BENKI ya NMB imetoa msaada wa viti 50, meza 50 kwa shule ya Sekondari ya Mkugilo na madawati 62 kwa Shule ya Msingi Chatembo, wilayani Mkuranga, Pwani vyote vikiwa na thamani ya Sh. Milioni 10.
Msaada huo, ulitolewa katika hafla iliyofanyika viwanja vya Shule ya Sekondari Mkugilo na Meneja Mahusiano, Biashara za Serikali wa NMB Kanda ya Mashabiki, Aneth Kwayu kwa niaba ya NMB na kumkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Khadija Nasser Ally.
Akizungumza katika hafla hiyo Aneth alisema kuwa NMB inazitazama changamoto za Sekta ya Elimu kama moja ya vipaumbele vyake vikuu, kutokana na ukweli kuwa elimu ndio ufunguo wa maendeleo sio tu ya mtu mmoja mmoja, bali pia kwa Taifa kwa ujumla- hivyo walivyopata maombi kuzisaidia shule hizi mbili waliona uhitaji na wamezisaidia.
NMB inatambua jitihada za Serikali katika kuboresha Elimu nchini na kama wadau wameahidi kuendelea kuunga mkono juhudi hizo za kusaidia jamii, ambayo wanamini ndiyo imeifanya NMB kuendea kuwa benki bora nchini.
“Tunawashukuru viongozi wa shule mbalimbali nchini wanavyoichagua NMB wanapokuwa na uhitaji, hii inaonesha kuwa mnathamini mchango wetu kwa maendeleo ya jamii. Na sisi tunafurahia kujitoa kwetu na tutahakikishia jamii inayotuzunguka inanufaika na faida tuipatayo," alisema Kwayu.
Akizungumza wakati akipokea msaada huo, Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Khadija Nasser Ally aliimwagia sifa NMB kwa namna ilivyojipambanua katika usaidizi na utatuzi wa changamoto za Sekta ya Elimu na Afya nchini, na kwamba yeye sio tu balozi mwema, bali pia ni shuhuda wa harakati chanya za benki hiyo katika kunyanyua elimu kote nchini.
Msaada huu, ni sehemu ya NMB kutatua changamoto zinazozikabili Sekta ya Elimu nchini lakini pia ni sehemu ya kurudisha kwa jamii sehemu ya faida baada ya kodi wanayoipata kila mwaka.
No comments:
Post a Comment