MKOA WA RUVUMA NA MKOA WA MOROGORO KUUNGANISHWA KWA BARABARA YA LAMI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Sunday 22 January 2023

MKOA WA RUVUMA NA MKOA WA MOROGORO KUUNGANISHWA KWA BARABARA YA LAMI

 

Barabara ya Songea - Makambako mkoani Njombe ambayo inaunganisha mikoa ya Ruvuma na Njombe, serikali  mwaka huu inatarajia kuanza ujenzi wa barabara hiyo kwa kuanzia kilometa 111 kutoka Songea hadi Lutukira Madaba.

Na Albano Midelo, Ruvuma

SERIKALI kupitia Wakala za Barabara TANROADS inatarajia kuanza mradi wa kuunganisha Mkoa wa Ruvuma na Mkoa wa Morogoro kwa barabara ya lami. Mkoa wa Ruvuma ni miongoni mwa mikoa nchini ambayo tayari wilaya zake zote zimeunganishwa kwa lami na makao makuu ya Mkoa.

Meneja wa TANROADS Mkoa wa Ruvuma Mhandisi Ephatar Mlavi amesema serikali inatarajia kutekeleza mradi wa ujenzi wa barabara ya Lumecha – Londo wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma hadi Kilosa – Kidatu mkoani Morogoro kwa kiwango cha lami.

 Mhandisi Mlavi ameutaja mradi huo kuwa utahusisha ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami, yenye urefu wa kilometa 512 ambao ukikamilika utaunganisha Mkoa wa Ruvuma na Morogoro kwa kiwango cha lami.

“Mradi huu upo katika hatua ya kupitia zabuni za wakandarasi ambapo zilifunguliwa tarehe 26 Agosti 2022. Mradi huu utatekelezwa kwa kutumia mtindo wa Usanifu, Manunuzi, Ujenzi na Ufadhili (Engineering, Procurement, Construction and Financing,” alisema Mhandisi Mlavi. 

Hata Hivyo Meneja huyo wa TANROADS Mkoa wa Ruvuma amesema utekelezaji wa mradi huo unatarajia kuanza muda wowote baada ya hatua stahiki za manunuzi kukamilika.

Akizungumzia ujenzi wa Barabara ya Songea – Makambako kwa kiwango cha lami, Mhandisi Mlavi amesema serikali ya Awamu ya Sita inatarajia pia kutekeleza mradi wa ujenzi wa barabara ya lami sehemu ya Songea – Lutukira ikijumuisha na sehemu ya Mtwara korido yenye urefu wa kilometa 111.


Mhandisi Mlavi amesema katika utekelezaji wa mradi huo, Serikali tayari imeshaingia makubaliano na Mfadhili ambaye ni Benki ya Dunia na hivi sasa hatua za mradi huo zipo katika hatua za awali za manunuzi.

Amebainisha Zaidi kuwa mradi huo utahusisha ujenzi wa kilometa 111 za lami ambazo zitajumuisha kilometa 14 za Songea bypass katika Manispaa ya Songea na ujenzi wa barabara ya Songea hadi Lutukira Halmashauri ya Madaba yenye urefu wa kilometa 97 hivyo kuunganisha wilaya ya Songea mkoani Ruvuma na wilaya ya Njombe mkoani Njombe.

Hata hivyo amesema Mkoa wa Ruvuma kupitia Wilaya ya Nyasa tayari umeunganishwa na  Mkoa wa Njombe kupitia wilaya ya Ludewa kwa kutumia  daraja la mto Ruhuhu unaomwaga maji yake ziwa Nyasa. 

Amesema mradi wa daraja la Ruhuhu ulianza kutekelezwa Juni 2016 na kukamilika Oktoba 2021 kwa gharama ya Zaidi ya shilingi bilioni 8.9 ambao umeunganisha wilaya za Nyasa na Ludewa.

Katika mwaka wa fedha 2022/2023, TANROADS Mkoa wa Ruvuma iliomba bajeti ya Zaidi ya shilingi bilioni 41 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo. Hata hivyo, kiasi cha Zaidi ya Shilingi 28 ndiyo kimeidhinishwa kwenye bajeti ya 2022/2023.

No comments:

Post a Comment