POPO WA NIGERIA KIVUTIO KINGINE MAKUMBUSHO YA MAJIMAJI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Sunday, 19 February 2023

POPO WA NIGERIA KIVUTIO KINGINE MAKUMBUSHO YA MAJIMAJI

Moja ya popo wakubwa dunaini wanaolingana na kunguru ambao wanafika ndani ya Makumbusho hayo kuanzia mwishoni mwa mwezi Novemba kila mwaka na kuzaliana kisha huondoka mwishoni mwa mwezi Februari. Inaaminika popo hao wanatoka nchini Nigeria.

MAKUMBUSHO ya Taifa ya Majimaji ni eneo ambalo limehifadhiwa vizuri na serikali ili kuwawezesha watu kujifunza kumbukumbu nyingi ambazo ni kivutio adimu cha utalii wa kishujaa na kiutamaduni. 

Watu  kutoka mkoa wa Ruvuma na  nje ya nchi wanatembelea eneo hili maarufu katika historia ya Tanzania hasa katika harakati ambazo zilifanywa na babu zetu kupambana na wakoloni ili kujitawala wenyewe bila kunyonywa.

Mkurugenzi wa  makumbusho ya Taifa ya Majimaji mhifadhi Kiongozi Balthazar Nyamusya anasema eneo hilo la makumbusho lina historia tatu ambazo ni historia ya vita vya majimaji, historia ya ujio wa wangoni kutoka Afrika ya Kusini na  historia ya uhuru wa Tanganyika. 

Anaitaja historia ya vita vya majimaji ililenga kumkomboa mtanzania kutoka mikononi mwa wakoloni Wajerumani na kwamba sio sahihi kuwa vita hiyo ilikuwa na uwezo wa kugeuza risasi kuwa maji bali ililenga kuwapa nguvu wapiganaji kujitolea hata ikibidi kupoteza maisha ili kujikomboa.

“vita vya majimaji vilianza mwaka 1905 na ilianzia Kilwa na sio Songea, ingawa vita hiyo ilipiganwa katika kanda ya kusini lakini Songea inazungumziwa zaidi kwa sababu watu wote waliokamatwa walinyongwa na kuzikwa Songea katika kaburi moja la pamoja ambalo walizikwa watu 68,’’ anasema Nyamusya. 

Historia ya Vita vya Majimaji inaonesha kuwa awali walikamatwa machifu 48 na baadaye kukamatwa wengine ambapo idadi ya machifu walionyongwa na kuzikwa katika kaburi moja ilifikia 66.

Unyongaji wa mashujaa hao ulifanyika Februari 27 mwaka 1906, Machi 20,1906 na Aprili 12,1906 katika eneo la Songea club mjini Songea pamoja na eneo la Mahenge mashujaa ambapo walizikwa kaburi moja.

“Siku ya kuwanyonga mashujaa hao watu wengine  walikusanyika wakasimamishwa mahali ambapo waliweza kuwaona wanyongwaji ili waone eti wasiige na wao kwa kuwa watanyongwa,” alisema Samwel Gama Mwenyekiti wa Baraza la wazee Makumbusho ya Taifa ya Majimaji.

Gama anabainisha zaidi kuwa wanyongwaji waliletwa katika eneo hilo wakiwa wamefungwa kila mmoja mnyororo mdogo uliofungwa kwenye mnyororo mkubwa  na kwamba katika eneo hilo nguzo kubwa mbili zilisimikwa pande mbili.

Anasema juu ya nguzo hizo kulipigiliwa nguzo imara iliyofungwa vitanzi vinne ambapo chini ya nguzo hizo kulikuwa na ubao uliowekwa juu ya nguzo fupi nne.

“Basi waliwafunga wafungwa wanne toka mnyororo ule mkubwa na wakawasimamisha juu ya ule ubao uliotegeshwa, wakawapachika zile kamba zilizoning’inia, kila mmoja na kamba yake huku wakiwa wamefungwa kamba mikono yote miwili ili wasiweze kujimudu na nyuso zao zilikuwa zimefungwa vitambaa vyekundu ili wasiweze kuona,” anasisitiza Gama.

