Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaendelea kutanua wigo wa kujitangaza ndani na nje ya nchi ili kuendelea kufungua fursa mbalimbali za uchumi kupitia sekta ya utalii na Sekta nyingine za uchumi ambapo televisheni ya Safari Chaneli imeonekana kuwa ni nyenzo muhimu sana kwa ajili ya kutangaza utalii na kuitangaza nchi na fursa mbalimbali zinazopatikana nchini
Akizungumza katika kikao cha Makatibu Wakuu na Wakuu wa Taasisi kuhusu uendeshaji wa Chaneli ya Safari kilichofanyika jijini Dodoma, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Jim Yonazi ametoa wito kwa sekta za umma kutumia channeli hiyo kutangaza fursa mbalimbali zinazopatikana nchini
“Nitoe wito kwa Sekta za Umma nchini kutumia Safari Chaneli kutangaza sekta zao kwa mtazamo wa utalii tukiwa wabunifu kila sekta ya uchumi inaweza kuwa sehemu ya utalii,
kuna fursa katika usafirishaji, mawaAsiliano, kilimo ambapo watu wanaweza kujifunza nchini kwetu kupitia hii chaneli hii ya utalii”, amezungumza Dkt. Yonazi
Naye Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. John Jingu amesema kuwa Serikali na wadau kutoka sekta binafsi wanalo jukumu la kuhakikisha wanawekeza kwa kiasi kikubwa katika Chaneli hiyo ya Safari ili malengo ya kukuza utalii kupitia channel hiyo na watu wengi ndani na nje ya nchi waweze kufahamu vivutio vilivyopo nchini yaweze kufanikiwa
“Tunahitaji kuongeza jitihada za uwekezaji wa rasilimali katika chaneli hii ya Safari hasa rasilimali fedha kwa ajili ya uendeshaji, rasilimali hizo zitatolewa na wadau ambao ni taasisi za umma lakini pia sekta binafsi ambao ni wadau wa utalii nao wanapaswa pia kuwekeza kadri watakavyoona manufaa yanayopatikana kupitia chaneli hiyo kuwekeza ili kukuza sekta ya utalii nchini”, amezungumza Dkt. Jingu
Kwa upande wa Bi Fatma Hamad Rajab, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari,Vijana, Utamaduni na Michezo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar amesema kuwa Zanzibar ni kituo kikubwa cha utalii na tayari ipo safari chaneli kupitia ZBC 3, ambapo ameahidi kushirikiana na kufanya kazi kwa pamoja na Tanzania Bara kwa ubunifu mkubwa ili kupitia ZBC 3 milango mingi zaidi ya utalii itafunguka
Kwa upande wa Meneja Uhusiano wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Bi Martha Chassama amesema kuwa TFS imepata mafanikio makubwa sana katika kutangaza maeneo yao ya utalii kupitia Safari Chaneli na imekwishatoa kiasi cha fedha kuchangia uendeshaji wa Chanel hiyo ili kuendelea kujitangaza na kuonekana zaidi ndani na nje ya nchi
Akizungumza katika kikao hiyo Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) dkt. Ayub Rioba amesema kupitia Safari Chaneli watanzania wanazidi kujua na kulinda uhifadhi, inaonesha umuhimu na kuhamasisha utalii wa ndani lakini pia dunia inatambua vivutio vingi vya utalii vinavyopatikana nchini
Imeandaliwa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari
No comments:
Post a Comment