WATANZANIA WATAKIWA KUZINGATIA SHERIA, KANUNI NA TARATIBU ZA NCHI WALIZOKO ILI KULINDA TASWIRA YA NCHI YAO - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Wednesday 25 January 2023

WATANZANIA WATAKIWA KUZINGATIA SHERIA, KANUNI NA TARATIBU ZA NCHI WALIZOKO ILI KULINDA TASWIRA YA NCHI YAO

Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb).

WATANZANIA wametakiwa kuwa mabalozi wazuri katika nchi za ugenini, wazingatie na kufuata sheria, kanuni na taratibu za nchi hizo ili kulinda taswira nzuri ya nchi yao.

Rai hiyo imetolewa jijini Dar es Salaam na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb) alipozungumza na waandishi wa habari kuelezea taarifa kuhusu kifo cha Mtanzania aliyefariki dunia nchini Urusi.

Ameongeza kwa mujibu wa sheria za Tanzania, Mtanzania yeyote haruhusiwi kujiunga na Jeshi la nchi yoyote duniani zaidi ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania kwa kufuata taratibu zilizopo na atakayefanya hivyo atakuwa amevunja sheria.

“Nitoe rai kwa Watanzania wote kuhakikisha wanazingatia Sheria, za nchi yetu, na kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu za nchi walizopo, na pia wawe mabalozi wazuri wa kulinda taswira ya nchi yetu. Ikumbukwe kuwa kwa mujibu wa sheria zetu, Mtanzania yoyote haruhusiwi kujiunga na jeshi la nchi yoyote isipokuwa Jeshi la Tanzania na kufanya hivyo ni kuvunja sheria”, amesema Dkt. Tax.

Akiongelea kuhusu kifo cha Bwana Nemes Tarimo kilichotokea Urusi Mhe. Dkt. Tax amesema Mtanzania huyo alikwenda nchini humo mwaka 2020 kwa ajili ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Moscow Technological University (MIREA) kwa masomo ya Shahada ya Uzamili katika fani ya Business Informatics.

Amesema Mwezi Machi 2022, Mtanzania huyo alitiwa hatiani kwa kuhusika na vitendo vya uhalifu na kwa mujibu wa Sheria za Urusi alihukumiwa kifungo cha miaka saba (7) jela.

Ameongeza kuwa akiwa gerezani Bw. Tarimo alijiunga na kikundi cha kijeshi cha Urusi chaWagner kwa ahadi ya kulipwa fedha na kuachiwa huru baada ya kumaliza muda wa kutumika kwenye vita na alifikwa na umauti tarehe 24 Oktoba, 2022 akiwa nchini humo.

Amesema Serikali imekuwa ikiwasiliana na Serikali ya Urusi ili kuhakikisha mwili wa Marehemu Tarimo unarejeshwa nchini na kukabidhiwa kwa familia yake ili taratibu za mazishi ziweze kufanyika kwa kuzingatia mila na desturi za Kitanzania na kuongeza kuwa mwili wa marehemu umeondoka nchini Urusi tarehe 24 Januari na unatarajiwa kuwasili nchini muda wowote kuanzia sasa.

Mhe. Waziri ametoa pole kwa familia ya marehemu, ndugu, jamaa na Watanzania kwa jumla kufuatia msiba huo na ameiombea roho ya marehemu Nemes ilazwe pema peponi.

Mhe. Waziri amewauhakikishia umma na Diaspora wa Kitanzania wakiwemo wanafunzi walioko masomoni nchini Urusi kuwa Serikali kupitia Ubalozi wake uliopo nchini Urusi itaendelea kuwapa ushirikiano na kuhakikisha Watanzania hao wako salama wakati wote.

No comments:

Post a Comment