Ili kuwasitiri  Gama anasema wanyongwaji hao walifungwa shuka ndogo ili kusitiri uchi wao na kuongeza kuwa askari alifyatua ubao na ndipo miili ya mashujaa hao ikwa inaning’nia kwenye vitanzi mpaka wakakata roho.

“Baada ya mashujaa hao kukata roho katika mateso makali wauaji hao waliiondoa miili hiyo na kuiweka kando katika sehemu hiyo waliowanyongea na kwamba waliwanyonga watu wanne kwa wakati mmoja na kufanya siku ya kwanza yaani Februari 27,1906 kunyonga watu 40”, anaeleza Gama.

Hata hivyo anasema  mashujaa walionyongwa vitanzini walikuwa 68, waliokufa gerezani kabla ya kunyongwa walikuwa wawili, waliopigwa risasi kuonesha nguvu ya risasi walikuwa watano na kufanya jumla mashujaa 75 kuuawa kikatili.

Kulingana na Mwenyekiti huyo wa Baraza la wazee, kaburi kubwa lililochimbwa na wafungwa kwa mwezi mmoja katika eneo la mashujaa mjini Songea ambalo limetengwa eneo la kumbukumbu ya mashujaa wa vita vya majimaji.

“maiti ya mashujaa walionyongwa kwa siku moja ililazwa katika kaburi hilo kiubavu bila sanda na kufukiwa kidogo ili kutoa nafasi kwa maiti wengine siku nyingine ili waje kulazwa  juu ya wale wa kwanza na kufikia tena kidogo mpaka wote walionyongwa watakapozikwa katika kaburi moja kubwa’’, anasema Gama.

Hata hivyo anasema chifu  wa wangoni yaani Nduna Songea Mbano hakuzikwa katika kaburi moja na wenzake kwa kuwa yeye aliuawa siku ya peke yake tarehe 4/3/1906 baada ya wengine wote kunyongwa.

Anasema chifu Songea Mbano alikuwa ndiyo Jemedari Mkuu wa Jeshi la wangoni na alikuwa ni hodari sana asiyeogopa lolote kwa hiyo wajerumani walitaka abakie ili wamtumie kwa malengo yao.

“Chifu Songea alidai na yeye anyongwe kama walivyonyongwa ndugu zake, basi alinyongwa na wajerumani waliondoka na kichwa chake wakakiweka ndani ya kasha na kuondoka nacho kwenda Ujerumani ambako hakijarudi hadi leo”, anadai Gama.

Anabainisha kuwa mwili wa chifu Songea Mbano ukiwa  kiwiliwili bila kichwa ulizikwa katika kaburi la pekee yake katika eneo la mashujaa la mjini Songea na kuongeza kuwa mashujaa wote hao walionyongwa na kuzikwa walikuwa na imani zao mbalimbali za kidini.

Mhifadhi Kiongozi wa Makumbusho ya Taifa Philipo Maligisu anasema kuwa katika makumbusho ya Taifa ya Majimaji zimewekwa kumbukumbu zote muhimu za historia ya majimaji ambapo watu wengi kutoka ndani na nje ya nchi wanafika kuangalia makumbusho  haya ambayo yamekuwa ni kivutio kikubwa cha utalii.

Historia inaonesha kuwa Songea ndiyo ilikuwa  sehemu ya kwanza ya kupima uwezo wa dawa ya Majimaji kabla ya kwenda katika maeneo mengine ya kusini ambako vita hiyo ilipiganwa. 

Hata hivyo anasema vita hiyo ilianza kupigwa katika eneo la Kilwa Kivinje wilaya ya Utete ikiongozwa na Kinjekitile na wenzake na  walifanikiwa kuchoma boma za wajerumani baada ya kwenda huko usiku na sio mchana.

“Dawa ya majimaji iliaminika kuwa inafaa  baada ya kujaribiwa katika eneo la Songea na wajumbe wote waliokuwa wanakwenda kuchukua ile dawa waliliridhika na ubora wa  dawa ambapo Kinjekitile Ngwale alikuwa ni mwanzilishi wa dawa hiyo pamoja na vita yenyewe ya majimaji’’,anasema Maligisu mhifadhi kiongozi wa makumbusho ya Taifa.

