Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akijaribu mashine maalumu ya kuoteshea alizeti, wakati alipokuwa akitembelea mabanda katika mkutano na wadau wa zao la alizeti, uliofanyika mkoani hapa leo. Kulia ni Meneja wa Wakulima Wadogo kutoka Kampuni ya Pyxus, Edwin Shio.
Waziri wa Kilimo Profesa, Adolf Mkenda, akizungumza kwenye mkutano huo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Andrew Masawe, akizungumza kwenye mkutano huo.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Singida, Alhaji Juma Kilimba, akizungumza kwenye mkutano huo. |
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiangalia, mbegu katika banda la Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA).
Na Dotto Mwaibale, Singida
"Hapa nchini kuna mazao na bidhaa ambazo hatujitoshelezi
hivyo kulazimika kuagiza kutoka nje ya nchi bidhaa hizo ni pamoja na mafuta ya
kula ambayo mahitaji yake yanakadiriwa kuwa ni tani 650,00 na uzalishaji wa
ndani ni wastani wa tani 290,000 sawa na asilimia 45 ya mahitaji kwa mwaka
hivyo, nchi hulazimika kuagiza wastani wa tani 360,000 hadi tani 400,000 kwa
mwaka kufidia upungufu huo ambapo hugharimu takribani Shilingi bilioni
474," alisema Majaliwa.
Majaliwa alisema kutokana na umuhimu wa mafuta ya kula, Serikali
imeweka mkakati wa kuongeza uzalishaji wa mazao ya mafuta yakiwemo chikichiki,
alizeti, pamba, karanga na ufuta ili kujitosheleza na kuondokana na uagizaji wa
mafuta kutoka nje ya nchi.
Alisema hatua za awali zilizofanyika ni kutekeleza mikakati
ya kuendeleza zao la michikichi kwa kuweka nguvu katika Mkoa wa Kigoma ambapo
kilianzishwa Kituo Maalum cha Utafiti wa Mchikichi cha Kihinga na kupitia
utafiti huo yameanza kuona matokeo makubwa ya uzalishaji wa miche bora yenye
uwezo wa kuzalisha mafuta kiasi cha wastani wa tani 5 kwa hekta ikilinganishwa
na aina ya michikichi ya zamani iliyopo sasa inayozalisha wastani wa mafuta ya
mawese tani 1.6 kwa hekta.
Majaliwa alisema kuwa hadi kufikia Mei, 2021 jumla ya mbegu 5,630,376
za chikichi na miche milioni 1.5 imezalishwa na kusambazwa katika Mikoa ya
Kigoma, Katavi, Kagera, Rukwa, Mbeya, Pwani na Ruvuma.
Waziri Mkuu Majaliwa alitumia nafasi hiyo kueleza kuwa Serikali
imeendelea kutoa kipaumbele cha kuendeleza sekta ya kilimo kuanzia ngazi ya
uzalishaji, viwanda na masoko na hiyo inatokana na ukweli kwamba takribani
asilimia 70 ya watanzania wanajishughulisha na kilimo na kuwa katika kipindi
hiki cha Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan
wameendelea kufanyia kazi changamoto zilizopo kwenye mazao ya kilimo hatua kwa
hatua kwa kuwasikiliza wadau, kupata maoni yao na kukubaliana mikakati thabiti
ya kuendeleza mazao katika mnyororo wa thamani.
Aidha alisema kuwa serikali mbali ya kuongeza kufanya
utafiti inatoa huduma za ugani, upatikanaji wa mbegu bora na viuatilifu,
kuongeza matumizi ya zana zana bora za kilimo, kuwajengea uwezo wazalishaji
kuhusu kanuni za kilimo bora, kuanzisha mfumo imara wa ugharamiaji wa mazao ya
mafuta kwa kushirikisha taasisi za fedha.
Alisema kufuatia hatua hiyo ni matarajio ya Serikali kuwa mikakati
hiyo itawezesha kuongeza uzalishaji kutoka wastani wa tani 649,437 hadi tani
1,500,000 za alizeti zitakazochangia upatikanaji wa mafuta kwa takribani tani
300,000 ifikapo mwaka 2025.
Alitaja mikakati mingine ya Serikali kuwa ni kuendelea kuwekeza
katika Taasisi zinazohusika na utafiti na uzalishaji wa mbegu ili kuongeza tija
na kuwa kwa kuzingatia umuhimu mbegu, Serikali imeongeza bajeti ya Taasisi ya
Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) kutoka Shilingi bilioni 7.35 mwaka 2020/2021
hadi Shilingi bilioni 11.63 mwaka 2021/2022. Vilevile, bajeti ya Wakala wa
Mbegu za Kilimo (ASA) imeongezeka kutoka bilioni 5.42 mwaka 2020/2021 hadi
Shilingi bilioni 10.58 mwaka 2021/2022 ili kuongeza upatikanaji wa mbegu bora
zikiwemo mbegu za mazao ya mafuta ya kula.
No comments:
Post a Comment