MKOA WA TABORA NA KIGOMA KUUNGANISHWA KWA BARABARA ZA LAMI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Thursday, 20 October 2022

MKOA WA TABORA NA KIGOMA KUUNGANISHWA KWA BARABARA ZA LAMI

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa (kulia) akimsikiliza Mhandisi Mshauri wa Kampuni ya Norplan Mhandisi Henry Ngogoro (kushoto), hatua za ujenzi wa  barabara ya Malagarasi – Ilunde - Uvinza (km 51.1), inayojengwa kwa kiwango cha lami, Mkoani Kigoma. Katikati ni Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Kigoma, Mhandisi Ngoko Mirumbe.

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa akiangalia uharibifu wa miundombinu wa taa za barabarani katika Wilaya ya Urambo Mkoani Tabora. Kulia ni Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Tabora, Mhandisi Raphael Mlimaji.

SERIKALI imewaahidi wakazi wa Mkoa wa Tabora na Kigoma kuunganisha mikoa hiyo kwa barabara za lami ifikapo mwakani 2023.

Akizungumza kwa nyakati tofauti mkoani Kigoma na Tabora wakati alipokagua miradi iliyobakia kuunganishwa mikoa hiyo Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa, amesema ujenzi wa barabara ya Malagarasi - Ilunde - Uvinza (km 51.1) na Kazilambwa - Chagu (km 36) kwa kiwango cha lami ni azma ya Serikali ya kuunganisha barabara zote za Mikoa na kuchochea shughuli za kibiashara  katika mikoa hiyo na mikoa jirani pamoja na nchi jirani za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Burundi. 

 

“Serikali inayoongozwa na Mama Samia inaendeleza Sera ya Ujenzi kwa kuhakikisha mikoa na wilaya zinaunganishwa kwa njia ya barabara bora sambamba na miradi mingine ya uchukuzi ikiimarishwa ili kumpa uhuru mwananchi achague usafiri atakaouweza", amefafanua Waziri Prof. Mbarawa.

 

Waziri Mbarawa amesema Serikali haitaongeza muda wa ziada kwa miradi hiyo miwili na hivyo kumtaka Mkandarasi Kampuni ya STECOL Cooperation anayejenga barabara hizo kukamilisha kwa wakati na viwango.

 

“Serikali haitaongeza muda wa ziada kwa miradi hii tunataka miradi hii iwe imekamilika na wananchi wafaidi matunda ya kodi wanazolipa sababu fedha tayari mmeshalipwa hivyo hakuna sababu nyingine za kuchelewesha kukamilika kwake", amesisitiza Waziri Prof. Mbarawa.

 

Vilevile Waziri Prof. Mbarawa amekagua uharibifu uliofanywa kwenye miundombinu ya taa za barabara katika Wilaya ya Urambo na kuomba uongozi wa Mkoa wa Tabora kuchukua hatua stahiki kwa wananchi walioharibu miundombinu hiyo kwa kung'oa taa saba na kuisababisha Serikali hasara ya takriban Shilingi Milioni 21.

 

Aidha, Waziri Prof. Mbarawa ametoa wito kwa wananchi kutofanya shughuli zozote karibu na alama za mipaka ya barabara zilizowekwa kwani kufanya hivyo ni kosa kisheria na hatua kali zitachukuliwa.

 

Kwa upande wake Meneja wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS), Mkoa wa Kigoma, Mhandisi Ngoko Mirumbe, amesema Wakala utahakikisha mkandarasi anaongeza kasi ya ujenzi ili kutochelewesha kukamilika kwa mradi huo kwani unatakiwa kukamilika Oktoba mwakani.

 

Naye Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), mkoa wa Tabora Mhandisi Raphael Mlimaji, amemuhakikishia Waziri Mbarawa kuwa TANROADS itamsimamia Mkandarasi anayejenga barabara ya Kazilambwa hadi Chagu ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati na viwango walivyokubaliana katika mkataba.

 

Ujenzi wa barabara ya Malagarasi-Ilunde hadi Uvinza wenye kilomita 51.1 unaojengwa kwa kiwango cha lami umefikia asilimia 17 na ujenzi wa barabara ya Kazilambwa hadi Chagu yenye urefu wa kilomita 36 unaojengwa kwa kiwango cha lami umefikia asilimia 65.

 

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.


No comments:

Post a Comment