Na Adeladius Makwega
NAIBU Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo, Pauline Gekul Februari 4, 2022 amewasilisha taarifa ya mikakati ya kuongeza viwanja vya michezo nchini na taarifa ya kufanikisha ushiriki wa timu za Tanzania katika mashindano ya kimataifa mbele ya Kamati ya Maendeleo ya Hudumu za Jamii ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kusema kuwa kuwezesha timu za taifa ni jukumu la serikali.
Akiwasilisha taarifa zote mbili kwa kina Naibu Waziri Gekul alifafanua kuwa; “Kulingana na sera ya maendeleo ya michezo ya mwaka 1995, kimsingi jukumu la kuwezesha timu za taifa katika michezo ya kimataifa ni la serikali. Kwa msingi huo kuanzia mwaka 2019/2020 serikali ilianza kutenga bajeti maalumu kwa lengo hilo na kusaidia malezi ya timu za taifa.”
Naibu Waziri Gekul alisisitiza kuwa serikali haitorudi nyuma katika hili itaendelea kutenga bajeti kwa ajili ya usaidizi wa timu za taifa ambazo zitafuzu katika mashindano hayo ya kimataifa kadiri ya bajeti itakavyokuwa ikiruhusu huku akiwaomba wajumbe wa kamati hii kuendelea kushirikiana kwa karibu ili Tanzania iweze kufikia shabaha ya mafanikio ya michezo.
Wakichangia katika kamati hii, mheshimiwa, Neema Lungangila alisema kuwa serikali ihakiishe kuwa wachezaji wetu wanaoshiriki katika michezo hiyo wanakuwa na lishe bora ili kuweza kushiriki vizuri na kulipatia ushindi taifa.
“Siyo mchezaji wetu anapigwa kikumbo kidogo, anapepesuka sana, nashauri serikali itumie wataalamu wa lishe ili wachezaji hawa wawe na afya bora tangu wakiwa wadogo na hii inabebwa na nidhamu ya chakula.”
Wajumbe wengine wa kamati hii walisisitiza juu ya maboresho ya sera ya michezo ya mwaka 1995 kuwa imepitwa na wakati.
Akilijibu hilo Naibu Katibu Mkuu wa wizara hii Said Yakub alisema kuwa unapoisoma sera ya michezo unabaini kuwa ina mambo mengi ya msingi ambayo yanaweza kutuongoza vizuri kufikia shabaha ya mafanikio katika michezo.
“Sasa tunajitahidi kuiwekea mpango mkakati wa utekelezaji wake kwa kushirikiana na wadau wote, ilikufanikisha mafanikio makubwa ya michezo.”
Akiendelea kuwasilisha taarifa hizo Naibu Waziri Gekul aliyataja mambo makubwa ambayo ndiyo mikakati ya seikali kuimarisha ushiriki wa Tanzania katika mashindano ya kimataifa.
“Kuimarisha bajeti ya kawaida ya wizara ya kila mwaka, kubuni vyanzo vipya vya mapato, kubainisha michezo ya kipaumbele, kuendeleza diplomasia ya michezo, kuwa na shule maalumu za michezo na kuanzishwa kwa vituo maalumu vya michezo.”
Akichangia katika kuhitimisha mjadala huo wa kamati hii makamu mwenyekiti wake Mheshimiwa Aloyce John Kimamba alisema kuwa suala la michezo ili kuweza kufanikiwa linahitaji fedha za kutosha ambazo sasa serikali imeanza kuzitenga. Pia alisisitiza kufufuliwa kwa michezo ya jadi ambayo ilikuwa ikichezwa tangu enzi na mababu zetu.
No comments:
Post a Comment