Na Godwin Myovela, Singida.
SHIRIKA la Maendeleo ya Elimu Mtinko (MEDO) lenye makao yake makuu mkoani Singida limetoa wito kwa serikali kuhakikisha vyanzo vya ndani vya mapato vinaimarishwa ipasavyo ili kuwasaidia watoto hususani wa kike na wenye mahitaji maalumu kuifikia elimu ya umma na jumuishi kwa ubora stahiki bila gharama yoyote.
Kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977 Ibara ya 11(2), inaeleza kuwa kila mtanzania anayo haki ya kujielimisha na kusoma ngazi zote za elimu hadi anapoamua kuacha yeye mwenyewe, hivyo elimu inayozingatia usawa na ubora stahiki bila ubaguzi kwa makundi hayo ni haki yao ya kikatiba.
Akizungumza mkoani hapa jana wakati akitoa mada za kujenga uwezo kwa makundi ya watoto wenye mahitaji maalumu, vijana na wadau wengine, sanjari na kutengeneza kikosi kazi kitakachofanya tathmini na kuangalia namna ya kuboresha kasoro zilizopo za uboreshaji elimu kupitia mradi wa 'Haki Kodi', Afisa Mradi kutoka MEDO Hashim Mruma alisema unyeti wa bajeti kwa kuangalia maboresho ya elimu hususani kwa makundi maalumu vinapaswa kupewa msukumo.
Mruma alisema ili kufikia lengo la mradi huo unaolenga kuondoa vikwazo, haki kodi na huduma za umma zenye kuzingatia/kujibu mahitaji ya jinsia-suala la ongezeko kubwa la mapato ya serikali kupitia rasilimali kodi na msukumo wa kuhakikisha kila anayepaswa kulipa kodi analipa havikwepeki.
Aliongeza kwamba hasa katika kipindi hiki cha bajeti upangaji wa bajeti ya serikali unapaswa kuzingatia unyeti wa mahitaji ya kijinsia na makundi maalum."Ni jukumu la jamii nzima kufuatilia mapato na matumizi ya fedha zao, kodi na ubora wa huduma za umma hasa elimu," alisema.
Hata hivyo, Mruma alikumbusha makubaliano ya mkutano wa dunia ulioketi Dakar Senegal mnamo mwaka 2000, pamoja na mambo mengine, wajumbe walikubaliana kuwepo na ongezeko la mgawo wa fedha inayotengwa kwenye bajeti Kuu ya nchi kwa ajili ya kutoa elimu, na bajeti husika inapaswa kuwa ni asilimia 20 ya bajeti nzima ya serikali ya mwaka husika, au asilimia 6 ya pato ghafi la ndani.
Mradi huo kwa mkoa wa Singida unahudumia shule zipatazo 20 ndani ya wilaya ya singida, kati ya hizo 3 ni sekondari na 17 ni shule za msingi, huku tathmini ya awali inaonyesha bado huduma za kielimu na miundombinu yake kwenye shule hizo hasa kwa watoto wenye ulemavu haijazingatiwa ipasavyo.
Mradi wa 'haki kodi' kitaifa unatekelezwa na Serikali ya Norway kupitia Wakala wake wa Maendeleo nchini humo (Norad), kwa kushirikiana na Mtandao wa Elimu nchini TEN/MET, huku MEDO ikibeba jukumu hilo kwa utekelezaji wa ngazi ya halmashauri ya Wilaya ya Singida.
Afisa mradi huyo alisema suala la utafiti na utambuzi wa utofauti wa mahitaji ya maboresho ya elimu kwa wanawake na wanaume yaani utoaji wa fursa za elimu kwa kuzingatia utofauti wa mahitaji- kwa wilaya ya singida bado ni changamoto.
