KANISA HALISI LA MUNGU BABA KUMUUNGA RAIS KIVITENDO - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Sunday, 2 January 2022

KANISA HALISI LA MUNGU BABA KUMUUNGA RAIS KIVITENDO

Baba halisi akimueleza mgeni Rasmi jinsi ukarabati wa miundombinu ulivyofanyika na namna walivyopa fedha za ukarabati.

Na Dunstan Mhilu

KANISA Halisi la MUNGU BABA lenye Makao yake Makuu Tegeta, jijini Dar es Salaam,limeikabidhi Serikali, madarasa sita (6) na Ofisi mbili (2) za Mwalimu Mkuu ambavyo limeyafanyia ukarabati mkubwa wa miundombinu na kuwa bora kabisa katika Shule ya Msingi Uhuru, katika Manispaa ya Kigoma Ujiji mkoani Kigoma

Akipokea hati ya makabidhiano ya majengo hayo, mgeni rasmi ambaye amuwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Kigoma Ujiji Rose Manumba, alisema mchango wa Kanisa hilo kwa jamii ni wakutukuka na hautasaulika na watazidi kubarikiwa kwa namna wanavyojitoa kwa jamii.

“Binafsi naguswa sana na namna ambavyo Kanisa hili linavyojitoa kwa jamii kwani naskia si mara ya kwanza kufanya jambo kama hili naskia mlifanya huko Tabora na kwingineko Mungu awabariki san ana wengine waige mfano kama huu” alisema

Ukarabati wa miundombinu hiyo umefanyika kutokana na ombi la wakazi wa eneo hilo walililolitoa wakati wa ibada ya hija iliyofanyika mwezi machi mwakajana katika viwanja vya Lake Tanganyika.

Katika kujibu ombi hilo Mkuu wa vituo vyote vya Kanisa hilo Baba Halisi aliketi na kikao tendaji cha Kanisa na ukarabati kuanza Novemba 26,2021 na kukamilika Desemba 14,2021 na hatimaye kukabidhiwa kwa uongozi wa Mkoa wa Kigoma katika Manispaa ya Kigoma Ujiji juzi

Ukarabati na ujenzi wa miundombinu hiyo umegharimu shilingi milioni 18.86(sh18,860,000) na kuifanya shule hiyo kuonekana mpya kabisa ambapo Mkurugenzi huyo aliwataka wanafunzi na walimu kuitunza miundombinu hiyo iweze kudumu.

"Hii siyo mara ya kwanza kwa Kanisa Halisi kusaidia hapa mkoani Kigoma, kama mtakumbuka mwaka 2019 Kanisa hili lilisaidia ujenzi wa shule mpya pale Buzebazeba, na hadi sasa shule ile inaendelea vizuri na imekuwa msaada mkubwa” alisema

Kwa upande wake Mkuu wa vituo vyote vya Kanisa hilo aliushukuru uongozi wa mkoa huo kwakile alichokiita kuwa ukarabati wa shule hiyo ni baraka kwao.

"Sisi Kanisa Halisi la MUNGU BABA, tuna furaha kubwa kwa kupewa nafasi ya kupokea Baraka kupitia kukarabati madarasa ya Shule ya Msingi Uhuru katika Manispaa ya Kigoma-Ujiji. Hivyo, licha ya kukabidhi madarasa yaliyokarabatiwa na Kanisa, lengo kubwa la kuja hapa leo ni kushukuru kwa kuwa kupitia ukarabati wa madarasa haya tumepokea Baraka nyingi kwa mujibu wa Isaya58:7-12. Tunashukuru mno.

Aidha BABA Halisi alisema Kanisa hilo halina mfadhiri wala miradi ya kiuchumi zaidi ya utiifu wa makuhani (waumini) wa Kanisa hilo kwa aliyeumba vyote pale inapotoka Sauti kwa Mungu Baba, basi Mkuu wa Kanisa hilo huwashirikisha makuhani na kutoa mifukoni mwao.

“Kwa kuwa sisi ni kanisa, tunapenda pia kuwashirikisha jinsi gani fedha iliyotumika kukarabati madarasa haya ilivyopatikana. Kila mmoja ndani ya Kanisa licha ya kutoa fungu la kumi la mapato yake kwa aliyeumba kila kitu, pia anatoa asilimia tano (5) ya mapato yake kusaidia Jamii iliyozunguka Kanisa. Kwa kufanya hivyo Kanisa tunapata baraka kwa kuwanyoshea mkono jamii yenye uhitaji",alisema Baba Halisi

Aliongeza kuwa"Popote ambapo tumewahi kutoa msaada, hatujawahi kupokea fedha yoyote kutoka kwenye Mashirika ya Misaada. Tunaliweka wazi jambo hili kwa kuwa mwanzoni kuna waliokuwa wanadhani tunapata misaada kutoka nje. Tunapenda jamii ielewe kuwa huwa hatupokei misaada Nje, bali ni Matunda (sadaka za wale walioko ndani ya Kanisa peke yake)"

Hata hivyo Mkuu huyo wa Kanisa aliwataka wananchi wanapaswa kujua kuwa maendeleo ya Taifa hili yataletwa na wananchi wenyewe na si vinginevyo

"Nikiwa bado katika kipegere hiki, Kanisa tunapenda kuwashirikisha wananchi wenzetu kuwa inawezekana kujiletea maendeleo sisi wenyewe kwa kila mmoja kutoa alicho nacho, kwa Moyo. Kwa mfano licha ya hiyo asilimia tano (5) ambayo kila mmoja anatakiwa kutoa kwa ajili ya jamii, kuna waliotoa sh.100, 200, 500, 1000. Sh. 5000 nakadhalika mpaka ikafika kiasi ambacho tumetumia kukarabati madarasa ya Shule ya Msingi Uhuru. Hivyo, hata katika miradi mingine ya maendeleo, jambo hili linawezekana” alisema Baba Halisi

No comments:

Post a Comment