Na Dotto Mwaibale, Singida
MKUU wa Mkoa wa Singida, Dk.Binilith Mahenge, amewaagiza Wakurugenzi wa
Halmashauri za Wilaya na watendaji katika wilaya zote za mkoa huu kufanya ziara
kusikiliza kero za wananchi na kuzipatia ufumbuzi badala ya kusubiri viongozi
wa serikali ya mkoa ndio wazitatue changamoto za wananchi.
Ametoa agizo hilo wakati wa kikao maalum cha kufanya majumuisho ya ziara
yake aliyoifanya hivi karibuni katika wilaya zote za mkoa huu kwa ajili ya
kusikiliza kero mbalimbali za wananchi.
Dk.Mahenge alisema serikali inatoa fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa
miradi mbalimbali ya maendeleo lakini wananchi hawajui kinachoendelea kwasababu
viongozi ambao wanapaswa kuwaeleza hawafanyi hivyo.
"Ni muhimu mno kufanya mikutano ya wananchi kusikiliza kero zao,
wahamasisheni madiwani, makatibu tarafa wafanye ziara, mkoa wetu mwaka wa fedha
uliopita tulipata Sh.230 bilioni ni wajibu wetu kama viongozi kuzisimamia ili
zilete tija katika maendeleo," alisema.
Dk.Mahenge alisema wakuu wa wilaya wanajitahidi sana kufanya ziara na
kusikiliza kero za wananchi lakini changamoto ipo kwa watendaji wengine wa
serikali ambao hawafanyi hivyo na hivyo kusababisha kuibuka kwa kero nyingi
ambazo kama ziara zingekuwa zinafanyika hali hiyo isingejitokeza.
Aliongeza kuwa katika baadhi ya maeneo wananchi wamekuwa wakilalamika
kutoshirikishwa kwenye mipango mbalimbali ya maendeleo hususani baadhi ya
wenyeviti wa serikali za vijiji ambao ndio wamekuwa na tabia hiyo.
"Baadhi ya wenyeviti wa vijiji wamekuwa kama miungu watu hawatowi
fursa ya kusikiliza wananchi, RAS (Katibu Tawala Mkoa) tufanye uchunguzi na
tuchukue hatua kwa kuzingatia sheria na taratibu za serikali," alisema
Dk.Mahenge.
Aidha, Dk.Mahenge aliagiza wakuu wa wilaya kwa kushirikiana na wataalam wa
ardhi kufuatilia migogoro yote ya ardhi na kuipatia ufumbuzi na kuiweka kwenye
'data base'.
Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dorothy Mwaluko amemuhakikishia Mkuu wa Mkoa huo kuwa yote aliyoyaagiza atayafanyia kazi kwa kushirikiana na Watendaji wa Halmashauri za Mkoa.
No comments:
Post a Comment