hadi tarehe 17, Februari, 2023 huku kikihusisha washiriki kutoka Wizara ya Afya, OR-TAMISEMI, Wadau mbalimbali ikiwemo mwakilishi kutoka Shirika la Kuhudumia Watoto Duniani (UNICEF], PSI, USAID, PACT, TCDC, SIKIKA, D-Tree, Marie Stopes, World Vision, Save the Children, TRCS, EGPAF, AMERICARES, Mkapa Foundation, Girl Effect Apotheker, na T - Marc Tanzania.
Hata hivyo kikao kazi hicho, kitaleta mabadiliko katika utekelezaji wa afua mbalimbali za afya hapa nchini ambapo leo ni siku ya tano tangu kianze siku ya Jumatatu huku wadau wengine wakishiriki kwa njia ya Mtandao.
No comments:
Post a Comment