Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge. |
MKUU wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge amewaagiza viongozi na wadau wa vyama vya ushirika kusimamia mapato ya Halmashauri kupitia mazao yanayouzwa kwa mfumo wa stakabadhi ghalani kwa lengo la kuongeza tija na maduhuli ya Serikali.
RC Ibuge ametoa agizo hilo wakati anazungumza katika kikao maalum cha Baraza la madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Songea cha kujadili Hesabu za Mkaguzi Mkuu wa Serikali kwa mwaka wa fedha 2019/2020.
Amesema kuwa, mapato ya Serikali na wakulima yamekuwa yanapotea kwa sababu ya usimamizi na ufuatiliaji mdogo,kwa baadhi viongozi kutosimamia ipasavyo mazao yanayopaswa kuuzwa kwa mfumo wa stakabadhi ghalani,kitendo kinachosababisha Halmashauri kukusanya chini ya kiwango kilichokusudiwa.
Ameagiza madiwani na watendaji kusimamia kwa umakini mkubwa uuzaji na ununuzi wa mazao ya wakulima kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani, ili waweze kuuza mazao hayo kwa bei yenye tija,na wakulima kunufaika na kilimo wanacholima badala ya kulanguliwa mazao yao.
”Mfumo wa stakabadhi ghalani ni matakwa ya Ilani ya CCM,kipengele cha 34(i) kinazungumzia wakulima kuuza mazao ya stakabadhi ghalani,pia umetolewa mwongozo wa mazao yanayotakiwa kuuzwa kwenye mfumo huu”,amesisitiza RC Ibuge.
Amesikitishwa na kitendo cha baadhi ya walanguzi wa mazao maeneo ya vijijini kununua ufuta kilo moja kwa shilingi 500 kwa kila wakati kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani kilo moja inauzwa shilingi 1400/=
Mfumo wa stakabadhi ghalani unawataka wakulima wa ufuta soya na mbaazi kuuza mazao yao kwenye vyama vya msingi vya ushirika (AMCOS).
Hata hivyo baadhi ya wakulima wamezitaja changamoto wanazokutana nazo katika mfumo huo ni kutembea umbali mrefu, gharama za kukodi vyombo vya usafiri kwa ajili ya kufikisha mizigo kwenye vyama vya msingi vya ushirika na kufanyika kwa mnada mara moja kwa wiki.
No comments:
Post a Comment