MVUA ZA CHINI YA WASTANI HADI WASTANI ZATARAJIWA MAENEO MENGI YA NCHI, TMA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Wednesday, 26 October 2022

MVUA ZA CHINI YA WASTANI HADI WASTANI ZATARAJIWA MAENEO MENGI YA NCHI, TMA

Mkurugenzi wa Huduma za Utabiri, Dk. Hamza Kabelwa akizungumza.


MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) leo jijini Dar es Salaam imekutana na waandishi wa habari na kutoa mwelekeo wa mvua za Msimu kwa maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka: huku ikitabiri uwepo wa mvua za chini ya wastani hadi wastani zinatarajiwa katika maeneo mengi ya nchi.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Mkurugenzi wa Huduma za Utabiri, Dk. Hamza Kabelwa alisema katika nusu ya kwanza ya msimu yaani Novemba, 2022 hadi Januari, 2023 vipindi virefu vya ukavu vinatarajiwa kujitokeza, hivyo kuzitaka sekta mbalimbali kujipanga na kukabiliana na hali hiyo.

Dk. Kabelwa aliitaja mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi, Singida, Dodoma, Ruvuma, Lindi na Mtwara kuwa itakubwa na hali hiyo na pia mvua za wastani hadi chini ya wastani zinatarajiwa katika baadhi ya maeneo ya mikoa ya Njombe, Rukwa, Songwe, Mbeya, Iringa na kusini mwa mkoa wa Morogoro.

"...Katika nusu ya kwanza ya msimu (Novemba, 2022 – Januari, 2023) vipindi virefu vya ukavu vinatarajiwa kujitokeza. Ongezeko la mvua linatarajiwa katika nusu ya pili ya msimu (Februari- Aprili, 2023). Aidha, mvua za nje ya msimu zinatarajiwa mwezi Mei, 2023 katika maeneo mengi.

Aliongeza kuwa maeneo ya mikoa ya Singida na Dodoma upo uwezekano wa mvua za msimu kuanza kwa kuchelewa katika wiki ya pili ya mwezi Januari, 2023.

Hata hivyo, alibainisha kuwa mwenendo wa mvua za vuli yaani Oktoba hadi Disemba, 2022 katika maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka, mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Mara, Manyara, Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Dar es Salaam, yanatarajiwa kupata mvua za chini ya wastani hadi wastani kama ilivyotabiriwa tangu awali.

Hali hiyo pia itajumuisha maeneo ya kaskazini mwa mkoa wa Morogoro, Pwani pamoja na Kisiwa cha Mafia na Zanzibar katika visiwa vya Unguja na Pemba, huku mvua za nje ya msimu zikitarajiwa pia kuanza katika mwezi Januari, 2023.

"..Mwelekeo wa mvua za Msimu yaani Novemba, 2022 hadi Aprili, 2023 Mvua za Msimu ni mahususi katika maeneo ya magharibi mwa nchi, kanda ya kati, nyanda za juu kusini magharibi, kusini mwa nchi, ukanda wa pwani ya kusini pamoja na maeneo ya kusini mwa mkoa wa Morogoro. Maeneo haya yanapata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka, unaoanza mwezi Novemba na kuisha kati ya mwezi Aprili na Mei ya mwaka unaofuata," alisema Mkurugenzi huyo wa Huduma za Utabiri, Dk. Kabelwa.

Pamoja na hayo TMA imetabiri upungufu mkubwa wa unyevunyevu katika udongo unatarajiwa kujitokeza Novemba na Disemba, 2022, katika maeneo mengi yanayopata mvua za Msimu jambo ambalo litaathiri ukuaji wa mazao na upatikanaji wa malisho kwa ajili ya mifugo.

"Kina cha maji katika mito na mabwawa kinatarajiwa kupungua na kuathiri upatikanaji wa maji kwa matumizi mbalimbali kama vile umwagiliaji na uzalishaji wa nishati. Mamlaka zinashauriwa kuhakikisha vyanzo vya maji vinatunzwa pamoja na kuweka miundombinu ya uvunaji maji sambamba na kuandaa na kutekeleza mipango mkakati ya kuhimiza kilimo himilivu. Alisema.

Aliongeza kuwa Mamlaka ya Hali ya Hewa itaendelea kufuatilia mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na kutoa mirejesho ya mwelekeo wa mvua nchini kadri inavyohitajika na kuwashauri wadau kuwasiliana na Mamlaka ili kupata taarifa mahsusi za utabiri wa msimu ili kukidhi mahitaji maalum katika sekta zao.

No comments:

Post a Comment