| Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa akizungumza alipokuwa akifungua Mkutano wa 15 wa mwaka wa tathmini ya utendaji sekta ya uchukuzi leo jijini Dar es Salaam. |
| Sehemu ya wadau mbalimbali wa sekta ya uchukuzi wakiwa katika Mkutano wa 15 wa mwaka wa tathmini ya utendaji sekta ya uchukuzi leo jijini Dar es Salaam. |
MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema taarifa za hali ya hewa zina umuhimu mkubwa katika sekta ya uchukuzi, kwa kuwa uendeshaji wa shughuli za sekta hiyo hutegemea sana taarifa za utabiri wa hali ya hewa.
Kauli hiyo imetolewa jijini Dar es Salaam na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Bw. Wilbert Muruke alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kwenye mkutano wa 15 wa mwaka wa wadau wa sekta ya uchukuzi uliowakutanisha wadao hao kufanya tathmini kuhusu maendeleo ya sekta hiyo.
Alisema TMA kupitia taarifa zake za utabiri wa hali ya hewa unaisaidia sekta ya uchukuzi katika kutekeleza shughuli zake, zikiwemo usafiri wa anga (ndege), usafiri wa majini, pamoja na shughuli zingine za ujenzi wa miundombinu ya sekta ya usafirishaji kama barabara na reli.
“...Huduma za hali ya hewa ni mtambuka kwa sekta mbalimbali na mojawapo ya sekta ambayo tunaihudumia ni sekta ya usafirishaji ambapo katika ujenzi wa miundombinu mbalimbali ikiwemo viwanja vya ndege, reli, barabara na madaraja moja ya taarifa muhimu katika mipango yao ni taarifa za hali ya hewa zitakazowawezesha kupanga vyema mipango yao na hivyo kusaidia kuepusha hasara zitakazojitokeza kutokana na majanga yatokanayo na hali mbaya ya hewa,”. alisema Bw. Muruke.
Pamoja na hayo aliwashauri sekta wadau wa TMA kuendelea kufuatilia taarifa za utabiri wa hali ya hewa mara kwa mara ili kupunguza changamoto zinazoweza kusababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa hasa katika utekelezaji wa shughuli zao za ki-sekta.
Naye Meneja Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dkt. Patricia Laverley akizungumza na wadau wa sekta ya uchukuzi, ameishukuru Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kwa kuandaa mkutano huo wa tathmini wa kila mwaka ambao unaibua changamoto na kuzipatia ufumbuzi kwa haraka.
Amesema AfDB imetenga asilimia 60 ya bajeti yake katika uwezeshaji ujenzi wa miundombinu ili kuchochea maendeleo ya uchumi kwa nchi za Afrika.

No comments:
Post a Comment