Muonekano wa kazi ikiendelea katika ujenzi wa Barabara ya Bugene-Kasulo-Kumunazi (KM 128.5) sehemu ya Bugene hadi Burigi (KM 60) inayojengwa kwa kiwango cha Lami, Mkoani Kagera. |
WAZIRI wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amewataka Wakazi wa Mkoa wa Kagera na Geita kutumia fursa ya ujenzi wa barabara ya Lusahunga hadi Rusumo (KM 92) kwa kiwango cha lami kuongeza uzalishaji katika mazao ya kilimo biashara na vivutio vya utalii ili kunufaika na uwepo wa mradi huo.
Akizungumza Wilayani Ngara, Mkoani Kigoma katika hafla ya utiaji saini wa ujenzi wa barabara hiyo Prof.Mbarawa amesema nia ya Serikali ni kuhakikisha inaweka miundombinu bora ya kiuchumi ili kuwawezesha wananchi kubuni fursa na kunufaika na miradi mikubwa inayoendeshwa na Serikali.
“Barabara hii ni kiungo muhimu katika nchi za Afrika Mashariki kwa usafirishaji wa bidhaa za nchi za Rwanda, Burundi, Kongo na Uganda zinazokwenda na zinazotoka bandari ya Dar es Salaam’ amesema Waziri Prof. Mbarawa.
Waziri Prof. Mbarawa amesisitiza kuwa barabara hiyo itakapokamilika itapunguza kero na ajali kwa watumiaji wa barabara hiyo na itaongeza ufanisi katika huduma za uchukuzi nchini.
“Usafirishaji wa mazao ya kilimo, utalii wa hifadhi ya Burigi na Rubondo ni miongoni mwa fursa zitakazoboreshwa na uwepo wa barabara hii’ amesisitiza Waziri Prof. Mbarawa.
Ameutaka Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) na wataalam mbalimbali watakaoshiriki katika mradi huo kuwa wazalendo na kujielimisha vyakutosha ili kujenga uzoefu na kuwaonya wananchi wanaopata fursa katika ujenzi wa barabara kuacha vitendo vya wizi na hujuma kwani kufanya hivyo kunaitia doa na hasara Serikali.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kagera Bw, Albert Chalamila amewahimiza wananchi kuzalisha kwa wingi mazao ya chakula na biashara ili kunufaika na miradi mikubwa ya kitaifa inayoendelea mkoani humo.
“Ndugu zangu Serikali imewekeza miundombinu ya fedha nyingi katika mkoa wetu ni vizuri tukajiuliza tutatumiaje fursa hii kunufaika kiuchumi’ amesisitiza Mkuu wa Mkoa Chalamila.
Naye Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Rogatus Mativila amesema ujenzi wa barabara ya Lusahunga hadi Rusumo (KM 92) ni moja ya mikakati ya Serikali ya Tanzania kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini.
“Tumejipanga kumsimamia mkandarasi kikamilifu ili barabara hii ikamilike kwa muda wa miezi 24 kama ilivyopangwa na kwa ubora unaoendana na thamani ya fedha’ amesema Mhandisi Mativila.
Barabara hiyo inayojengwa na Mkandarasi China Civil Enginerring Construction Corporation (CCECC) ya nchini China inatarajiwa kugharimu kiasi cha bilioni 153 itakapokamilika.
Katika hatua nyingine Prof. Mbarawa amekagua Ujenzi wa Barabara ya Bugene-Kasulo-Kumunazi (KM 128.5) sehemu ya Bugene hadi Burigi (KM 60) na kumtaka Mkandarasi kampuni ya China Road and Bridge Corporation (CRBC) kuongeza kasi katika ujenzi wa mradi huo ili kuunganisha kirahisi Wilaya za Ngara na Karagwe kupitia hifadhi ya Burigi-Chato.
Waziri Prof. Mbarawa amesisitiza umuhimu wa uadilifu na uzalendo kwa wafanyakazi wanaoendelea na ujenzi wa mradi huo na kuwataka kuhakikisha unakamilika kama kama ilivyopangwa ifikapo Novemba 2024.
(Imetolewa Na Kitengo Cha Habari Na Mawasiliano Serikalini Wizara Ya Ujenzi Na Uchukuzi)
No comments:
Post a Comment