SERIKALI KUPITIA UPYA SERA YA UTALII - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Wednesday, 5 October 2022

SERIKALI KUPITIA UPYA SERA YA UTALII

Kushoto ni Kamishna  wa Sera Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Elijah Mwandumbya akitoa ufafanuzi kwa wadau wa utalii (hawamo pichani) kulia ni Naibu Kamishna wa Hifadhi anayesimamia Kurugenzi ya Uhifadhi Pamoja na Huduma za Biashara ndani ya Shirika ya Hifadhi za Taifa Tanzania – TANAPA Bw. Herman Mbatio.

SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Fedha na Mipango inataka kupitia upya sera za utalii ili kuendana na uhalisia wa mazingira, hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Lawrence Mafuru alipokuwa akifungua kikao kazi na sekta binafsi chenye lengo la kupata uelewa zaidi kuhusiana na shughuli za utalii kilichofanyika jijini Arusha kwa njia ya  mtandao. 

“Sisi kama Wizara ya Fedha na Mipango jukumu letu kubwa ni kutengeneza au kuandaa Sera za uchumi na Sera za kibajeti au Sera za fedha. Kwa sehemu kubwa  Sera zetu za kibajeti zina athari “either” chanya au hasi kwenye sekta mbalimbali, na kuna wakati Sera zetu zimekwenda kinyume na matarajio ya sekta za uchumi. Wakati ambapo tunataka kukuza uchumi tunajikuta kumbe Sera tulizozitengeneza zinakwenda “against”. Alisema Bw. Mafuru.

Aidha Bw. Mafuru alisema kuwa dhumuni la kikao kazi hichi ni kutaka kujifunza na kuzijua Sekta binafsi zinapitia changamoto gani. Fursa hii inatoa wigo wa kujadiliana ili Serikali iweze kuchukua hatua stahiki na kufikia lengo lililokusudiwa. Pia kwa kuzingatia Dunia imetoka kwenye kipindi ambacho  uchumi wa Tanzania na Nchi nyingine Duniani uliyumba kutokana na  changamoto ya Uviko 19 na vita vinavyoendelea huko Russia na Ukrain. 

Bw. Mafuru aliongeza kuwa Sekta nyingi ziliathirika zikiwemo za uzalishaji, Biashara na Sekta ya Utalii ambayo ndio iliathika sana kwa sababu raia wengi wa nchi hizo ndio ambao pia wanapendelea kuja katika nchi zetu hizi kufanya utalii. Hivyo Serikali inapaswa kuelewa mambo yanayotokea nje na ndani ya nchi ili Itengeneza sera zinaendena na uhalisia wa sasa.

 “Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan alishasema zaidi ya mara mbili na ameendelea kusisitiza, tutengeneze mazingira wezeshi yatakayoiwezesha Sekta binafsi kukua na kuleta maendeleo ya uchumi kwa kutengeneza ajira, kuleta mapato kutokana na faida na mambo mengine ambayo yanatokana na maendeleo ya kiuchumi. Lakini maalumu kabisa katika sekta ya Utalii, yeye mwenyewe ametoka na kushiriki kwenye “Royal Tour” japo ana majukumu mengi lakini aliweka muda wake na kuweza kuinvest kwenye hiyo sekta. Ikumbukwe kuwa kwa miaka minne mitano iliyopita ilikuwa inachangia karibia dola bilioni mbili kwenye uchumi wetu sio kiasi kidogo cha fedha kuingia kwenye uchumi” Alisema Bw. Mafuru. 

Kwa upande wa Kamishna  wa Sera Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Elijah Mwandumbya alisema kikao kazi cha leo kimewezesha kujua changamoto mbalimbali ikiwemo changamoto ya ushuru mkubwa katika mageti ya Halmashauri na uchelewashaji wa Mifumo ya Ulipaji kodi au tozo mbalimbali.

