SEKTA BINAFSI SHIRIKINI UJENZI WA MIUNDOMBINU - PROF. MBARAWA - THE HABARII

THE HABARII

HABARI | MATUKIO | MICHEZO.


ASAS GROUP

Habari Mpya


Wednesday, 16 November 2022

SEKTA BINAFSI SHIRIKINI UJENZI WA MIUNDOMBINU - PROF. MBARAWA

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa akizungumza alipokuwa akifungua Mkutano wa 15 wa mwaka wa tathmini ya utendaji sekta ya uchukuzi leo jijini Dar es Salaam.

Meneja Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dkt. Patricia Laverley (kushoto), pamoja na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa akipata maelezo toka kwenye Banda la Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) katika Mkutano wa mwaka wa tathmini ya utendaji sekta ya uchukuzi uliofanyika jijini Dar es salaam.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Bw. Wilbert Muruke (kushoto) akizungumza na waandishi wa habari kwenye mkutano wa 15 wa mwaka wa wadau wa sekta ya uchukuzi uliowakutanisha wadao hao kufanya tathmini kuhusu maendeleo ya sekta hiyo.

ya Afrika (AfDB), Dkt. Patricia Laverley (kushoto), akisaini kitabu cha wageni alipotembelea Banda la Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) katika Mkutano wa mwaka wa tathmini ya utendaji sekta ya uchukuzi jijini Dar es salaam leo.

Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), Eng. Kingdom Mbangula akifafanua jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani), kuhusiana na ujenzi wa barabara mpya ya kulipia Kibaha – Chalinze - Morogoro kilomita 215 (express way)inayotarajiwa kuanza kujengwa baadae mwakani.

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa akizungumza alipokuwa akifungua Mkutano wa 15 wa mwaka wa tathmini ya utendaji sekta ya uchukuzi leo jijini Dar es Salaam.

WAZIRI wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa amezungumzia umuhimu wa sekta binafsi kushirikiana na Serikali katika ujenzi wa miundombinu ili kuharakisha maendeleo na kukuza uchumi wa taifa na mtu mmoja mmoja.

Akifungua mkutano wa 15 wa mwaka wa wadau wa sekta ya uchukuzi wenye lengo la kufanya tathmini kuhusu maendeleo ya sekta hiyo nchini, Prof. Mbarawa amesema ushiriki wa sekta binafsi, Serikali na wadau wa maendeleo utaharakisha ujenzi wa reli, barabara, viwanja vya ndege na meli na hivyo kutoa fursa nyingi za ajira na kuhuisha miundombinu ambayo ni uti wa mgongo wa uchumi wa taifa.

“Serikali tumejipanga kushirikiana na sekta binafsi katika ujenzi wa barabara mpya ya Kibaha-Chalinze-Morogoro kilomita 215 (express way), ambapo mkandarasi atajenga kwa fedha yake na watakaotumia barabara hiyo watalipia,” amesema Prof. Mbarawa.

Amebainisha kuwa Serikali inajipanga kubadilisha sheria ya TAZARA na TRC ili kuwezesha sekta binafsi kushiriki katika huduma ya usafiri wa reli kwa kununua mabehewa na kuyaendesha.

Amezungumzia umuhimu wa Tanzania kuwa na miundombinu bora kwa haraka ili kumudu kuhudumia kikamilifu soko la ndani na nchi sita ambazo hutegemea huduma ya uchukuzi kutoka Tanzania, ambazo ni Malawi, Zambia, Burundi, Rwanda, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Kwa upande wake Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), Eng. Kingdom Mbangula akizungumzia ujenzi wa barabara mpya ya kulipia, amesema barabara hiyo itakuwa na njia nne, mbili kwenda Morogoro na Mbili kurudi Kibaha na magari hayatapishana ili kuepusha msongamano na ajali.

“ TANROADS tumejipanga ipasavyo kuhakikisha mradi huu unajengwa kwa ubora uliokusudiwa na kukamilika kwa wakati,” amefafanua Eng. Mbangula.

Naye Meneja Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dkt. Patricia Laverley ameishukuru Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi  kwa kuandaa mkutano huo wa tathmini wa kila mwaka ambao unaibua changamoto na kuzipatia ufumbuzi kwa haraka.

Amesisitiza kuwa AfDB imetenga asilimia 60 ya bajeti yake katika uwezeshaji ujenzi wa miundombinu ili kuchochea maendeleo ya uchumi kwa nchi za Afrika.

Katibu Mkuu sekta ya Uchukuzi Bw. Gabriel Migire amesema mkutano huo pamoja na mambo mengine utaibua hoja mbalimbali zinazolenga kuboresha sekta ya uchukuzi nchini hivyo kuvutia wawekezaji wengi kupitisha mizigo yao Tanzania na hivyo kukuza uchumi wa taifa.

Meneja Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dkt. Patricia Laverley (kushoto), akimsikiliza Ofisa Habari wa TAZARA, Bi. Regina Tarimo alipotembelea banda hilo kwenye Mkutano wa 15 wa mwaka wa tathmini ya utendaji sekta ya uchukuzi.

Mkurugenzi Msaidizi wa Barabara, Eng. John Ngowi (kushoto), akizungumza kwenye Mkutano wa 15 wa mwaka wa tathmini ya utendaji sekta ya uchukuzi leo jijini Dar es Salaam. Wengine kutoka kulia ni Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa pamoja na Meneja Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dkt. Patricia Laverley.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (sekta ya uchukuzi), Bw. Gabriel Migire kulia akizungumza katika Mkutano wa 15 wa mwaka wa tathmini ya utendaji sekta ya uchukuzi leo jijini Dar es Salaam. Wengine kutoka kushoto ni Meneja Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dkt. Patricia Laverley na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa.

No comments:

Post a Comment