Watano kutoka kulia ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dk Seif Shekalaghe katika picha ya pamoja na wabunifu na washiriki washa ya wabunifu iliyofanyika mwishoni mwa wiki.
Na Dunstan Mhilu
WABUNIFU wa vifaa tiba nchini kwa niaba ya wabunifu mbalimbali wanaingukia serikali kuwasaidia katika mahitaji yao ya msingi pindi wanapohitaji msaada kutoka serikalini na mamlaka zeke.
Ombwe hilo limeibuliwa na wabunifu wa vifaa tiba katika washa ya siku moja iliyoandaliwa na Kiota cha Ubunifu cha Ifakara iliyofanyika Juni 10, 2022 katika ukumbi wa mikutano wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH).
Washa hiyo ilikuwa na lengo la kupatia ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili wabunifu wa vifaa tiba nchini ambapo ukiritimba umeonekana kuwa kikwazo kwa wabunifu kusonga mbele.
Daktari wa Binadamu Emanuel Mushi kutoka kituo cha afya cha Mererani Wilayani Simanjiro anasema aligundua kifaa cha kuongeza joto kwa Watoto njiti na mama wajawazito mwaka 2019 lakini hadi leo hajapatiwa leseni ya kuweza kuzalisha vifaa vingi zaidi ilhali wafadhili wapo wakutosha.
“Tokea 2019 nigundue kifaa hicho nimesotea Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) nikihemea leseni, hadi leo hakuna jibu napigwa kalenda tu, labda kwakuwa leo wahusika wa TMDA wapo na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dk. Seif Shekalaghe yupo, huenda suala langu litapatiwa ufumbuzi maana nina wahisani nchi za Scandinavia lakini wanashindwa kunifadhili kwakuwa sina leseni na Watoto wachanga wanazidi kupotteza maisha kidogo sasa Napata ahueni baada yak iota cha ubunifu cha Ifakara kuonesha nia ya kunisaidia,” alisema Dk. Mushi.
Akijibu Malalamiko ya Dk. Mushi, Meneja sehemu ya usajili wa vifaa tiba na vitendanishi (TMDA), Rehema Mariki alisema, wabunifu wachanga hawana uelewa wa kutosha kuhusu wapi waanzie.
![]() |
| Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Kiota cha Ubunifu cha Ifakara akihutubia washiri wa washa ya siku moja yakuwajengea uwezo wabunifu wachanga. |
“kazi yetu ni kuwaelemisha na kuwataka kufika ofisi zetu za Kanda na Makao makuu ili kupata muongozo hatimaye watengeneze vifaa tiba vyenye ubora na ufanisi, wasikate tamaa wanapokosolewa,” alisema Rehema.
Rehema alisema kuwa yawezekana wabunifu kama Dk. Mushi walikutana na masahihisho ikawa hawajarudi tena hivyo wasikate tamaa kwani kukosolewa ndiyo huleta tija katika kazi mbalimbali na zenye ubora.
Suala la mtaji nalo ni changamoto kwa wabunifu, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dk. Seif Shekalaghe anafafanua.
Dk. Shekalaghe aliwataka wabunifu hao kufuata utaratibu na kuzingatia ubora katika kazi zao.
“Nimesikiliza hoja nyingi ikiwemo ucheleweshwaji wa leseni kwa wabunifu, wagunduzi na wafumbuzi wa vifaa tiba, kama nikweli kwanza niwape pole, pia niwaombe wakati mwingine waanzie Costech ambapo wataelekezwa wapi waende kutokana na ubunifu walionao, Costech itawapa muongozo kama waende TMDA) au Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kuanzia Costech kunaondoa mkanganyiko na usumbufu,” alisema Dk. Shekalaghe.
Kuhusu rasilimali fedha kwa wabunifu Dk. Shekalaghe alisema pesa haijawahi kuwa tatizo isipokuwa wazo la kibunifu ndiyo tatizo.
“Kupitia Wizara ya Afya milango ipo wazi muda wote, njoni tutashauriana na panapohitajika msaada wa kifedha tutatoa, wewe njoo na wazo lako lakutaka kuokoa Maisha ya watanzania na lenye tija kwa Taifa halafu uone kama Rais wetu mpendwa Samia Suluhu Hassan hatatoa fedha, ndugu zangu fedha siyo tatizo,” alisema Dk. Shekalaghe.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, Dk. Amos Nungu, anaiambia HabariLeo kwamba ubunifu umesaidia kutekelezwa mpango wa maendeleo kitaifa, hata kusaidia vijana wengi kujiajiri.