" Kuhusu hili kila kitu kipo wazi, lengo namba 4 la Malengo Endelevu ya Kidunia (SDG4) ni kuhakikisha watoto na vijana wote wanajua kusoma, kuhesabu, na kutoa mazingira jumuishi ya kujifunzia kwa wote bila kujali jinsia na ulemavu," alisema Mruma na akaongeza;
"Mradi huu una malengo yake tarajiwa ikiwemo watoto wote hasa wenye ulemavu waweze kupata elimu ya umma bure ambayo inagharamiwa na serikali kwa vyanzo vya mapato ya ndani"
Kwa upande wake, Afisa Mipango na Fedha kutoka Medo, Michael Chegge alishauri miundombinu yote ya elimu inayojengwa izingatie mahitaji ya makundi maalumu.
"Tunakumbusha kwa wanaopewa kazi ya kutekeleza miradi ya elimu hasa ujenzi wa madarasa na muundo wa madawati vitekelezwe kwa kikidhi haja za watu wenye ulemavu," alisema Chegge.
Kwa upande wake, mdau wa shirika hilo, Patrick Mdachi, alisema licha ya jitihada kubwa zinazofanywa na watendaji wa mradi huo kwa takribani miaka zaidi ya mitatu sasa inasikitisha kuona watoto wanaendelea kusoma katika mazingira magumu.
"Ningeomba sana kupitia bajeti ya mwaka wa fedha unaoanza serikali itazame mateso ya watoto hawa hasa wenye mahitaji maalumu vinginevyo tutakuwa hatuwatendei haki," alisema Mdachi.
Mdau mwingine, Philbert Swai, alisema kwa uzoefu wake wa miaka mingi ameshuhudia shule nyingi za elimu jumuishi zilizojengwa kwenye ngazi ya Tarafa zinaitwa jumuisha lakini bado mifumo yake ni ile ile ya kuhudumia watoto wa kawaida.
Hata hivyo, Swai alishauri mabaraza ya madiwani kupitia kata husika wangeunganisha nguvu ili kusaidia kurekebisha miundombinu ya shule hizo kuwezesha watoto hao kusoma kwenye mazingira rafiki.
Mdau mwingine wa shirika hilo, Zawadi Gelard alionesha kusikitishwa na uwepo wa miundombinu mibovu ya kujifunzia kwenye shule ya Msingi Mgori iliyopo wilaya ya Singida.
"Tumefika eneo la shule lakini hakuna darasa lolote kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalumu, lakini kuna uhaba mkubwa wa madarasa watoto wamewekewa dawati wanasoma nje ya mlango wa ofisi ya Mwalimu Mkuu," alisema.
Alisema kero nyingine shuleni hapo na kwenye shule nyingine jirani ya Mtinko wilayani hapo ambayo wadau kwa mda mrefu wamekuwa wakizungumzia sana bila mafanikio ni uhaba wa mabweni kutokana na watoto wengi kuchelewa vipindi kutokana na kuishi maeneo ya mbali.
"Ninaomba serikali kupitia vyanzo vyake ichukue na kushughulikia changamoto hii kama dharula ili kuleta usawa na ustawi wa elimu ya watoto hawa na hasa wale wenye mahitaji maalumu," alisema Bi. Gelard.
Imeelezwa, pamoja na serikali kupeleka fedha ya ujenzi wa madarasa mawili na ofisi ya mwalimu kwenye shule hiyo ya Mgori lakini ujenzi wake bado hauendi kwa kasi kulingana na mahitaji yaliyopo.
"Madarasa hayatoshi, ni miongoni mwa shule jumuishi lakini haina mifumo ya elimu jumuishi, matundu ya vyoo vyake ni hatarishi kwa afya ya watoto na ni machache ikilinganishwa na idadi ya takribani wanafunzi zaidi ya 700 waliopo," alisema na kuongeza;
"Kwa sasa katika shule hiyo ofisi ya mwalimu wa Taaluma imegeuzwa kuwa bweni la wavulana na nyumba ya mwalimu imegeuzwa bweni la wasichana..tunaomba serikali izingatie haki ya utoaji elimu kadiri ya utofauti wa mahitaji"
No comments:
Post a Comment