“Sisi Wizara ya Fedha na Mipango tutakaa Pamoja na Wizara hii ya kisekta ambayo ndio ina jukumu la kuanzisha hayo mageti ama hizo tozo lakini pia kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii ambao wanasimamia sekta hii ya utalii Pamoja na TAMISEMI tuweze kukaa chini na kuhakikisha kwamba changamoto hizo za mageti mbalimbali zinaondolewa mojawapo ya eneo ambalo sisi tunapaswa kuelekea ni muhimu sana tukatengeneza dirisha moja ambapo wadau wa sekta ya utalii watakuwa wanalipa yale mapato ama tozo, ama kodiwazolipa. Tumefanya hivyo lakini tunapaswa tumalizie vipande vidogo vidogo ambavyo vimebaki ili kusudi wale wadau  wakishalipa eneo moja basi waendelee na shughuli zao za kuwahudumia wale watalii washamirishe biashara zao ziweze kustawi na matokeo mengine chanya ambayo yapo katika eneo hilo. Pia kuhusu mifumo ya ulipaji ni eneo ambalo limeanzishwa miaka ya karibuni ni maboresho ambayo yanafanyika kila siku na sisi tutachukua hatua za makusudi kuhakikisha kwamba changamoto hii inakwisha kabisa iwe ni historia katika utendaji kazi wetu. Ni muhimu sana wafanyabiashara hawa wanapotaka kulipa kodi basi wasipate tatizo lolote la mtandao” Alisemba Bw. Mwandumbya.

Naye Naibu Kamishna wa Hifadhi anayesimamia Kurugenzi ya Uhifadhi Pamoja na Huduma za Biashara ndani ya Shirika ya Hifadhi za Taifa Tanzania – TANAPA Bw. Herman Mbatio alisema anawashukuru Wizara ya Fedha na Mipango kwa kuweza kuandaa kikao kazi hiki kwani yamejadiliwa mambo mhuhimu yenye lengo la kuboresha shughuli za utalii. 

“Changamoto mojawapo iliyojitokeza ni katika miundombinu kwenye maeneo ya hifadhi, lakini sisi kama Shirika la Hifadhi za Taifa ambao tunapokea watalii tumejipanga kuboresha miundombinu ya barabara. Kwa sasa hivi kama Shirika tumenunua mitambo ya Thamani ya shilingi bilioni kama 16.4 kuweza kutengeneza miundombinu katika hizi hifadhi zetu. “Alisema Bw. Mbatio. 

Kwa upande wa Katibu Mtendaji wa Shirikisho la Vyama vya Utalii Tanzania, Bw. Richard Rugimbana alisema ni muhimu kuwa na utaratibu wa majadiliano kama haya ili kujaribu kubadili utaratibu wa ushirikiano kati ya Serikali na wadau wa utalii.

“Leo tulichoitiwa hapa ni kutusikiliza kwamba jamani nyinyi mna changamoto zipi, ni mambo gani ambayo mngependa Serikali iyafikirie ili nayo iweze ikayaendeleza na kuweza kuhakikisha kwamba kweli tunaweza tukaanza ukurasa mpya na ambao utatusaidia katika masuala ya utalii kwani kilichotokea  baada ya utalii kukwama wakati wa Machi 2020. Utalii ulianza kuzama lakini baadae kutokana na juhudi za Serikali za viongozi na pia Mhe. Mama Samia wakabuni mkakati wa kujaribu kuinua utalii na kama mtavyoona kuanzia mwaka huu tangu mwezi wa sita idadi ya utalii imeongezeka haifiki idadi ya utalii ya zamani lakini angalau inafika kwenye idadi ya milioni moja na kadhalika hivi” Alisema Bw. Rugimbana.

Kikao kazi cha maboresho ya Sera na kusikiliza changamoto za wadau wa Utalii kimejumuisha Wizara ya Fedha na Mipango, Mamlaka ya Mapato Tanzania – TRA Pamoja na Wizara ya Maliasili na Utalii iliyojumuisha Taasisi zake za TANAPA na Ngorongoro.


No comments:

Post a Comment