MBARAWA AMTAKA MKANDARASI DARAJA LA WAMI KUONGEZA KASI YA UJENZI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Tuesday, 21 September 2021

MBARAWA AMTAKA MKANDARASI DARAJA LA WAMI KUONGEZA KASI YA UJENZI

Msimamizi  wa ujenzi wa Daraja jipya la Wami kutoka kampuni  Power Construction Corporation kutoka China, Mhandisi Cheon Youngcheol, akitoa maelezo kwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa (wa kwanza kushoto), wakati alipokagua maendeleo ya ujenzi wa daraja hilo, mkoani Pwani.

WAZIRI wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, amemtaka mkandarasi Power Construction Cooperation Ltd kutoka China anayejenga Daraja jipya la Wami kuongeza kasi ili kukamilisha ujenzi kabla ya muda walioongezewa kwenye mkataba kumalizika.

 

Moja ya nguzo ya Daraja jipya la wami ambao ujenzi wake umefikia asilimia 61. Ujenzi wa Daraja hilo unatarajiwa kukamilika mwezi Novemba 2022.


Muonekano wa nguzo za Daraja jipya  la Wami ambalo ujenzi wake umefikia asilimia 61 na unatarajia kukamilika mwezi Novemba, 2022.


Prof. Mbarawa aliitoa agizo hilo wakati akikagua maendeleo ya daraja hilo  lenye urefu wa mita 510, upana wa mita 11.85 lililoko mkoani Pwani. Daraja hilo ni kiungo muhimu kutoka Mji wa Chalinze kwenda mikoa ya kaskazini mwa nchi  na nchi za jirani.

 

Akiwa katika ukaguzi huo, profesa Mbarawa alisema ujenzi wa mradi huo kwa sasa umefikia asilimia 61, ulitarajiwa kukamikika Septemba mwaka huu.

 

Alisema  ila kutokana na changamoto mbalimbali zilizojitokeza ikiwemo mvua kubwa zilizonyesha mwaka jana pamoja na ucheleweshaji wa vifaa kuingia nchini kulikosababishwa na mlipuko wa  UVIKO -19, Mkandarasi aliongezewa  muda hadi Novemba, 2022. 

 

"Hakikisheni mnajipanga vizuri pamoja na kuongeza saa za kufanya  kazi hata nyakati za usiku ili kukamilisha ujenzi kabla ya muda ulioongezwa" alisema Prof. Mbarawa.

 

Aidha, Waziri Mbarawa alimhakikishia mkandarasi huyo kuwa Serikali itaendelea kutoa fedha kwa wakati na kumtaka kuhakikisha anaongeza kasi ya ujenzi kwa kuzingatia viwango vilivyoweka ili daraja hilo liweze kudumu.

 

Awali akitoa taarifa ya mradi huo kwa Waziri Mbarawa, Meneja wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) Mhandisi Andrew Kasamwa alisema gharama ya mradi wa ujenzi huo  ni Sh. bilioni 72 ikiwa ni fedha za malipo ya mkandarasi  na mhandisi - mshauri. 

 

Mhandisi Kasamwa alisema kuwa kwa sasa kasi ya ujenzi inaendelea vizuri na tayari nguzo za daraja zimekamilika kwa asilimia 100, ujenzi wa kuta mbili za mwanzo na mwisho wa daraja umekamilika kwa asilimia 85.

 

Alisema ujenzi wa nguzo namba moja na nne zenye urefu wa mita 19.6 umekamilika kwa asilimia 100 na nguzo namba tatu zenye urefu wa mita 44.1 ambayo ndiyo nguzo ndefu zaidi kuliko zote umekamilika kwa asilimia 100.

 

Ujenzi wa Daraja jipya la Wami unajumuisha ujenzi wa barabara za maingilio ya daraja kwa pande zote mbili zenye jumla ya urefu wa kilomita 3.8 zilizogawanywa upande wa kusini wa daraja kilomita 2.1 na upande wa kaskazini kilomita 1.7.


No comments:

Post a Comment