Katika makumbusho ya Taifa ya majimaji kuna kumbukumbu ya silaha mbalimbali walizotumia mashujaa wa majimaji kupigana na mkoloni ukiwemo mkuki ambao ulipatikana nyumbani kwa chief Songea Mbano wa kabila la wangoni ambaye alikuwa anautumia mwenyewe katika mapigano.

Makumbusho hayo pia yana vitu mbalimbali vya kale vikiwemo mafiga ya mawe, kiko, majembe ya kale pia kuna chungu kikubwa alichokuwa anatumia chifu Songea Mbano ambacho kilikuwa kinatumika kuhifadhia mazao kama vile karanga ambacho kilifukiwa mwaka 1905.

Chungu hicho kiligundulika mwaka 1980 katika eneo la Mputa wilayani Namtumbo ambapo mtu mmoja wakati analima shamba lake  alikigonga chungu hicho na alipoangalia akakuta karanga nyingi na inaaminika chungu hicho alikuwa anatumia mke wa chifu Mputa wa Songea. 

Ndani ya makumbusho ya Taifa ya majimaji kuna picha mbalimbali ambazo zinaonesha wapigania uhuru wa kwanza akiwemo hayati baba wa Taifa Julius Nyerere, mzee Rashid Kawawa na picha za tukio la muungano wa Tanganyika na Zanzibar kuwa nchi moja ya Tanzania.

Licha ya kuwepo historia hizo, makumbusho ya Taifa ya Majimaji imepata aina nyingine ya kivutio cha utalii baada ya kubainika katika makumbusho hayo kuna aina ya spishi ya popo wakubwa duniani ambao asili yake ni nchini Nigeria.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, popo hao wa aina yake kila mwaka kuanzia Oktoba wanafika katika Makumbusho hayo na kuweka makazi kwenye eneo la miti mikubwa iliyopo  katika kaburi la pamoja ambalo wamezikwa mashujaa 67.

“Hawa popo wanaokadiriwa kuwa kati ya 6000 hadi 10,000 wakifika hapa wanaishi kuanzia Oktoba hadi Februari kila mwaka, kutokana na uzito wa popo hawa baadhi ya matawi ya miti mikavu inaanguka na miti mingine inainama kutokana na uzito’’, anasisitiza Nyamusya.

Hata hivyo utafiti unaonesha kuwa popo wakubwa kuliko wote duniani wanapatikana hapa nchini katika visiwa vya Pemba na Zanzibar.

Kwa mujibu wa taarifa ya Mtafiti Ng’oko Innocent, popo wanaopatikana katika visiwa hivyo wanafahamika kwa  jina la flying fox bat au fruit bat ambao wanatajwa kuwa ndiyo popo wakubwa kuliko wote duniani hivyo kuwa kivutio kikubwa kwa watalii.

Ukubwa wa popo hao unakadiliwa kufikia gramu 400 hadi 650 na kwamba wana mabawa yenye urefu wa mita 1.6 wakiwa na  sura inayofanana na mnyama aina ya mbweha.

Anasema Popo hao ambao baadhi yao wapo katika msitu wa bandari ya Wete Pemba wana rangi ya chungwa sehemu ya tumbo na wana masikio, pua na mabawa meusi ambapo  mara nyingi ukiwa katika kisiwa hicho popo hao wanapatikana kwenye misitu mikubwa yenye asili ya matunda.

Kisayansi popo wana faida  kubwa ikiwemo ya kusambaza misitu kutokana na kula matunda ya aina mbalimbali na kuchavusha maua na kwamba popo hupendelea misitu yenye mvua.

Popo hujamiana kati ya Januari hadi Juni ambapo jike huzaa mtoto mmoja kwa mwaka.Inakadiriwa popo wana uwezo wa kuishi kati  ya miaka 15  hadi 30 ingawa  baadhi yao hufikisha hadi miaka 40.

Imeandikwa na Albano Midelo wa Kitengo cha Mawasiliano Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Ruvuma.


No comments:

Post a Comment