“Hivyo tunathamini na kujali wabunifu kwa wale waliofanikiwa wanafahamu mchango wetu kwao kwa wachanga waje waanzie hapa tutawaunganisha na mamlaka wanazopaswa kwenda kutokana na aina ya ubunifu walionao,” anasema Dk. Nungu.
Anasema, wizara inayohusika na ufundi, sasa inaandaa mijadala kwa kuwashirikisha wabunifu na wadau wa biashara wakiwemo wa sekta binafsi, wanakusanya mawazo yatakayosaidia kuandaa sera kuwalinda katika kuendeleza ubunifu na biashara zao.
Anaeleza kuwa, waliandaa wiki ya ubunifu kwa mikoa 15, ikiwemo Dar es Salaam na imeshafanyika kwa kuendesha mijadala, midahalo na maonesho ya ubunifu, mbalimbali kuwatangaza wabunifu.
“Wizara ya Elimu na Teknolojia imeamua tuwe na wiki ya ubunifu, kikubwa ni kwamba ubunifu tunaouongelea uweze kuwa ni ajenda ya kudumu na tunachokifurahia ni kupata mrejesho kutoka kwa wadau hili kwetu hutupa faraja zaidi,” anasema Nungu.
Anafafanua kwamba, serikali jukumu lake kuu ni kuweka mazingira wezeshi, ikiwemo sera, miongozo na miundombinu sambamba na kuandaa maonesho, pia ikipokea maoni na kuyafanyia kazi.
Dk. Nungu anasema, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, ameshauri Wiki ya Ubunifu ifanyike kwa wilaya na mikoa yote na ndiyo maana mwaka, huu wameanza na mikoa 15, kwa matarajio mwakani watafanya nchi nzima.
Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Ubunifu cha Ifakara, Masoud Mnonji alisema lengo la kuanzishwa kwa kiota cha Ifakara ni kuiunga mkono serikali katika jitihada za kuwapatia vijana ajira.
“Tunawasaidia wabunifu wa aina mbili, wa vifaa tiba na upande wa lishe, kilimo na Maisha bora kwakuwapatia fedha za kufanikisha ndoto zao na mafunzo ili wafanye kazi kwa ubora na ufanisi,” alisema Mnonji.
Mnonji anasema kuwa wamewafikia wafumbuzi na wajasiriamali wengi tu katika mikoa ya Pwani, Arusha, Mbeya, Mwanza na Dar es Salaam.
“Naweza chelea kusema kuwa ni katribani nchi nzima maana wengine tunawatembelea katika vyuo mbalimbali ikiwemo Chuo Kikuu cha Nelson Mandela, Chuo cha Ufundi Arusha, Chuo cha Sayansi na Teknolojia Mbeya, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na hospitali mbalimbali nchini.
Hata hivyo Mnonji amewataka wabinifu kutimia fedha za ufadhili kuendeleza mawazo ya kibunifu kuliko kuzielekeza kwenye biashara nyingine.
Kiota hicho kipo chini ya Taasisi ya Afya ya Ifakara kinafadhiliwa pia na Ubalozi wa Uswizi nchini na na Chuo cha Ufundi cha Botner kilichopo Uswizi.
Ofisa Miradi Kitaifa wa Ubalozi wa Uswizi nchini Tanzania Esta Majani anasema aliliambia HabariLeo kuwa takribani miaka mitatu na nusu sasa wanakiunga mkono kiota hicho kwakifadhili kuweza kutimiza ndoto za wabunifu kwakuwa bado kipo chini ya ulezi wa Taasisi ya Afya ya Ifakara kwa asilimia mia moja.
“Hadi sasa tuna miradi ya maendeleo yenye thamani ya Sh 20 Bilioni nchini ikiwemo inayotekelezwa na Kiota cha ubunifu cha Ifakara na tutaendelea kukilea kituo hiki ili kitimize ndoto za watanzania vijana na serikali katika kupiga vita umasikini,”alisema Esta.
Hadi sasa serikali imeshatoa kipaumbele kwa wabunifu, waanzilishi na wamiliki wa biashara, kuweka mikakati, ikiwamo kutunga sera itakayosaidia na kuwalinda, waweze kuendesha shughuli zao bila matatizo.


No comments:
Post a Comment