Na Mwandishi wetu Dar es Salaam
NAIBU Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Mwanaidi Ali Khamis ameitaka jamii kushirikiana kikamilifu na wajane katika kupambana na ugonjwa wa Covid 19 nchini. Mhe. Mwanaidi ameyasema hayo leo katika kuadhimisha siku ya Wajane Duniani katika Viwanja vya Mnazi Mmoja, Mkoani Dar es Salaam.
Amesema kutokana na ugonjwa huo, uliosababisha ongezeko la wajane, bado wapo kwenye hatari zaidi kuliko makundi mengine kwani ndiyo wanahakikisha wanalinda afya ya watoto na familia kwa ujumla.
"Kaulimbiu hii inahimiza umuhimu wa makundi yote katika jamii kushiriki katika mapambano dhidi ya Covid 19 ikiwemo wajane kwa sababu imesababisha ongezeko la wajane duniani kwa kuwa idadi kubwa ya vifo imehusisha wanaume"
Mhe. Mwanaidi pia ameongeza kuwa idadi ya wajane 115 duniani bado wanakabiliwa na dhuluma, vitendo vya ukatili, wanatengwa na jamii na kuishi katika umaskini hivyo jamii inawajibu wa kuwalinda dhidi ya changamoto hizo.
Amesema Serikali inawatambua na kuwajali wajane na itaendelea kusimamia sheria inayowalinda hususani katika mgawanyo wa mirathi.
Naye Katibu Mkuu wa Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu amesisitiza jamii kuona umuhimu wa siku hii na kutafakari namna inavyowatendea wajane.
"Katika hatua zote za kupambana na Covid 19, Wajane washirikishwe kama kundi maalumu kwa kuwa ndilo linaathirika zaidi ya makundi mengine" amesisitiza Dkt. Jingu.
Kwa upande wake Rose Stewart ambaye ni Mkurugenzi wa Shirika la Wajane Tanzania TAWIA akisoma risala kwa niaba ya wajane, amesema kuwa bado wajane wengi wana changamoto za kutengwa na jamii hivyo kuishi maisha ya hofu.
Wakati huo huo, Mhe. Mwanaidi amezindua rasmi Kampeni ya Linda Ardhi ya Mjane yenye lengo la kuwasaidia wajane kuweza kumiliki ardhi.
Siku ya wajane huadhimishwa kila mwaka tarehe 23 Juni kutokana na azimio la Umoja wa Mataifa na kaulimbiu ya mwaka huu ni "Mapambano Dhidi ya CORONA, Wajane washiriki kikamilifu".
No comments:
Post a Comment