Mhe. Bashungwa akivishwa medali kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo. Dk, Hassan Abbasi. |
Na John Mapepele, WUSM
WAZIRI wa Utamaduni, Sanaa
na Michezo. Mhe, Innocent Bashungwa ameipongeza Benki ya NBC kwa ushirikiano wao
na Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), wa kuandaa mikakati madhubuti ya
kuhudumia jamii, hususan waathirika wa ugonjwa wa Saratani ya Shingo ya Uzazi na
amewasihi waendelee kushirikiana ili kulinda afya za wananchi na kukuza mchezo
wa riadha nchini, hasa mbio ndefu.
Mhe. Bashungwa ameyasema
hayo leo Novemba 7, 2021 kwenye hotuba
yake akiwa Mgeni Rasmi aliyemwakilisha Mhe. Dkt. Philip
Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika mbio za NBC Dodoma Marathon 2021 kwenye Uwanja
wa Jamhuri jijini Dodoma.
“Dhumuni ya mbio hizi, ni
kuchangia vita dhidi ya ugonjwa wa saratani ya shingo ya uzazi. Ugonjwa huu
ndio unaoongoza kwa vifo vinavyosababishwa na saratani hapa nchini. Tumesikia
kwamba mwaka jana NBC ilichangia jumla ya TZS 100 milioni, fedha zilizotokana
na usajili wa wakimbiaji, na michango ya wafadhili mbalimbali”. Ameongeza Mhe.
Bashungwa.
Aidha, amesema amefurahishwa
na uamuzi Benki hiyo kuingia mkataba wa miaka mitano na RT, wa kuendesha mbio
hizi katika jiji la Dodoma ambapo amesema uamuzi huo utalifanya jiji la Dodoma kuwa na tukio kubwa la mchezo wa riadha, unaovutia
washiriki kutoka nchi mbalimbali barani Afrika.
Pia ameupongeza uongozi wa
benki ya NBC, na Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), kwa kuandaa mbio hizo
ambapo ameeleza kuwa zimeleta hamasa, na mwitikio mkubwa wa wananchi, na wakazi
wa Jiji la Dodoma.
“Wakazi wa jiji la Dodoma
napenda kuwapongeza kwa kushiriki vizuri katika mbio hizi. Hizi mbio
zinatarajiwa kuwa mbio kubwa sana katika siku za usoni, na hivyo ushiriki wenu
kwa wingi, katika mbio hizi ndio nguzo ya mafanikio. Vilevile ushiriki wenu
utachangia vilivyo, katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa saratani ya shingo ya
uzazi. Hii sio kwa Dodoma pekee, bali nchi nzima. Nawasihi wakazi wote hasa
vijana na wakinamama, mjitokeze kwa wingi kuliko leo ili sote tuchangie katika
mapambano haya”. Amefafanua Mhe. Bashungwa
Pia kupitia tukio hilo
amewashukuru wafadhili waliofanikisha kufanyika kwa kwa mbio hizo na amesema kuandaa
tukio kama hilo, kunahitaji ubunifu mkubwa, moyo wa kujitolea, ushirikiano, na
nia njema kwa jamii inayozunguka.
Kwa upande mwingine Mhe.
Bashungwa amesema amefarijika kusikia kwamba Benki imeingia mkataba na Shirikisho
la Mpira wa Miguu (TFF) kudhamini Ligi Kuu ya Tanzania bara, kwa kipindi cha
miaka mitatu kuanzia mwaka huu.
“Ni jambo jema na la kupewa
sifa. NBC pia wanaisaidia Taifa Stars, wamedhamini Samia Cup 2021, na NBC ni
washirika wa Tanzanite Women Sports
Festival. NBC muendelee na sera yenu ya kuwakaribia wananchi kupitia
michezo”. Amepongeza Mhe Bashungwa
No comments:
Post a Comment