Wajumbe mbalimbali wa Baraza la Wafanyakazi la TEA
wakifuatilia taarifa kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Taasisi hiyo wakati wa
kikao cha Baraza hilo Jijini Dar es Salaam
0Wajumbe mbalimbali wa Baraza la Wafanyakazi la TEA
wakifuatilia taarifa kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Taasisi hiyo wakati wa
kikao cha Baraza hilo Jijini Dar es Salaam.
Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi la TEA wakiwa katika picha ya pamoja walipokutana katika kikao cha Baraza hilo Jijini Dar es Salaam.
Na Eliafile Solla -TEA
MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) na Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi la TEA Bi. Bahati Geuzye ameupongeza uongozi wa Baraza la Wafanyakazi la TEA kwa jinsi wanavyofanya kazi na kusimamia sheria jambo ambalo linawapa wajumbe wa baraza hilo nafasi ya kujadiliana kwa kina kuhusu mipango na utekelezaji wa shughuli za Taasisi.
Alizungumza haya katika kikao cha siku moja cha Baraza hilo, ambacho kilifanyika leo Jijini Dar es salaam na kuhudhuriwa na wajumbe mbalimbali wanaounda baraza hilo, wageni waalikwa ambao siyo wanachama na mwakilishi kutoka Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu (THTU) makao makuu.
Mwenyekiti huyo wa Baraza na Mkurugenzi Mkuu wa TEA alisema, tangu kuundwa kwa Baraza hilo wamekuwa na vikao sita, ambapo kila mwaka wamekuwa wakiendesha vikao viwili ambavyo vimefanyika katika mikoa ya Morogoro, Arusha, Pwani, Tanga na Dar es Salaam ambako wamekutana leo.
Mwenyekiti huyo aliongeza kuwa, katika miaka mitatu ya uhai wa Baraza hilo, limefanikiwa kufanya kazi zake kikamilifu na kwa weledi wa hali ya juu kwa kuhakikisha vikao vyote vya kisheria vinafanyika kwa lengo la kuhakikisha ushirikishwaji wa wafanyakazi katika maamuzi ya msingi ya Taasisi.
Alibainisha kuwa, Baraza hilo limekuwa linatekeleza majukumu yake kwa ufasaha ambapo, kama sehemu ya majukumu yake ya msingi, limekuwa likishirikishwa katika uandaaji wa maoteo ya bajeti ya TEA kila mwaka na limekuwa likipata taarifa za utekelezaji wa bajeti hiyo, kuangalia mafanikio, changamoto na kisha kutoa mapendekezo ya kuboresha.
Aidha, alisema Baraza hilo linakamilisha muda wake wa utumishi hii leo baada viongozi wake kumaliza kipindi cha utumishi wao ambacho ni miaka mitatu na hivyo Baraza jipya litaundwa kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu.
No comments:
Post a Comment