BARAZA LA KISWAHILI LA TAIFA LAZIDI KUIMARIKA, LAPATA VIFAA VYA KISASA VYA KUFUNDISHIA WAKALIMANI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Monday 6 September 2021

BARAZA LA KISWAHILI LA TAIFA LAZIDI KUIMARIKA, LAPATA VIFAA VYA KISASA VYA KUFUNDISHIA WAKALIMANI

Waziri wa Habari Sanaa Utamaduni na Michezo Innocent Bashungwa, Naibu Waziri wa Habari Sanaa Utamaduni na Michezo Mh. Pauline Gekul wakisikiliza vifaa maalum vya ukalimani vilivyozinduliwa hivi karibuni.

 Na Jovina Bujulu, BAKITA

HIVI karibuni, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Innocent Bashungwa alizindua vifaa vya kisasa vya ukalimani ambavyo vitatumiwa na Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) kufundishia wakalimani wa lugha mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Hii ni hatua kubwa kwa  BAKITA  katika kuhakikisha lugha ya Kiswahili inazidi kukua na kuenea kitaifa na kimataifa, kwani wakalimani watapata ujuzi wa ukalimani na kuwa mabalozi wazuri wa Kiswahili ndani na nje ya Tanzania.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Waziri Bashungwa alisema kuwa wanaohitaji kujua lugha ya Kiswahili wanapaswa kupata rasilimali mbalimbali ikiwemo utaalamu wa ukalimani.

“Kuenea na kukubalika kwa Kiswahili duniani kunadhihirisha na msemo wa ‘Chanda chema huvikwa pete’. Watanzania tuna wajibu mkubwa wa kuwasaidia wengine wanaokitafuta. Wanaohitaji kujua Kiswahili wanapaswa kupatiwa rasilimali mbalimbali zitakazowawezesha kukielewa na kukitumia kwa ufasaha zaidi na moja ya rasilimali hizo muhimu ni utaalamu huu wa ukalimani”, alisema Mhe. Bashungwa.

Alibainisha kuwa Serikali imenunua vifaa hivyo ikiwa ni utekelezaji wa malengo yanayohusiana na lugha ya Kiswahili yaliyomo katika ahadi za Serikali Bungeni na pia malengo yaliyomo katika Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2020-2025. “Vifaa hivi vitaliwezesha BAKITA kutoa mafunzo ya msasa na kuwasajili wakalimani watakaotumiwa katika mikutano mbalimbali ya ndani na nje ya nchi.

Waziri Bashungwa alifafanua kwamba Kiswahili kwa sasa kinatumika katika mikutano mbalimbali ya kimataifa kama vile katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) pamoja na Bunge la Afrika na Umoja wa Afrika.

“Ili Kiswahili kiendelee kutumika katika mikutano hiyo na mingine zaidi hapo baadaye, ni lazima kuwe na wakalimani wa kutosha watakaokuwa wanatoa huduma ya ukalimani kwa Kiswahili kutoka lugha mbalimbali za Kimataifa”, aliongeza Mhe. Bashungwa.

Aidha, aliagiza BAKITA kutumia vifaa hivyo kwa ajili ya kuwaandaa wakalimani wa kutosha ili nchi iwe na uwezo wa kuwapeleka katika mikutano mbalimbali kulingana na mahitaji ya kimataifa. 

Alitoa wito kwa Watanzania wenye utaalamu wa ukalimani na wanaojua ligha za kimataifa kama vile Kiingereza, Kireno, Kichina, Kifaransa, Kijerumani na Kiarabu kwenda BAKITA kupata mafunzo ya msasa ya kutumia vifaa hivyo na kusajiliwa ili Serikali iweze kutambua idadi yao na ili kuwatumia katika kazi mbalimbali ikiwemo kuwapeleka katika mikutano ya kimataifa pindi mahitaji hayo yatakapowasilishwa nchini.

Kwa upande wake, Kaimu Katibu Mtendaji wa BAKITA, Consolata Mushi alisema uwepo wa vifaa hivyo ni mafanikio makubwa sana katika taasisi hiyo hasa katika kipindi hiki ambacho taifa linajishughulisha na ubidhaishaji wa Kiswahili kwani Watanzania wenye weledi wa lugha ya Kiswahili wanaweza kupata fursa zitokanazo na lugha hii kitaifa na kimataifa.

“BAKITA litavitumia vifaa hivi kwa ajili ya kupima uwezo wa wakalimani tulionao nchini, na watakaothibitika kuwa na ubora watasajiliwa katika kanzidata ili Serikali na taasisi zake, asasi zisizo za Serikali pamoja na watu binafsi waweze kuwatumia katika mikutano mbalimbali ya kitaifa na kimataifa”, alisema Mushi.

Alivitaja vifaa hivyo kuwa ni pamoja na chombo maalumu kwa ajili ya kuchagua lugha na kuzungumza, seva, vipaza sauti, visikizi, spika, kikuza sauti na mashine ya mkalimani. 

Vifaa hivyo vina thamani ya shilingi milioni 187.5, ambapo Serikali kupitia BAKITA imenunua kizimba cha ukalimani kwa shilingi milioni 5.1 ili kuwezesha utendaji wenye ufanisi na pia Baraza limeandaa chumba maalumu kilichofungwa vifaa hivyo.

“Vifaa hivi vitawezesha jumla ya lugha nane kufanyiwa ukalimani kwa wakati mmoja na vinaweza kutumiwa na watu 30 kwa wakati mmoja,” aliongeza Mushi.

Pamoja na wakalimani kunufaika na vifaa hivyo, pia vitatumiwa na vyuo vikuu vya hapa nchini kwa ajili ya mafunzo ya ukalimani kwa vitendo na kuwawezesha kuimarisha zaidi uwezo wa wanafunzi katika taaluma ya ukalimani jambo ambalo litakuwa na faida kubwa kwa wanafunzi wenyewe, vyuo na taifa kwa ujumla.

Kaimu Katibu Mtendaji wa BAKITA, alitoa wito kwa wakalimani wote nchini waliopita kwenye mafunzo rasmi na wale wa nje ya mafunzo rasmi ambao wanajishughulisha na ukalimani, kuwasiliana na BAKITA, kwa ajili ya kufanikisha mpango huu madhubuti wa kuwapa mafunzo na kuwatambua.

Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Pauline Gekul amewahimiza BAKITA kuwa sasa ni wakati wao kufanya tafsiri ya kanuni na miongozo mbalimbali ya kisheria kwa lugha ya Kiswahili ili kuwawezesha Watanzania wengi kushiriki katika mambo yanayowahusu bila changamoto ya uelewa wa lugha.

No comments:

Post a Comment