NAIBU WAZIRI MABULA AITAKA MANISPAA MPANDA KUANDAA MPANGO KAZI KUTEKELEZA MPANGO KABAMBE - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Wednesday, 21 July 2021

NAIBU WAZIRI MABULA AITAKA MANISPAA MPANDA KUANDAA MPANGO KAZI KUTEKELEZA MPANGO KABAMBE

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akikata utepe kuzindua ukumbi wa halmashauri ya Manispaa ya Mpanda jana mkoani Katavi uliojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akionesha Mpango Kabambe wa Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi mara baada ya kuuzindua jana.


Na Munir Shemweta, KATAVI

NAIBU Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya makazi Dkt Angeline Mabula ametoa wito kwa halmashauri ya na Wadau wa maendeleo katika halmashauri ya Manispaa ya Mpanda kuandaa mkakati na mpango kazi wa utekelezaji mpango kabambe.

Dkt Mabula alitoa wito huo tarehe 20 Julai 2021 wakati wa uzinduzi wa Mpango Kabambe wa Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi uliofanyika kwenye ukumbi wa halmashauri mkoani humo.

Aidha, aliitaka halmashauri ya Manispaa ya Mpanda kutafuta wabia na wawekezaji kwa ajili ya kuwekeza kwenye sekta mbalimbali zilizoainishwa kwenye Mpango Kabambe.

‘’Nitoe wito kwa taasisi zinazotoa huduma mbalimbali katika Manispaa ya Mpanda kuutumia Mpango Kabambe ulioandaliwa katika utekelezaji shughuli zao na miradi ya maendeleo’’ alisema Dkt Mabula

Aliitaka halmashauri ya Manispaa ya Mpanda katika mkoa wa Katavi kuendelea kuratibu utekelezaji Mpango Kabambe aliouzindua kwa kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo ya Manispaa.

Kwa mujibu wa Dkt Mabula, Kifungu cha 4 (3) cha sheria ya mipango miji ya mwaka 2007 kinazitaka Mamlaka za upangaji yaani Mamlaka za miji midogo, Manispaa na Majiji kuandaa ripoti za utekelezaji wa Mipango Kabambe na kuiwasilisha kwa Mkurugenzi wa Maendeleo ya Makazi kila mwaka na kubainisha kuwa ripoti hiyo haiwezi kutayarishwa bila ya kuwa na mipango na mikakati mahsusi ya utekelezaji.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda Michael Nzyungu kwa upande wake alisema, mkakati wa utekelezaji mpango kabambe wa Manispaa ya Mpanda 2018-2038 unatekelezwa kwa awamu tatu na kuainisha vyanzo vya mapato kwa ajili ya utekelezaji wake ni kutoka mapato ya ndani ya halmashauri.

Nzyungu alitaja vyanzo vingine kuwa ni kutoka serikali kuu, ubia na sekta binafsi, mifuko ya barabara pamoja na wafadhili mbalimbali.

Wakati huo huo, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amezindua na kuukabidhi ukumbi wa mikutano wa halmashauri ya Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi. Ukumbi huo umejengwa na shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kwa gharama ya shilingi milioni 367.

No comments:

Post a Comment