WAZIRI NAPE ATOA MAELEKEZO KWA TCRA, MAKAMPUNI YA SIMU - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Wednesday 1 June 2022

WAZIRI NAPE ATOA MAELEKEZO KWA TCRA, MAKAMPUNI YA SIMU

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye (kulia), akizungumza wakati wa kikao cha kukabidhiwa ripoti ya tathimini ya hali ya mawasiliano pamoja na hatua mbalimbali zilizochukuliwa na Kampuni ya Simu ya Vodacom kufuatia malalamiko ya watumiaji wa huduma za mawasiliano alipokutana na viongozi wa mtandao huo leo Juni 1, jijini Dodoma. (Picha na WHMTH).

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Simu ya Vodacom, Sitholizwe Mdlalose akifafanua jambo wakati wa kikao cha kukabidhi ripoti ya tathimini ya hali ya mawasiliano pamoja na hatua zilizochukuliwa na Kampuni hiyo kufuatia malalamiko mbalimbali ya watumiaji wa huduma za mawasiliano kilichofanyika leo Juni 1, jijini Dodoma. Kikao hicho kilihudhuriwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye. (Picha na WHMTH).


Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uhusiano wa Vodacom, Rosalynn Mworia akifafanua jambo wakati wa kikao cha kukabidhi ripoti ya tathimini ya hali ya mawasiliano pamoja na hatua zilizochukuliwa na Kampuni hiyo kufuatia malalamiko mbalimbali ya watumiaji wa huduma za mawasiliano kilichofanyika leo Juni 1, jijini Dodoma. Kikao hicho kilihudhuriwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye. (Picha na WHMTH).

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye (kulia), akizungumza jambo na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Simu ya Vodacom, Sitholizwe Mdlalose (katikati) pamoja na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uhusiano wa Vodacom, Rosalynn Mworia mara baada ya kikao cha kukabidhiwa ripoti ya tathmini ya hali ya mawasiliano pamoja na hatua mbalimbali zilizochukuliwa kufuatia malalamiko ya watumiaji wa huduma za mtandao huo nchini leo Juni 1, jijini Dodoma. (Picha na WHMTH).

Na Mwandishi Wetu, DODOMA

WAZIRI wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye ametoa maelekezo kwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na makampuni ya simu kutatua kero na malalamiko ya wananchi kuhusu huduma za mawasiliano pamoja na kuangalia namna ya kuwawezesha watanzania kuongeza matumizi ya simu janja


Maelekezo hayo ameyatoa Juni Mosi, jijini Dodoma wakati akipokea taarifa ya tathmini ya hali ya mawasiliano pamoja na hatua mbalimbali zilizochukuliwa kufuatia malalamiko ya watumiaji wa huduma za kampuni ya  simu ya Vodacom Tanzania 


“Kumekuwa na kero kwa wananchi kuingizwa kwenye huduma ambazo hawakuziomba, TCRA na makampuni ya simu kaeni mtafute utatuzi walikomeshe hili mara moja “, amesema Waziri Nape


Ameongeza kuwa, “Kila mtoa huduma ya mawasiliano aende kwa wateja wake pamoja na wadau wanaowasaidia kutoa huduma kwa wananchi ili wasikilize malalamiko na kuyatatua ,haiwezekani Serikali pekee ndio iwe inasikiliza na nyie makampuni y7a simu ina wajibu wa kufanya hivyo”.


Waziri Nape ameilekeza TCRA na makampuni ya simu kukaa na kutatua malalamiko ya matumizi ya bando ambayo mtumiaji hajui limetumikaje ambapo ameelekeza makampuni ya simu kuboresha program tumizi (mobile application) ili iwe rahisi kuisoma na itoe taarifa nyingi zaidi ili kupunguza malalamiko ya watu kutojua wametumiaje data zao.


Katika hatua nyingine, Waziri huyo ameitaka TCRA na makampuni ya simu kuona namna ya kumsaidia kila mtanzania kumiliki na kutumia simu janja kwa kuangalia namna ya upatikanaji wa simu janja kwa bei nafuu na ikiwezekana ufanyike utaratibu wa mwananchi kununua simu kwa mfumo wa kulipia kwa awamu ndani ya mwaka mmoja au miwili ili kuongeza matumizi ya intaneti nchini.


“Ikumbukwe kuwa Serikali iliondoa kodi kwenye simu janja lakini takwimu zinaonesha matumizi ya simu janja yameongezeka kwa asilimia mbili tu, kwa kuwezesha wananchi kutumia simu janja itaongeza watumiaji wa huduma ya intaneti, makampuni mtapata fedha Serikali itaongeza mapato na mwananchi atapata huduma anayostahili,” amezungumza Waziri huyo.


Aidha, Waziri Nape ameipongeza Kampuni ya Vodacom Tanzania kwa kuwa wa kwanza kwenda kufanyia kazi malalamiko ya wananchi na kuyashauri makampuni mengine kutekeleza hilo huku akiwashukuru wote waliowekeza katika sekta ya mawasiliano na kuwahakikishia kuwa Serikali inaendelea kushirikiana na sekta binafsi ili kumhudumia mtanzania.


Awali, Mkurugenzi Mkuu wa Vodacom Tanzania, Sitholizwe Mdlalose Vodacom Tanzania ilifanya kazi kwa ushirikiano na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) na kujenga minara ya mawasiliano 23 ili kupanua wigo wa mtandao wa simu kufikia asilimia 93 ya watu watanzania wanaopata huduma ya mawasiliano ya simu ikiwa pia ni sehemu ya kampeni ya kampuni hiyo ya kuiunganisha Afrika ambayo inatambua fursa za zinazotolewa na maunganisho ya kidijitali katika bara la Afrika.


Ameongeza kuwa Kampuni hiyo ya simu ilifanya ukaguzi wa kina kwenye huduma zao zote za kidijitali zinazotolewa na mawakala wasimamizi, na kugundua baadhi ya changamoto ambazo zishughulikiwa na tayari simu za malalamiko kutoka kwa wateja zimepungua kwa asilimia 30.


Imeandaliwa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.


No comments:

Post a Comment