MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa utabiri kuonesha mwelekeo wa mvua za Masika zinazotarajia kuanza mwezi Machi hadi Mei, 2023 na kubainisha kuwa mvua hizo zitakuwa za wastani hadi chini ya wastani katika maeneo mengi nyanda za juu kaskazini mashariki kujumuisha Mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro.
Akizungumza na vyombo vya habari akitoa utabiri huo leo jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugunzi Mkuu wa TMA, Dkt. Ladislaus Chang’a aliitaja mikoa itakayo kumbwa na hali hiyo pia ni pamoja na Pwani ikijumuishwa mkoa wa Morogoro, visiwa vya Mafia, Dar es Salaam, Tanga na visiwa vya Unguja na Pemba. Aliongeza kuwa hali hiyo itajitokeza pia ukanda wa Ziwa Victoria unaojumuisha Mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Mara) pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma.
"Kutokana na mifumo ya hali ya hewa inayotarajiwa katika kipindi cha msimu kwa ujumla mvua zitakuwa za wastani hadi chini ya wastani katika maeneo mengi ya mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Mara, Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Tanga pamoja kisiwa cha Pemba katika msimu wa mvua za Masika, 2023.
"Hata hivyo, mvua za wastani hadi juu ya wastani zinatarajiwa katika maeneo ya mikoa ya Dar es Salaam, Pwani (ikiwemo visiwa vya Mafia), kaskazini mwa mkoa wa Morogoro na kisiwa cha Unguja, huku Ongezeko la mvua likitarajiwa mwezi Mei, 2023 katika maeneo hayo.
Aliongeza kuwa kwa Kanda ya Ziwa Victoria: Mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, na Mara pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma katika wilaya za Kakonko na Kibondo Mvua za Masika zinatarajiwa kuwa za wastani hadi chini ya wastani katika maeneo mengi ya ukanda wa Ziwa Victoria pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma. Mvua hizo zinatarajiwa kuanza wiki ya kwanza na ya pili ya mwezi Machi, 2023 na zinatarajiwa kuisha wiki ya nne ya mwezi Mei, 2023," alisema, Dkt. Chang’a
Alibainisha kuwa mvua za wastani hadi juu ya wastani zinatarajiwa pia kwa mikoa ya Dar es Salaam, Pwani ikiwemo visiwa vya Mafia, kaskazini mwa mkoa wa Morogoro na kisiwa cha Unguja; huku mvua za wastani hadi chini ya wastani zikitarajiwa kunyesha katika maeneo ya mkoa wa Tanga pamoja na kisiwa cha Pemba kuanzia wiki ya pili na ya tatu ya mwezi Machi, 2023 na kuisha Juni, 2023.
Aidha kwa Mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro Mvua katika maeneo hayo zinatarajiwa kuwa za wastani hadi chini ya wastani huku zikitegemewa kuanza wiki ya pili na ya tatu ya mwezi Machi, 2023 na zinatarajiwa kuisha wiki ya tatu na ya nne ya mwezi Mei, 2023.
TMA imewaomba watumiaji wote wa taarifa za hali ya hewa ikiwa ni pamoja na wakulima, wafugaji, mamlaka za wanyamapori, wasafirishaji, mamlaka za maji na afya kuendelea kutafuta, kupata na kuzingatia ushauri wa wataalam katika sekta husika ili ziweze kuwasaidia katika shughuli zao.
No comments:
Post a Comment