SEMINA YA KUMUINUA MWANAMKE KISAIKOLOJIA...! - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Wednesday, 18 May 2022

SEMINA YA KUMUINUA MWANAMKE KISAIKOLOJIA...!

Mtaalamu wa Saikolojia Dk. Nkwabi Sabasaba kutoka jijini Dar es Salaam akiendesha Semina ya Kuwainua Wanawake Kisaikolojia iliyofanyika mwishoni mwa wiki Kata ya Kizaga wilayani Iramba mkoani Singida.

 Afisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Iramba, Jane Ng'ondi akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya hiyo.

Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) wa Chama Cha Mapinduzi wa wilaya hiyo, Rudia Kidaila akizungumza kwenye semina hiyo.
Katibu wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Iramba, Iddy Mohamed Kijamba, akizungumza na wanawake hao kwenye semina hiyo.

Mratibu wa shirika hilo Winjuka Mkumbo ambaye pia ni Diwani wa Viti Maalumu wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, akizungumza kwenye semina hiyo.

Wimbo wa Taifa ukiimbwa.

Zawadi ikitolewa kwa mgeni rasmi.

Semina ikiendelea.

Taswira ya semina hiyo.

Picha ya pamoja. 

Na Dotto Mwaibale, Iramba

SEMINA ya Kumuinua Kisaikolojia  Mwanamke iliyotolewa kwa wanawake wa Wilaya ya Iramba mkoani Singida iliyoandaliwa na Shirika lisilo la kiserikali la Ndugu la Kata ya Kizaga imetajwa kuwa inakwenda kuponya ndoa zilizokuwa zimeteteleka wilayani humo.

Hayo yalibainika mwishoni mwa wiki wakati wa semina hiyo iliyokuwa mahususi kwa wanawake iliyoendeshwa na Mtaalamu wa Saikolojia Dk. Nkwabi Sabasaba kutoka jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari Dk.Sabasaba alisema semina hiyo ya kuwawezesha wanawake kisaikolojia itawawezesha wanawake kusimama wao kama wanawake na kujiamini kwani maisha yao ni tofauti kabisa na wanaume hivyo semina hiyo itawawezesha kuwa na uwezo wa kujijengea uwezo wa kujiamini na uwezo wakusimama wenyewe na pia kujitambua.

"Semina hii ni muhimu sana  kwa wanawake kwani itawasaidia kuwa walezi bora katika jamii kwani kunahusemi unaosema kwamba ukimwezesha mwanamke unakuwa umeiwezesha jamii" alisema Sabasaba.

Sabasaba aliongeza kuwa semina hiyo itawasaidia wao na kuwapa nguvu ya kulea watoto na namna ya kuishi na familia kwani wanawake wengi wamekuwa wakipatwa na mihemuko wakilalamika wameachwa na wanaume wao wamebadilika ghafla hivyo katika kipindi hicho ambacho wameachwa wataishije hivyo hapo ndipo wanapohitaji msaada wa mwanasaikolojia.

Alisema lengo kubwa ya semina hiyo ni kumuondoa mwanamke kutoka katika mazingira ya mfumo dume kwa kumjengea uwezo wa kisaikolojia na kuweza kujikomboa kiuchumi na kuondoka katika utegemezi.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya hiyo Afisa Maendeleo ya Jamii, Jane Ng'ondi aliwataka wanawake hao kila wanapoamka wawe na mpango kazi ili shughuli zao ziweze kwenda vizuri.

"Mwanamke ndio injini ya nyumba hivyo hauwezi kufanya chochote katika nyumba yako pasipo kuwa na mpango kazi wenzako watakuwa wanaenda kwenye shughuli za kiuchumi wewe utakuwa unakwenda kwao kuangalia wanafanya nini" alisema Ng'ondi.

Katibu wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Iramba, Iddy Mohamed Kijamba alisema semina hiyo ni ya muhimu sana kwa wakina mama hao na kueleza wanawake ni jeshi kubwa hivyo aliwaomba waendelee kushirikiana kwa ajili ya kuijenga nchi.

Aliwataka wanawake hao kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali kwenye uchaguzi wa ndani wa chama hicho kwani wao wana nguvu na ushawishi mkubwa katika jamii na hata vitabu vya dini vimeeleza hivyo na akawataka kumuunga mkono mwanamke mwenzao Rais Samia  Suluhu Hassan.

Mratibu wa shirika hilo Winjuka Mkumbo ambaye pia ni Diwani wa Viti Maalumu wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba alisema amefarijika sana kwa kuweza kuwaalika wanawake wa wilaya hiyo wapatao 90 kushiriki semina hiyo ya kuwajengea uwezo wa kujiamini na kuwa wabunifu wa kubuni miradi mbalimbali itakayowainua kiuchumi.

"Kupitia mafunzo waliyoyapata naamini na wao watakwendakuwaelimisha wenzao na si wa wilaya hii pekee bali mkoa mzima wa Singida na kuwa mazunzo haya ni endelevu kila nitakapopata nafasi nitawapatia" alisema Mkumbo.

Alisema mwanamke akielimika anaweza kama ilivyo sasa tunaye Rais Samia Suluhu Hassan ambaye ni mwanamke na anaongoza nchi vizuri hivyo wanaamini mwanamke akipewa nafasi anaweza ambapo alitoa wito wa kuendelea kuwaelimisha na kufanya hivyo watakuwa wameielimisha jamii yote kwa ujumla.

Mshiriki wa semina hiyo Heri ni pendo Masanja kutoka Kijiji  cha Ulemo alisema semina hiyo imewasaidia kujitambua na sasa wataweza kusaidia familia zao na kuepuka migogoro mbalimbali hasa ya ndoa kwani wanawake wengi walikuwa wakikosa mbinu ya kuitatua hivyo kupitia semina hiyo wataweza kuitatua na kuwaepushia matatizo ya kifamilia.

No comments:

Post a Comment