Na Dotto Mwaibale Singida
MKUU wa wilaya ya Ikungi Jerry Muro ametoa onyo kwa mtu yeyote atakayeingia katika wilaya hiyo kwa nia ya kutaka kufanya uhalifu wa kutumia silaha kuwa hataweza kutoka salama kwa kuwa vyombo vya usalama vimejipanga ipasavyo kukabiliana na matukio yote ya kiharifu na kuwa wilala hiyo ipo salama.
DC Muro aliyasema hayo juzi wakati akizungumza katika kilele cha maadhimisho ya miaka 45 ya kuzaliwa chama cha Mapinduzi (CCM) yaliyoazimishwa kiwilaya katika Kata ya Mang'onyi wilayani humo.
" Ndani ya miaka 45 vyombo vya ulinzi na usalama vimedumisha amani na ulinzi kwa kushirikiana na raia wema hatua iliyosababisha wilaya kuendelea kuwa salama na wananchi kuendelea na shughuli za maendeleo pasipo mashaka yoyote" alisema DC Muro.
Alisema mtu awaye yeyote asijaribu kuingia katika wilaya hiyo kwa nia hofu ni lazima atakamatwa na kufikishwa kwenye mkono wa sheria.
Mwenyekiti wa CCM wa wilaya hiyo Mika Likapakapa alisema kuwa nchi yetu hususani Wilaya ya Ikungi imekuwa na mafanikio makubwa ya ujenzi wa barabara na miradi mingi a hiyo yote imetokana na mfumo uliopo nfani ya chama hicho ulioasisiwa na Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Aliutaja mfumo huo kuwa ni wa mafiga matatu akimaanisha Jumuiya ya Wazazi, Vijana na UWT na kuwa alifanya hivyo lengo likiwa kuwasogezea wananchi wapate huduma karibu.
Likapakapa alisema mwaka huu kutakuwa na uchaguzi wa viongozi wa chama ambao kwa ngazi ya mashina utakuwa Aprili 10 hicho hivyo kila mwana chama anaruhusiwa kuchukua fomu na kugombea kwani hakuna mtu ambaye alizaliwa ili awe kiongozi bali wote wanaweza kugombea na kuwa viongozi.
Diwani wa Kata ya Mang'onyi Innocent Makomelo alitumia maadhimisho hayo kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za kujenga miradi mbalimbali katika wilaya hiyo na kuwa kiu kubwa waliyokuwa nayo ni kujengewa madarasa katika Shule Shikizi ya Namba 7.
" Mwaka juzi wananchi wa kata hii waliomba mambo yote wayaache badala yake washughulikie suala la elimu kwanza na mimi niliyapokea kunapo husika na sasa tumepata madarasa" alisema Makomelo.
Makomelo aliomba shule hiyo isajiriwe na kupata walimu kutoka serikalini ili watoto hao wapate elimu iliyotarajiwa.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi Ally Mwanga aliishukuru Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwapelea fedha za kutekeleza miradi mbalimbali.
Alisema mwishoni mwa mwaka uliopita wilaya hiyo ilipokea zaidi ya Sh. Bilioni 2.6 kwa ajili ya miradi mbalimbali ambazo zilienda kutatua miundombinu ya ujenzi wa shule za sekondari, msingi na shikizi ambapo jumla ya madarasa 103 yamekamilishwa.
Katika kilele cha maadhimisho hayo shughuli mbalimbali zilizofanyika ni kukagua miradi ya maendeleo ikiwemo barabara ya kilomita tatu, madarasa manne Shule Shikizi ya Namba 7, ujenzi wa vyoo na madarasa mawili shule ya Msingi Mlumbi, mradi wa maji utakao hudumia wananchi wa vijiji vya Mang'onyi na Mlumbi, ukarabati wa Zahanati ya Kata ya Mang'onyi pamoja na ujezi wa kichomea taka za uzio wake katika zahanati hiyo miradi hiyo yote imetekelezwa na Kampuni ya uchimbaji Madini ya Shanta kwa gharama ya Sh.235,495,327.
Shughuli nyingine iliyofanyika ni kuwapokea wanachama wapya wakiwemo viongozi 11 waliohamia CCM wakitokea upinzani sambamba na kukabidhi kadi zaidi ya 100 kwa wanachama wapya.
No comments:
Post a Comment