SWEDEN YAIPATIA TANZANIA MSAADA WA SHILINGI BILIONI 118 KUNUSURU KAYA MASIKINI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Thursday 26 August 2021

SWEDEN YAIPATIA TANZANIA MSAADA WA SHILINGI BILIONI 118 KUNUSURU KAYA MASIKINI

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango na Mlipaji Mkuu wa Serikali Bw. Emmanuel Tutuba na Balozi wa Sweden nchini Tanzania Mhe. Anders Sjoberg wakiwaonesha wanahabari (Hawapo pichani) Hati ya makuliano ya msaada wa SEK milioni 450 sawa na sh. bilioni 118 za Tanzania zilizotolewa na nchi hiyo kwa ajili ya kusaidia Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini kupitia Mfuko wa TASAF, katika Ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania, Jijini Dar es Salaam.

Na Benny Mwaipaja, WFM, Dar es Salaam

SERIKALI ya Sweden imeipatia Tanzania msaada wa sarafu ya nchi hiyo (SEK) milioni 450 sawa na shilingi bilioni 118 za kitanzania kwa ajili ya utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini Awamu ya Pili kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii-TASAF.

Hati za makubaliano ya msaada huo zimetiwa saini Jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango na Mlipaji Mkuu wa Serikali Bw. Emmanuel Tutuba na Balozi wa Sweden nchini Tanzania Mheshimiwa Anders Sjöberg.

“Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini Awamu ya Pili ulianza kutekelezwa mwaka 2020 na unatarajiwa kukamilika mwaka 2023, umepangiwa kutekelezwa kwa gharama ya dola za Marekani milioni 883.3 sawa na shilingi trilioni 2.02 na Sweden imesaidia jumla ya dola na Marekani milioni 237 sawa na shilingi bilioni 542.2” alisema Bw. Tutuba.

Alisema kuwa mradi huo umelenga kuongeza fursa za kiuchumi na kijamii kwa kaya za walengwa pamoja na kulinda na kuimarisha rasilimali watu kwa kutoa ruzuku kwa kaya zilizoko kwenye mpango huo.

“Hadi kufikia Desemba 2020 zaidi ya kaya milioni 1 zilihakikiwa Tanzania Bara na Zanzibar na kuingizwa katika mpango huo huku kaya 56,800 kazi ya kuzihakiki inaendelea ili nazo ziweze kuingizwa kwenye mpango huo ulioonesha mafanikio makubwa” alisema Bw. Tutuba

Bw. Tutuba alieleza kuwa kuanzia mwezi Julai 2020 hadi Julai 2021, kaya za walengwa 871,654 zililipwa kiasi ha shilingi bilioni 171.8 kwa pande zote za Muungano na takwimu kuonesha kuwa ufukara ulipungua kwa asilimia 8 kwa walengwa.

Aliyataja baadhi ya mafanikio mengine ya mradi huo kuwa ni kuongezeka kwa idadi ya watoto wanaoandikishwa shule kutoka kaya za walengwa kwa asilimia 6, kuongezeka kwa mahudhurio ya watoto wenye miezi 0 hadi 24 kwenye vituo vya afya na kuongezeka kwa walengwa wenye nyumba bora za kuishi.

Alipongeza uhusiano imara uliopo kati ya Tanzania na Sweden na kwamba nchi hiyo inafadhili Miradi na program zinazoendelea ambazo thamani yake inafikia kiasi cha SEK bilioni 2.76 sawa na shilingi bilioni 723.2 na miradi na program zilizokamilika kwa ufadhili wa Sweden zinafikia kiwango cha SEK bilioni 2.59 sawa na shilingi bilioni 677.2.

“Kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa Serikali ya Sweden kwa msaada huu muhimu ambao unaendana na Mapango wetu wa Maendelo wa Miaka Mitano” Alisema Bw. Tutuba

No comments:

Post a Comment