MAKANDARASI WASISITIZWA KUMALIZA MIRADI KWA WAKATI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Sunday 11 July 2021

MAKANDARASI WASISITIZWA KUMALIZA MIRADI KWA WAKATI

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, akimuelekeza jambo Mhandisi Mkazi Tadesse Dirba (Wakwanza kulia), wakati akikagua  mradi wa ujenzi wa barabara ya Kabingo- Kasulu hadi Manyovu, kipande cha Kanyani hadi Mvugwe (KM 70.5),  kinachojengwa na Kampuni ya Sinohydro Corporation Limited kwa kiwango cha lami.

Mhandisi Mkazi Khatibu Khamis, akimuelezea jambo Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya (wa tatu kushoto), wakati akikagua ujenzi wa barabara ya Kabingo, Kasulu hadi Manyovu (KM 260) mkoani Kigoma, kipande cha Mvugwe hadi Nduta (KM 59.35), kinachojengwa na Kampuni ya STECOL Corporation kwa kiwango cha lami.

NAIBU Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, amewataka Makandarasi wanaojenga miradi ya barabara nchini kuhakikisha wanafanya kazi usiku na mchana hususan katika kipindi cha kiangazi ili kukamilisha miradi kwa wakati.

Kasekenya ameyasema hayo wilani Kasulu, mkoani Kigoma, wakati alipokuwa akikagua maendeleo ya mradi wa barabara ya Kabingo- Kasulu- Manyovu yenye urefu wa kilometa 260.

Amefafanua kuwa kitendo cha kuongeza muda wa kufanya kazi kwa Makandarasi hao kutafidia muda watakaoupoteza wakati wa kipindi cha masika ambapo miradi ya barabara husimama kutokana na mvua.

"Nimepita kuangalia maendeleo ya mradi huu wa barabara yenye urefu wa kilometa 260 ambao unatekelezwa na makandarasi mbalimbali katika vipande vinne tofauti, nimefurahishwa na baadhi ya makandarasi hawa kujiongeza kwa kuamua kuongeza muda wa ufanyaji kazi, hii itasaidia hata miradi kukamilika kwa wakati, hivyo nawaagiza makandarasi wengine nao kuiga mfano huu”, amesema Kasekenya.

Aidha, amewataka Makandarasi na wasimamizi wa miradi hiyo kuzingatia viwango vya ubora wakati wa ujenzi wa miradi hiyo na kuhakikisha kuwa kila kilichoandikwa kwenye mchoro ndicho kinachofuatwa.

Amewasisitiza Makandarasi na wasimamizi wa miradi hiyo kubainisha changamoto zozote zinazowakabili ili zitatuliwe mapema wakati mradi ukiwa kwenye hatua za awali.

Amewahakikishia Makandarasi hao na wasimamizi wake kuwa Serikali itaendelea kutoa fedha kwa wakati ili kuhakikisha miradi haikwami kutokana na ucheleweshaji wa malipo.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Kasekenya wakati akimalizia ziara yake wilayani Kibondo mkoani humo, akiwa anakagua kipande cha Tatu cha barabara cha Mvugwe - Nduta Junction (Km 59.35) amesema kuwa kukamilika kwa barabara hiyo kutapunguza muda wa safari kutoka wilayani hapo kuelekea mikoa mingine kama vile Mwanza, Kagera na nchi jirani ya Burundi. 

Kwa upande wake, Mhandisi Mshauri kutoka kampuni ya Afrisa, ambao ni wasimamizi wa kipande cha barabara kutoka Kanyani - Mvugwe (Km 70.5) Reginald Kaganga,   amesema kuwa kipande hicho kinatekelezwa na Mkandarasi Sinohydro ambapo kazi zinazoendelea kwa sasa ni kusafisha, kujenga tuta na kuweka tabaka la mwanzo la barabara pamoja na ujenzi wa makalvati.

Nao wananchi wa Kasulu wamesema kuwa kukamilika kwa ujenzi wa barabara hiyo kutarahisisha huduma za usafiri na usafirishaji wa mazao na  hivyo kuweza kuyafikia kwa urahisi masoko ya ndani na nje ya nchi.

Barabara hii ya Kabingo- Kasulu- Manyovu yenye urefu wa kilometa 260 inajengwa kwa vipande vinne tofauti ambavyo ni Kasulu – Manyovu (Km 68.25), Kanyani – Mvugwe (Km 70.5), Mvugwe – Nduta Junction (Km 59.35) na Nduta Junction – Kabingo (Km 62.5)  ambapo ujenzi wa vipande hivi vyote unafadhiliwa na Benki ya maendeleo ya Afrika ( AfDB).

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi


No comments:

Post a Comment