Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mohamed Hassan Moyo akiliagiza Jeshi la polisi pamoja na TAKUKURU kufanya uchunguzi dhidi ya Mwenyekiti wa Kijiji Cha Welu anayedaiwa kujihusisha na vitendo Vya rushwa na kumaliza Kesi za ubakaji Kiholela.
Wananchi wakiwa kwenye mkutano na DC. |
Na Fredy Mgunda, Iringa
MKUU wa Wilaya ya Iringa, Mohamed Hassan Moyo ameagiza Jeshi la Polisi pamoja na TAKUKURU kufanya uchunguzi dhidi ya Mwenyekiti wa Kijiji Cha Welu anayedaiwa kujihusisha na vitendo Vya rushwa na kumaliza Kesi za ubakaji Kiholela.
Akiwa kwenye mkutano wa hadhara mkuu wa wilaya hiyo,waliibuka baadhi ya Wananchi wakimtaja mwenyekiti Ponsian Makapa amekuwa akishughulikia kesi za ubakaji na nyinginezo na kuzimaliza kwa kupokea rushwa jambo ambalo ni kinyume na sheria za nchi.
Moyo alisema kuwa malalamiko ya wananchi kuonewa na kiongozi huyo hayapaswi kufumbiwa macho na hasa tukio na mwanamke mmoja kubakwa na wanaume wa wawili ambalo Kesi yake pia ilimalizwa Kiholela.
Alisema kuwa miongoni mwa Kesi zinazotajwa kumalizwaa kiholela ni pamoja na kesi ubakaji inayowahusisha vijana wawili Mathayo Ngeng`ena na Bidan Mkuvasa wanaodaiwa kushirikiana kumbaka mwanamke mmoja mkazi wa Kijiji hicho Cha Welu kata Ulanda Mkoani Iringa.
Moyo alisema haiwezekani kesi ya ubakaji inamalizika kirahisi hivyo huku ushaidi ukiwepo kwa wanaume hao wawili kumbaka mama moja mwenye watoto watatu anaishi katika kijiji hicho na kesi hiyo ikaisha kirahisi na watuhumiwa kuachiwa huru na kuendelea na kazi zao kama kawaida.
Alisema kuwa utamaduni uliojengeka kwa wahalifu kuendeleza vitendo hivyo wakijivunia Kutofikishwa kwenye vyombo vya Dola ama kutochukuliwa hatua stahiki za kisheria haukubariki hata kidogo.
Kesi za kijamii ikiwemo zinazohusisha migogoro ya wanakijiji na zinatajwa kuwa sehemu ya Mwenyekiti huyu Ponsian Makapa kujipatia fedha isivyo halali na kuendelea kuzusha manung'uniko kwa Wananchi wa kijiji cha Welu.
Awali wakitoa malalamiko kwa mkuu wa wilaya ya Iringa baadhi ya wananchi walisema kuwa kiongozi huyo amekuwa anakikiuka sheria,taratibu,na kanuni za kuongoza kijiji hicho kwa kuendekeza rushwa ambazo zimekuwa zinawaumiza baadhi ya wananchi wa kijiji hicho.
Walisema kuwa kumekuwa na kesi za ubakaji,mimba za utotoni,unyanyasaji wa kijinsia na uongozi usio bora unaopelekea kuvunjika kwa amani katika kijiji hicho ambacho wananchi wake wamekuwa wanakihusisha na kilimo kwa asilimia kubwa.
Wananchi hao walisema kuwa kushamili kwa vitendo hivyo kumesababisha wananchi wengi hasa wanawake na mabinti kuogopa kwenda kuokota kuni porini wakihofia kubakwa kama ambavyo wengine wamekuwa wakifanyiwa na wanaume wa kijiji hicho.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Kijiji Cha Welu Ponsian Makapa alikanusha tuhuma hizo na kusema kuwa sio kweli anazushiwa tu kutokana na tatizo la maswala ya kisiasa hasa walewanaoitaka nafasi yake.
Hata hivyo Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mohamed Moyo akatoa maagizo ya kufanyika uchunguzi dhidi ya madai yote yanayomkabili Kiongozi huyo wa Kijiji.
Kando ya hayo amesisitiza uwajibikaji bora kwa viongozi wa Serikali serikali za mitaa,vijiji,kata na tarafa na kuwataka kuacha mara moja kufanya kazi kwa mazoea la sivyo atawapeleka polisi wao.
Tatizo la ubakaji na mimba za utotoni limeendelea kuwa janga kwa wananchi wa wilaya ya Iringa kutokana na baadhi ya wanaume kuendelea kufanya vitendo hivyo huku vitendo hivyo vimekuwa havichukulikiwi kwa uzito unaostahili na viongozi wa vijiji,kata na tarafa kwa ujumla wakati sheria za vitendo hivyo zipo wazi.
Nao jeshi la polisi wilaya ya
Iringa walisema kuwa wameyapokea maagizo ya mkuu wa wilaya na watayafanyia kazi
kama ambavyo yanatakiwa kufanyiwa kazi kwa mjibu wa sheria.
No comments:
Post a Comment